HIZI HAPA SALAMU ZA WAZIRI WA AFYA, MHE.UMMY MWALIMU ZA SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2023, ATOA ANGALIZO KUHUSU UVIKO-19



Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu.

Ndugu wananchi, tukiwa katika msimu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, Wizara ya Afya inawatakia wananchi wote Heri ya Krisimasi na Mwaka Mpya 2023.

Kama tunavyofahamu Mtu ni Afya, hivyo nitumie fursa hii pia kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza ikiwemo magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.

Kwa mujibu wa taarifa zetu, katika kipindi cha kati ya wiki ya kwanza ya Mwezi Novemba na wiki ya pili ya Desemba 2022 kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa.

Ufuatiliaji wa wizara umeonesha kuwa, visababishi vikuu vya magonjwa haya ni virusi vya UVIKO-19 pamoja na virusi wengine wenye kusababisha mafua na kikohozi mfano virusi vya Influenza (Influenza viruses).

Ndugu wananchi, wagonjwa wa UVIKO-19 wameongezeka kutoka asilimia 4.1 hadi asilimia 5.5 ambapo takwimu za Wiki ya kwanza ya Mwezi Novemba 2022 zinaonyesha kuwa watu 1,154 waliopima UVIKO-19, kati yao watu 47 walikuwa wanaugua UVIKO-19 huku takwimu za Wiki ya pili ya Mwezi Desemba 2022 zinaonyesha kuwa, kati ya watu 1,294 waliopima UVIKO-19, watu 71 walikuwa wanaugua UVIKO-19.

Wagonjwa wa Influenza wameongezeka kutoka asilimia 4.8 hadi asilimia 6.5 (kati ya watu 277 waliopima Influenza katika Wiki ya kwanza ya Mwezi Novemba 2022,watu 11 walikuwa wanaugua ugonjwa huo huku takwimu hizo hizo pia katika Wiki ya pili ya Mwezi Desemba zinaonyesha kuwa kati ya watu 155 waliopima, watu 10 walikuwa wanaugua ugonjwa wa Influenza.

Kutokana na hali hii, wizara inaendea kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua ili kujikinga na magonjwa haya ikiwemo :-
i) Kupata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO-19 kwa ambao hawajachanja. Hatua hii itawaepusha kupata ugonjwa mkali wa UVIKO-19 na hata kifo,
ii) Kuvaa barakoa pindi mtu anapokuwa na dalili za mafua au kikohozi; na awapo kwenye mikusanyiko,
iii) Kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara.
iv) Kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuzingatia kanuni za afya na usafi binafsi ikiwemo kujikinga kwa kitambaa au kiwiko cha mkono wakati wa kupiga chafya au kukohoa.

Ndugu wananchi, vile vile tunaendelea kuwakumbusha kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa kwa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara angalau mara tatu kwa wiki kwa muda usiopungua dakika 30, kuzingatia lishe bora na ulaji wa vyakula unaofaa pamoja na kupunguza unywaji wa pombe na vilevi vingine.

Aidha, pindi mtu anapohisi ugonjwa wowote kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu pamoja na kutoa taarifa za kuwepo kwa watu wenye dalili za magonjwa ya kuambukiza katika jamii yetu kupitia namba ya simu ya bure 199.

Ndugu wananchi, sambamba na kuchukua tahadhari ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza, ninatoa rai kwa watumiaji wote wa vyombo vya moto barabarani katika kipindi hiki cha sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, kuchukua tahadhari ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo au ulemavu wa kudumu na kuipa Serikali mzigo mkubwa wa kuhudumia wahanga.

Takwimu za Taasisi ya Mifupa MOI za kipindi cha Julai hadi Septemba 2022 zinaonyesha kuwa wagonjwa wa ajali walikuwa 2,410 na kati yao asilimia 70 walikuwa ni wagonjwa kutokana na ajali za barabarani.

Ndugu wananchi, wakati tunaufunga mwaka huu wa 2022, tathmini ya utendaji wa Sekta ya Afya chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpenda maendeleo, mwenye maono na kujali watu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasssan inaonyesha kuwa tumepiga hatua zaidi katika kuboresha huduma za afya nchini.
 
Ikiwemo kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kutoa huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa, kuimarisha upatikanaji wa dawa katika Bohari ya Dawa (MSD) na katika vituo vya kutoa huduma, kununua vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine za uchunguzi za CT SCAN kwa Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini pamoja na Xray na vifaa tiba vinginevyo katika Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Kanda, Taifa na Hospitali Maalum.

Aidha, tumeweza kuongeza Idadi ya Watumishi wa Afya katika ngazi zote sambamba na kuanzisha Mpango wa Mafunzo ya Ubingwa na Ubingwa Bobezi kwa Wataalam wa Sekta ya Afya unaojulikana kama Samia Health Super Specialization Program ambapo Mpango huu katika mwaka 2022/23 utazalisha wataalam 457 wa kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi katika nchi yetu.
Ndugu wananchi, kwa mwaka 2023 tunaahidi kuendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi, vipaumbele vyetu vikuu vikiwa ni:-
i) Kuimarisha Ubora wa Huduma za Afya ili wananchi wapate huduma bora za afya kwa wakati na katika mazingizira bora na rafiki.
ii) Kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za Afya bila ya kikwazo cha fedha kupitia utaratibu wa Bima ya Afya kwa Wote. Hivyo ninatoa rai kwa wananchi kujiunga na skimu mbalimbali za Bima ya Afya ili kuwa na Uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

Mwisho, ninapenda kuwashukuru watumishi wote wa Sekta ya Afya nchini kuanzia ngazi ya Msingi hadi Taifa, Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii pamoja na Wadau wote wa Maendeleo ya Sekta ya Afya kwa kuwa mstari wa mbele katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Tuendelee na kazi hii ya kuwahudumia watanzania kwa kuzingatia Weledi, Maadili, Utu na Upendo kwa Wagonjwa. Na kwa watanzania wenzangu Tuungane pamoja kuzilinda afya zetu na za wenzetu kwa mustakabali wa maendeleo yetu, jamii zetu na ya Taifa kwa ujumla.

Mtu ni Afya, Jali Afya Yako
NINAWATAKIA HERI YA SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2023
Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news