KORONA: Mtambo ni wa maana, Mkonge fao ni nyuzi

NA LWAGA MWAMBANDE

MKONGE au kwa jina lingine katani ni mojawapo ya mazao yaliyoonesha mafanikio makubwa katika mikoa ya Tanga, Morogoro na hivi karibuni wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kutokana na kuhimili hali ya ukame ambayo huwa ni changamoto kubwa kutokana na uhaba wa mvua.

Aidha,uzalishaji wa mkonge nchini Tanzania ulianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 na Kampuni ya Afrika Mashariki ya Ujerumani.

Mkonge ulizalishwa kwa namna endelevu katika tawala za Ujerumani na Uingereza na ndio usafirishaji mkubwa zaidi wa koloni uliothaminiwa sana kwa matumizi ya kamba na mazulia duniani.

Juhudi za uzalishaji huo hata baada ya Uhuru ziliendelea ingawa si kwa ukubwa huo wa miaka ya nyuma, ni kutokana na ukweli kwamba, hili ni zao la biashara ambalo nyuzi zake hutumika katika kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo ni muhimu katika maisha ya kila siku ya mwananchi.

Kitaalamu, majani ya mkonge wa Tanzania yana urefu wa mita moja na kwa wastani unaweza kuishi miaka 13 hadi 14 na idadi ya majani yake yanaweza kufikia 200 hadi 300 katika maisha yake.

Majani hayo yanaweza kutumika katika kutengenezea bidhaa mbalimbali kama vile kamba, mazulia, magunia, mafuta ya kulainisha mitambo, viatu na hata mavazi.

Aidha, mbali ya bidhaa hizo, pia makapi ya majani ya mkonge hutumika kama chakula cha mifugo hasa ng’ombe ambacho kimeonesha kuwa na lishe nzuri na wakati mwingie hutumika kutengezea sukari.

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasema kuwa, ili kupata matokeo bora kupitia zao la mkonge kama enzi za ukoloni, kuna umuhimu wa kuwekeza vilivyo katika kilimo hicho na mitambo ya kisasa, endelea;

1.Hapa tumepata shida, uzalishaji hakuna,
Mambo siyo kawaida, vile tulivyopatana,
Mzigo kupata shida, hapa twatarifiana,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

2.Korona kwetu muhimu, mtambo ni wa maana,
Vile unalo jukumu, mkonge kuchanachana,
Lengo tena yetu hamu, ni nyuzi kupatikana,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

3.Oda tuliyoipata, uzalishaji hakuna,
Hasara tunaipata, vile mtambo hatuna,
Kwa kweli yametukuta, kuharibika korona,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

4.Uwekezaji muhimu, mbele huko ninaona,
Tujenge korona humu, tena kwa kuhimizana,
Moja kiingia sumu, nyingine tafaa sana,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

5.Mkonge fao ni nyuzi, pale tunapouchana,
Mtambo kufanya kazi, ndiyo waitwa korona,
Lakini ukila pozi, ndio tunaangushana,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

6.Wawekezaji nchini, hebu jengeni korona,
Zienee mashambani, nyuzi tuzalishe sana,
Pesa zetu na kigeni, tuzipate nyingi sana,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

7.Mchakato kamilika, mkonge pata korona,
Hiyo ndiyo yatumika, nyuzi tuweze ziona,
Tuzidi kuchakarika, matunda tutayaona,
Korona kuharibika, hatuwezi pata nyuzi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news