Kocha wa Ghana, Otto Addo ajiuzulu

NA DIRAMAKINI

KOCHA wa Ghana,Nana Otto Addo amethibitisha kuwa, ataondoka baada ya timu hiyo kutolewa kwenye Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) siku ya Ijumaa, baada ya kusema kabla ya michuano hiyo nchini Qatar kuwa, hatabaki baada ya hapo.

Kocha wa Ghana, Otto Addo anaonekana mwenye huzuni baada ya kuondolewa kwenye Kombe la Dunia wakati wa mechi ya mwisho ya Kundi H kati ya Ghana na Uruguay kwenye Uwanja wa Al Janoub mnamo Desemba 2, 2022. (Picha na John Sibley/Reuters).

Nana Otto Addo mwenye umri wa miaka 47 ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana ambaye alizaliwa Ujerumani na kuichezea Black Stars katika mechi yao ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006.

Ghana ilikuwa timu ya kwanza ya Afrika kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar baada ya kulazimishia Nigeria sare ya 1-1 jijini Abuja na kusonga mbele kwa kanuni ya bao la ugenini.

Hata hivyo, mashabiki wa Nigeria walizua vurugu mwishoni mwa mechi hiyo kwa kurushia wachezaji na maafisa wa Ghana chupa za maji walipokuwa wakiondoka uwanjani.

Kiungo mkabaji wa Arsenal, Thomas Partey aliwaweka Ghana kifua mbele katika dakika ya 10 kabla ya beki wa Watford, William Trost-Ekong kusawazisha kupitia penalti baada ya Ademola Lookman kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku.

Ghana na Nigeria walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo ya marudiano baada ya kuambulia sare tasa katika mkondo wa kwanza mjini Kumasi mnamo Machi 25, 2022. Aidha, Black Stars ya Ghana haikufuzu Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

Ingawa uzoefu wake pekee wa awali wa kufundisha ulikuwa ni timu za vijana za Hamburg na Borussia Dortmund, Nana Otto Addo alikuwa na meneja wa zamani wa Newcastle United na Brighton &Hove Albion FC, Chris Hughton kama mshauri wake wakati Ghana ikipata bahati yake kuiondoa Nigeria kwa nafasi ya Qatar.

"Nilisema hapo awali, ilikuwa wazi ningesimama baada ya Kombe la Dunia. Kwa sasa, mimi na familia yangu tunaona mustakabali wetu upo Ujerumani, napenda nafasi yangu huko Dortmund," Addo alisema baada ya Ghana kuondoka kwenye michuano hiyo kufuatia kufungwa 2-0 na kupoteza kwa Uruguay kwenye Uwanja wa Al Janoub.

"Nilisema nitajiuzulu baada ya Kombe la Dunia hata kama tungekuwa mabingwa wa Dunia," aliongeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news