IBARA KUMI NA NANE MBILI

NA ADELADIUS MAKWEGA

KATIKA mila za Kiafrika safari za kwenda kwa Waganga wa Jadi ni sehemu ya maisha ya iwe kwa ugonjwa, kuhisi kufanyiwa mabaya au kwenda kubashiri mambo yajayo (kupiga ramli).

Safari hizi huwa mbili kwa nne, moja kwenda na kurudi (kupokea maelekezo) na ya pili kwenda na kurudi (kutimiza maelekezo ya mganga).

Kwanza unapofika anakupigia ramli anakwambia shida yako na namna ya kuitatua, maagizo yatatolewa kalete hiki na kile mathalani leta kuku mweupe, hapo unarudi kwenu kumtafuta kuku huyo.

Pili kuku kwapani hadi kwa mganga.“Hodi tumerudi, jana tulifika hapa ulituagiza kuku mweupe ni huyu hapa ili kuitatua ile shida yetu.”

Hapo sasa mganga anawatibu huku mkipokea maelekezo, yakishatolewa jukumu la mpokeaji ni kutekeleza bila ya kuyakosea. Kupona kwa mgonjwa ni kufuata maagizo kwa usahihi.

“Familia ile ilipata shida hii kwa kuwa babu yao alikosea masharti ya mganga.” Kwa upande mwingine wapo wanapokea maelekezo wa waganga yanawashinda na kuondoka wakibaki na yanayowasibu.

Mara zote mganga yeye ni bingwa wa maagizo kwa kuwa yeye amepewa ujuzi (utaalamu wa kutibu) mgonjwa kwa kuwa nia yake ni kupona na ameaminishwa kuwa anaweza kupona kwa mganga fulani hana budi awe mnyonge ili apate nafuu aweze kurudi kuendelea na shughuli zake zinazomuingizia kipato.

Katika jamii za Kiafrika wapo ambao ni mabingwa ya kuyakamilisha masharti ya waganga viwavyo na iwe.“Yule mtoto mdogo lakini bingwa wa shiriki, yule mshirikina sana na ndiyo maana anafanikiwa.”

Wapo wengine nusu dini nusu ushirikina na wapo wengine hawapo kabisa huko ushirikinani wapo kwenye dini tu.

Jambo hili linaleta migogoro mikubwa katika familia za Kiafrika mgonjwa akiumwa tu makundi matatu haya yanaibuka wengine wanasema kalogwa wangine wanaamini nusu kwa nusu na wengine hawaamini kabisa.

Huu mseto unaleta tabu kubwa na jamii kugombana, kununiana na kuacha kuzikana kwa kushikana uchawi

Leo mwanakwetu ana nini? Jambo hilo mwanakwetu analilinganisha fika na Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini Tanzania maana wengine hawaamini kabisa katika uhuru wa vyombo vya habari, wengine wanaamini katika uhuru huo na wengine wapo kote kote wazee wa njia panda kama zile za familia nyingi za Kiafrika katika ushirikina.

Desemba17, 2022 Waziri wa Habari na Tekinolojia ya Habari nchini Tanzania ndugu Nape Nnauye akifungua Kongamano ya Maendeleo ya Sekta ya Habari aliungama wazi wazi mbele ya wanahabari na wadau wa habari zaidi 1000 juu ya yeye kuwa muumini wa uhuru wa habari na alikwenda mbali zaidi na kusema haya,

“Naomba kukumbusha kuwa hakuna maendeleo, hakuna amani, hakuna furaha katika jamii kama Uhuru wa Habari katika jamii hiyo haupo.”

Waziri huyu aliirudia sentensi hiyo huru mara mbili katika kongamano hilo kuonesha umuhimu wa jambo hilo.

Mwanakwetu hilo anakubaliana nalo asilimia zote, lakini kidole chake cha shahada anakinyanyua juu kulenga ajenda za kongomano hilo na hotuba ya Waziri Nape juu uumini wake wa Uhuru wa Habari kama hili la kwenda kwa mganga lenye misuguano mingi.

“Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.” Ibara ya 18-2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake inatukumbusha.
Kwa bahati nzuri mwanakwetu anakumbuka waziri huyu si mgeni katika wizara hii tangu ikiwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, hapa kuku mweupe wa kupelekwa wa mganga aliingia doa Januari 27, 2016.

Mheshimiwa Nape Nnauye (Spika Job Ndugai aliita) wabunge walishangilia. Karibu mheshimiwa endelea (Spika Job Ndugai alisema).

“…Mheshimiwa Spika ! Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), lilianza kurusha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005, kabla ya kuanza kurusha moja kwa moja TBC wakati huo Televisheni ya Taifa ilikuwa inarekodi matukio yote ya Bunge na kurusha usiku katika vipindi maalumu vilivyojulikana kama Bungeni Leo, kwa maana yaliojili ndani ya ukumbi wa Bunge kwa siku husika.

Baada ya kuanza kwa utaratibu wa kurusha matangazo moja kwa moja mwaka 2005 gharama za kuifanya kazi hiyo zimekuwa zikipanda kwa kasi hadi kufikia shilingi bilioni 4.2 kwa mwaka kwa maana mikutano minne ya Bunge.

Shirika limekuwa likigharamia sehemu kubwa ya matangazo hayo kwa kutumia mapato yake yanayopatikana kutoka matangazo madogo madogo ya biashara , ifahamike kuwa 75% ni vipindi vingi vinayolenga kutoa elimu kwa umma na asilimia 25 ni burudani.

Mheshimiwa Spika kutokana na hali hii TBC imeona kuwa ni busara kubadilisha mfumo wa utangazaji wa shughuli za Bunge ili kukabiliana na kuzidi kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Hivyo basi TBC imeona ni busara kuanzia mkutano huu wa Bunge iwe inarusha baadhi ya matangazo ya Bunge moja kwa moja, ikiwa ni njia ya kubana matumizi.

Chini ya utaratibu huu TBC itahakisha kuwa baadhi ya matangazo ya Bunge yatarushwa moja kwa moja na mengine kurekodiwa na kuandaliwa kipindi maalumu kitakachoitwa Leo katika Bunge.

Kipindi hichi kitakuwa kitakuwa na mambo yote muhimu yaliyojiri ndani ya Bunge kwa siku husika na kipindi hiki kitakuwa kinarushwa kuanzia saa 4 usiku hadi saa 5 usiku.

Kipindi hicho kimeanza tarehe 26 Januari 2016 yaani jana na tayari baadhi ya wananchi wameoneshwa kuridhishwa na utaratibu huu na kuwa na kipindi cha Bunge usiku kikishungulikia shughuli za Bunge.

Mheshimiwa spika uamuzi huu utapunguza gharama za uendeshaji wa shirika na pia kwa kupitia kipindi cha Leo Katika Bunge Watanzania walio wengi watapata nafasi ya kufahamu yalijiri Bungeni, kwani wakati Bunge linaendelea na mijadala yake Watanzania walio wengi huwa wana kazi za kiofisi au zingine za ujenzi wa taifa kwa maali walipo, Mheshimiwa Spika nakushukuru.”

Mwanakwetu analipiga chapuo la kila mmoja wetu kuukata uduma kuwili katika Uhuru wa Habari Tanzania maana Ibara 18-2 ilishamaliza kueleza kila kitu.Sote tukumbuke Februari 14, 1967 Mwalimu Julius Nyerere alisema haya,

“Misingi ya Ujamaa ni kuamini umoja wa binadamu, na kwamba katika historia ya binadamu watu huanguka pamoja na huinuka pamoja. Ndiyo kusema kwamba msingi wa Ujamaa ni usawa wa binadamu.”

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news