Hii ni historia katika Sekta ya Habari nchini-Msigwa

NA GODFREY NNKO

ZAIDI ya wadau 1,000 wa habari nchini wakiwemo viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali,wanahabari, wamiliki wa vyombo vya habari, mabalozi na sekta binafsi wamekusanyika jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 nchini Tanzania.

Kongamano hilo linafanyika leo Desemba 17, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamnhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan la wadau wa vyombo vya habari kukutana ili kujadiliana kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Akizungumzia kuhusu kongamano hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa amefafanua kuwa,hili ni kongamano la kwanza nchini ambalo ni kiashiri chema kwa sekta hiyo nchini tunapojiandaa kuupokea mwaka mpya wa 2023.

"Hii ni siku ya kihistoria katika nchi yetu, tumelianzisha tukio la kihistoria ambalo hatujawahi kuwa nalo tangu nchi yetu izaliwe (ipate Uhuru).

"Kwa sisi wanahabari hii itakuwa ndiyo Krisimasi yetu, ndiyo mwaka mpya wetu, ndiyo funga mwaka yetu. Kwa hiyo ni siku muhimu sana na nina furaha kuona leo tumeungana na Mheshimiwa Waziri wetu kuianza safari hii muhimu katika Sekta ya Habari,"amefafanua Msigwa.

Desemba 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza na kuendelea kuwa sehemu ya Jumuiya ya Madola na mwaka 1962 Tanganyika ikawa Jamhuri. Tanganyika iliungana na Zanzibar tarehe 26 Aprili 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa zaidi ya miaka 60 sasa,Sekta ya Habari Tanzania inaonekana kuchanua zaidi licha ya changamoto za hapa na pale ambazo Serikali hususani hii ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi hasa upande wa sheria ambazo zinaonekana kuwa na utata.

Lengo likiwa ni kuiwezesha sekta hii muhimu ambayo ni muhimili wa nne wa Serikali ambao si rasmi uweze kukidhi matarajio yake ya kuhudumia wananchi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.

Ikumbukwe, mwaka 1993 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuona umuhimu wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, iliamua kufungua milango na kuruhusu kuanzishwa kwa runinga, redio na magazeti ya binafsi.

Kamisheni ya Utangazaji ilianzishwa Novemba 1993 chini ya Mwenyekiti wake,Mark Bomani na kuanza majukumu ya kupokea maombi na kutoa leseni za redio na televisheni, kufuatilia na kusimamia urushaji wa matangazo ya redio na televisheni pamoja na kufuatilia na kutoa masafa kwa vyombo vya utangazaji vya binafsi.

Mafanikio hayo ndiyo yalifungua safari ya kuikuza sekta hiyo ambayo mpaka sasa hapa nchini kuna mamia ya magazeti/machapisho, redio, runinga na blogu zilizosajiliwa rasmi.

Hivi karibuni Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) kuelekea mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 walipendekeza mambo mbalimbali.

Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Pia wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Aidha, wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2) (b) (lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.

Katika hatua nyingine, Msigwa amefafanua kuwa,kongamano hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Kongamano hili linawakutanisha watu takribani 1000 wanaotoka katika taasisi na maeneo mbalimbali yanaohusiana na vyombo vya habari, tumekutana kwa nia moja la kujadili maendeleo ya Sekta ya Habari.

"Kongamano hili ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa katika wakati wa Maadhimiso ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani,ambapo kwa hapa nchini yaliadhimishwa kwa mkutano wa wadau wa habari uliofanyika Arusha, Mei 3, 2022.

"Mheshimiwa Rais alituagiza kukutana na wadau wote wa vyombo vya habari kujadiliana kuhusu maendeleo ya Sekta ya Habari nchini. Ninayo furaha kwamba tumelitekekeza agizo hili kabla ya mwaka kuisha,"amefafanua Msigwa. 
 
Tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news