NA LWAGA MWAMBANDE
NI wazi kuwa,alama za barabarani zina umuhimu mkubwa iwe kule vijijini na hata mijini. Kwani, alama hizo zinatoa maelekezo na pia kuonya ili kuepusha ajali za mara kwa mara ambazo huwa zinasababisha maafa kwa jamii na hata Taifa.
Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa,upuuzaji wa alama za barabarani mara kwa mara husababisha ajali za barabarani, hivyo ni wajibu wetu kutii sheria bila shuruti.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,ni jukumu letu kuhakikisha tunazipa kipaumbele cha kwanza alama hizo ikiwemo sehemu iliyochorwa mistari mieupe ambayo ndiyo rasmi ya kuvukia barabara, kwa wale wanaotembea kwa miguu, endelea;
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,ni jukumu letu kuhakikisha tunazipa kipaumbele cha kwanza alama hizo ikiwemo sehemu iliyochorwa mistari mieupe ambayo ndiyo rasmi ya kuvukia barabara, kwa wale wanaotembea kwa miguu, endelea;
1. Mimi ninawaambia, dharau sijesikia,
Alama kutotumia, barabara kifikia,
Ajali tajikatia, matanga yakatujia.
Cheki kivukomilia, barabara kutumia.
2. Wamekurahisishia, hicho kivukomilia,
Na tena wamezidia, alama nyingine pia,
Fika na kuangalia, kichwakichwa utalia,
Cheki kivukomilia, barabara kutumia.
3. Vyombo vya moto sikia, barabara kitumia,
Vizuri kuangalia, kwenye kivukomilia,
Siyo mnajipitia, na fujo kutufanyia,
Cheki kivukomilia, barabara kutumia.
4. Alama kuzingatia, wakati mwajipitia,
Waenda miguu pia, hapo tutafurahia,
Ajali nazosikia, hizo zote taishia,
Cheki kivukomilia., barabara kitumia.
5. Mjini ukipitia, kama wanazingatia,
Vile ukiangalia, watu wengi watumia,
Huko kusijefifia, huko mbele kipitia,
Cheki kivukomilia, barabara kitumia.
6. Ajali ninakwambia, uzembe unachangia,
Alama dharaulia, kienyeji jipitia,
Hasara tunaingia, hali mali tunalia,
Cheki kivukomilia, barabara kitumia.
7. Sehemu nyingine pia, watoto wanapitia,
Taratibu nakwambia, usije kuwaingia,
Tukabali tunalia, hatari ikiingia,
Cheki kivukomilia, barabara kitumia.
8. Elimu tunasikia, wenyewe watupatia,
Uangalie kulia, kushoto tena kulia,
Barabarani ingia, pale unapopitia,
Cheki kivukomilia, barabara kitumia.
9. Hayo tukishikilia, pia kufuatilia,
Pazuri tutafikia, ajali zitafifia,
Vilio vitatulia, ajali kujitakia,
Cheki kivukomilia, barabara kitumia.
10. Alama zikififia, hatari itatujia,
Hivyo kivukomilia, ni muhimu kuchapia,
Ili tunapoingia, hatari sijetujia,
Cheki kivukomilia, barabara kitumia.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Tags
Habari
Kiswahili
Kivukomilia
Safiri Salama
Usalama kwa Watembea kwa Miguuu
Zebra Crossing
Zingatia Usalama Barabarani