KWIKA!!!:Hebu kwika hilo jembe, shamba linakusubiri

NA LWAGA MWAMBANDE

SEKTA ya Kilimo nchini inachangia zaidi ya asilimia 26 ya pato la taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu huku ikisaidia kuongeza mapato na kuboresha maisha.

Katika kuhakikisha wakulima wanaweza kuongeza uzalishaji mbegu na mavuno mengi,Serikali imekuwa mstari wa mbele kuweka mazingira wezeshi ambayo yanamfanya mkulima kufurahia kazi ya mikono yake.

Mathalani, Aprili 6, 2022 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023 bungeni jijini Dodoma alisema,Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maboresho makubwa katika Sekta ya Kilimo.

Waziri Mkuu alisema,mwezi Desemba 2021, Serikali ya Awamu ya Sita iliipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania mtaji wa shilingi bilioni 208 ikiwa ni nyongeza kwenye mtaji wa awali wa shilingi bilioni 60 uliowekwa na Serikali wakati wa uanzishwaji wa benki mwaka 2012.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, Serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha mkulima anafaidika kupitia kazi ya mikono yake huku akisisitiza kuwa,haupaswi kufanya uzembe wa kutokwenda shambani. Endelea;

1. Nakuona una jembe, tena unao mpini,
Usijefanya uzembe, wa kutokwenda shambani,
Kesho njaa ikukumbe, uombeombe njiani,
Hebu kwika hilo jembe, shamba linakusubiri.

2. Ya kwako malalamiko, jembe halina mpini,
Kwa sasa hayo hayako, ushaletewa mpini,
Vipi kuchelewa huko, ili uende shambani?
Hebu kwika hilo jembe, shamba linakusubiri.

3. Endapo jembe unalo, unatafuta mpini,
Au na shoka unalo, haujakwika mpini,
Ujue unalo hilo, havikufai shammbani,
Hebu kwika hilo jembe, shamba linakusubiri.

4. Kama una jembe kwika, litakufaa shambani,
Kama una shoka kwika, nenda safisha shambani,
Wala usijebweteka, takufaa njaa nyumbani,
Hebu kwika hilo jembe, shamba linakusubiri.

5. Kuna jembe la kukwika, hilo lafaa shambani,
Lingine la kuchomeka, pia lafaa shambani,
Ili kuweza tumika, tuitumie mipini,
Hebu kwika hilo jembe, shamba linakusubiri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news