NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imeweka mikakati ya kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji katika safu ya milima ya Wota na Wangi yenye uwezo wa kuhudumia nusu ya Wilaya ya Mpwapwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb), Mhe.George Simbachawene akiongoza kikao kilichoweka maazimio kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene katika kikao kazi kilichohusisha viongozi katika ngazi ya wilaya kata na kijiji katika Jimbo la Kibakwe lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kilichokuja na maazimio ya kutokomeza vitendo vya uharibifu wa mazingira.
“Vijiji vilivyo katika Kata ya Luhundwa, Kibakwe na Kingiti vyenye jumla ya watu takribani 60,000 vinategemea maji kutoka kwenye safu ya milima Wota na Wangi ambazo zinajulikana kama Lugundalule au Igombo. Vyanzo hivyo vinachezewa, watu wanalima, wanakata miti na wanaingiza mifugo.
"Tumeshindwa kudhibiti na kukamata watu wanaojihusisha na vitendo vya uharibifu wa mazingira na hata wakikamatwa wakipelekwa mahakamani wanalipa faini tu na kurudi kuharibu vyanzo vya maji.
“Tusipolinda vyanzo hivi vya maji vikaharibiwa kama hali jinsi ilivyo hivi sasa ndani ya miaka michache ijayo wananchi watakosa huduma ya maji. Tumekubaliana katika mambo kadha kwenye kikao ambayo yatasimamiwa katika utendaji wake.’’
Akichangia katika kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mhe.Richard Maponda amesema, viongozi wa chini wakikamata watu wanaoharibu mazingira wakifika wilayani wanarudishwa kwa kigezo kwamba sheria hazijakaa vizuri.
"Uharibifu wa mazingira unafanyika kama biashara, tunayo haki ya kuchukua hatua za kuanzia, kwa ngazi yetu na kwa nafasi zetu. Linapokuwa jambo kubwa ndipo tunaomba msaada.
“Maeneo ya vyanzo vya maji hayajapimwa, hivyo kusababisha watu wanaojihusisha na shughuli za kilimo kuingia mpaka kwenye hifadhi ya vyanzo vya maji.”
Naye Mhe.Sophia Chidalamai amesema, lazima wawe na ushirikiano wakati wa kutoa ushahidi mahakamani wa watu wanaojihusha na uharibifu wa mazingira.
“Lazima tuwafahamu watuhumiwa wa uharibifu wa mazingira na kisha kuandaa ushahidi kwa watendaji wa kata, watendaji wa kijiji, mwenyekiti wa kitongoji pamoja na askari polisi.”
Naye Mtendaji Kata wa Kibakwe, Bw.Baraka Zebedayo amesema, wanaofanya uharibifu wa mazingira ni watu werevu na wanajua wanachokifanya ni kosa, wanatumia watumishi ambao sio waaminifu kuharibu ushahidi.
“Wakati mwingine hata kupewa taarifa ya kesi inasomwa lini ili tuweze kutoa ushahidi, huwa hakuna, matokeo yake wahalifu wakishaenda wilayani wanarudi."
Tags
Habari
Halmashauri za Tanzania
Jimbo la Kibakwe
Kataa Uhalifu Uishi Salama
MAENDELEO JIMBONI
Wilaya ya Mpwapwa