Heko Rais Dkt.Samia, mcheza kwao hutunzwa

NA DR.JUMA MOHAMMED

IKIWA imesalia wiki moja kabla ya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jamii ya Wanazuoni inaona umuhimu wa kumtunuku Udaktari wa Falsafa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima Novemba 30, 2022 ikiwa ni Shahada ya Udaktari wa Juu katika Humanitia na Sayansi Jamii na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.

Unapozungumzia kutulia kwa siasa za Tanzania katika zama hizi jina la Dkt.Samia halitaweza kuwekwa kapuni, litawekwa peupeni, litunzwe na kuhenziwa na kila mpenda haki, demokrasia na umoja.

Kuzikwa kwa siasa za kushupaliana, vitisho, ubabe, kuimarisha sekta ya elimu, kuongeza nguvu ya bajeti katika sekta ya kilimo, kuimarisha uhusiano na mataifa ya nje ni miongoni mwa mambo makubwa ambayo yanamuweka katika historia nzuri Rais Dkt.Samia.

Akiwa Rais wa Awamu ya Sita, Rais Dkt.Samia mara tu alipoingia Ikulu amehimiza na amekuwa muumini juu ya kuheshimu haki za binadamu,uvumilivu wa kisiasa na kuhimiza siasa za kileo zenye kuzingatia hoja badala ya porojo,fujo na ubabe.

Katika kuthamini jitihada zake, falsafa zake katika ujenzi wa Tanzania mpya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeamua kumpa heshima kubwa na ya kipekee kwa kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa.

Novemba 30, 2022 katika Viunga vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vilisheheni watu wa kila rika, kike kwa kiume.

Wananchi na jamii ya wanazuoni walifika kushuhudia tukio muhimu katika historia ya nchi yetu kwa kiongozi wetu kutunukiwa kiwango hicho cha elimu kwa kuthamini mchango wake kwa umma.

Shahada ya Udaktari wa Uzamivu- PhD ya heshima katika Falsafa aliyotunukiwa Dkt.Samia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imebadili wasifu na kuandika historia mpya ya Rais Dkt.Samia na wananchi wa Tanzania.

Kwa nini Chuo Kikuu kimemtunuku Shahada ya Uzamivu katika Falsafa Rais Dkt.Samia?. Katika utaratibu wa Vyuo Vikuu duniani, mtu anayetunukiwa Shahada ya aina hii mara nyingi anakuwa ni mtu wa kipekee, mwenye sifa njema, muungwana, mchakapazi ambaye amefanya na anaendelea kufanya mambo makubwa na ya msingi katika jamii na ambaye rekodi yake ya haki za binadamu inakuwa isiyoshaka na katika kuwatumikia raia wenzake.

Rais Dkt.Samia anaingia katika rekodi ya utendaji bora na uliotukuka akionesha ushupavu wa uongozi, akionesha uwezo na uhodari sio tu katika kutawala uwanja wa siasa, bali hata katika uhusiano wetu na mataifa ya nje.



Ingawa wapo watakaosema haya na yale, lakini ukweli utabaki kuwa hivyo maana kila aliye na macho anaona umakini wake, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo imetafsiriwa katika mipango ya maendeleo ya Serikali ni uthibitisho wa dhamira njema ya Rais Dkt.Samia.

Malezi aliyopata Rais Dkt.Samia kwa wazazi wake, ndani ya CCM katika jamii na Serikalini yanamfunga kutokuwa kiongozi mbabe, Rais Dkt.Samia si kiongozi mwenye makeke, kama walivyo viongozi wengine katika mataifa mbalimbali tuliopata kuwaona au kuwasikia katika tawala zao.

Rais Dkt.Samia si mtu mwenye visasi, chuki, si mtu wa kujilimbikizia mali,katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kama angekuwa kiongozi tamaa basi leo ungesikia miguno kutoka kwa wananchi kuwa "ahaa jumba lile la Samia, kiwanda kile cha mwanawe" licha ya kuwa pengine mwanawe anastahiki kuwa hivyo, lakini watu wasingefahamu hivyo.

Hakuna hata chembe ya shaka kuwa Rais Dkt.Samia na familia yake si katika viongozi wanaokumbatia mali, kwake yeye utumishi wa umma ni muhimu zaidi.

Kwa hakika, Rais Dkt.Samia ni Rais makini, mchapakazi na aliyetayari kujifunza kutoka kwa wengine, wawe wakubwa, wadogo na hata wafanyakazi wa kawaida, kwake yeye urais si kikwazo cha kuongeza weledi katika uongozi na katika siasa.

Umakini na umahiri katika kuongoza nchi ulianza kujitokeza katika siku 100 za mwanzo, namna anavyoshughulikia matatizo ya kijamii, anavyokerwa na tabia za ubabe na wizi wa mali za umma, anavyowajibika katika kusimamia utekelezaji wa maagizo yake, unatoa mwanga wa kule tuendako.

Maendeleo ya Tanzania ndiyo kipaumbele chake, imekuwa dira ya uongozi wake itakayompa muongozo wa kusimamia yale yaliyoainishwa kwenye Ilani na mwelekeo wa Sera za CCM wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Pengine isingelitosha kwa Rais Dkt. Samia kuwa na mawazo chanya peke yake bila kuwa na nia ya kuyatimiza yale anayoyaamini.

Wataalam wa Tasnia ya uongozi wanasema kwamba kuna wakati malengo yanakumbana na vikwazo, hivyo ni wajibu wa Kiongozi kusimamia uamuzi sahihi na kuwa mtu wa mwisho.

Rais Dkt.Samia si katika aina ya viongozi wanaofuata hisia zao, au vionjo vyake; hofu, woga, wasiwasi, hasira, chuki, kinyongo havina nafasi katika utawala wake.

Kwa mnasaba huo, tumeshuhudia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, moja katika vyuo vyenye kuheshimika Kimataifa na kikiwa miongoni mwa vyuo vyenye hadhi ya juu, kikimtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa. Heko Rais Dkt.Samia, mcheza kwao hutunzwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news