MAELEZO YA MHE.WAZIRI MKUU KUHUSU UTEKELEZAJI WA ILANI 2022

MAELEZO YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI KUHUSU UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CHAMA CHA MAPINDUZI YA MWAKA 2020 KWA KIPINDI CHA NOVEMBA 2020 HADI OKTOBA 2022

Ndugu Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Ndugu Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Ndugu Abdulrahman Omari Kinana, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Bara;

Ndugu Daniel Godfrey Chongolo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi;

Ndugu Dkt. Philip Isdor Mpango, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Ndugu Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;

Ndugu Christina Solomon Mndeme, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Bara;

Ndugu Dkt. Abdallah Juma Saadala, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar;

Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa;

Ndugu Viongozi Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Ndugu zetu Wenza wa Viongozi mliopo hapa;

Ndugu Wajumbe kutoka Vyama vya Siasa Rafiki; na

Waheshimiwa Mabalozi kutoka nchi mbalimbali mliopo hapa;

Mabibi na Mabwana.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

UTANGULIZI

1. Ndugu Mwenyekiti, ninaomba kuanza maelezo yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutufikisha siku hii ya leo tukiwa salama na wenye afya njema.

2. Ndugu Mwenyekiti, leo tunaandika historia nyingine ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mkutano Mkuu huu wa 10 kwa kuwa kikao hiki ni cha kwanza kupokea Taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020.

3. Ndugu Mwenyekiti, Ilani tunayoitekeleza ni ya mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo CCM imeielekeza Serikali kutekeleza maeneo makuu sita ya kipaumbele yafuatayo: -

Mosi: Kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu;

Pili: Kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi;

Tatu: Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi;

Nne: Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini;

Tano: Kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi; na

Sita: Kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.

UTEKELEZAJI WA ILANI (NOVEMBA 2020 HADI OKTOBA 2022)

4. Ndugu Mwenyekiti, taarifa hii itabainisha hatua iliyofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2022. 

Wasilisho hili ni muhtasari wa taarifa ya kina iliyopo katika vitabu viwili vikubwa ambavyo kila mmoja wetu amepatiwa. 

Taarifa hizo zimegusa maeneo mbalimbali ikiwemo: Afya, Elimu, Maji, Utalii, Kilimo na Umwagiliaji, Miundombinu ya Barabara, Reli, Madaraja, Bandari, Viwanja vya Ndege na Ukusanyaji wa Mapato.

5. Ndugu Wajumbe, ninaungana na wenzangu kukupongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupata Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa kutokana na mafanikio yako katika mageuzi ya kiuchumi, uimarishaji wa misingi ya demokrasia, utawala bora na maendeleo ya jamii.

6. Ndugu Mwenyekiti, mchango wako katika kuliongoza Taifa hili kwa weledi, ukomavu na kujenga matumaini mapya kwa Watanzania umeleta chachu mpya ya kulijenga Taifa letu na kusaidia tupate mafanikio ya haraka.

7. Ndugu Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, mafanikio makubwa na ya haraka yamepatikana katika nyanja na sekta zote. Ninaomba kutumia nafasi hii kuwaeleza kwa kifupi baadhi ya mafanikio.

a) Ukusanyaji wa Mapato

Ndugu Mwenyekiti, Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026) ukiwa na dhima ya Kujenga Uchumi Shindani wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. 

Chini ya uongozi wako mahiri na kuhimiza ulipaji kodi kwa hiari, ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeendelea kuongezeka hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.74 kwa mwezi ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.46 kwa mwezi mwaka 2020/2021. 

Aidha, hadi Agosti, 2022 mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kubaki kwenye tarakimu moja.

b) Elimu

Ndugu Mwenyekiti, katika kutekeleza Ilani ya CCM, Serikali yako imeendelea kutekeleza mpango wa kutoa elimu ya msingi na sekondari bila ada ikiwemo ada za mitihani na hivyo kuimarisha uandikishaji na uhitimu wa wanafunzi shuleni.

Ndugu Mwenyekiti, ni jitihada zako zilizowezesha kupatikana fedha za kujenga vyumba vya madarasa 12,000 katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa 3,000 katika vituo shikizi na kufanya uandike historia mpya katika nchi hii ambapo kwa mara ya kwanza, wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa saba mwaka 2021 walipata nafasi ya kuanza kidato cha kwanza Januari, 2022 bila kuwa na chaguo la pili.

Ndugu Mwenyekiti, ujenzi wa shule za wasichana katika mikoa yote 26 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 na 1,200 ambao watakuwa wanasoma masomo ya sayansi ni mpango mkakati wa kuongeza fursa kwa watoto wa kike nchini. 

Nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kuridhia kutenga shilingi bilioni nne kwa kila shule kwa mikoa 10 ya kwanza nchini katika bajeti ya mwaka huu na ujenzi unaendelea.

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea kugharamia elimu ya juu ambapo katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2022, imetoa mikopo ya shilingi trilioni 1.03 kwa wanafunzi 327,175 wa vyuo vya elimu ya juu.

c) Kilimo na Huduma za Ugani

Ndugu Mwenyekiti, ili kuimarisha sekta ya kilimo, umefanya maamuzi ya kimapinduzi kwa kuridhia ongezeko la bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023. 

Tarehe 4 Aprili, 2022 hapa hapa mkoani Dodoma, ulikabidhi vitendea kazi kwa maafisa ugani wote nchini zikiwemo pikipiki 2,000, vifaa vya kupima afya ya udongo 143, simujanja 384 na visanduku vya ufundi 3,400 vya maafisa ugani. 

Aidha, ili kuhakikisha upatikanaji wa mbolea na kuongeza tija katika uzalishaji kwa wakulima, uliridhia ruzuku ya shilingi bilioni 150 ili isaidie kushusha bei ya mbolea na kwa sasa usambazaji unaendelea kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

d) Kukuza Demokrasia

Ndugu Mwenyekiti, demokrasia popote pale duniani huwa ina misingi na taratibu ambazo Taifa husika limejiwekea. 

Dhamira yako ya dhati ya kuweka mazingira mazuri ya demokrasia na siasa hapa nchini, imejidhihirisha kupitia sera ya upatanishi, kuvumiliana, kuishi pamoja na kujenga nchi uliyoipa jina la R4 yaani Reconciliation, Resiliency, Reforms and Rebuilding of the nation. Hii imejenga mazingira ya demokrasia nzuri na inayoendana na hali halisi ya Kitanzania.

Ndugu Mwenyekiti, tarehe 21 Oktoba 2022 ulipokea taarifa ya Kikosi Kazi ambayo imebainisha masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusisha kutungwa kwa sheria mpya, marekebisho ya sheria mbalimbali na kanuni. 

Serikali inafanyia kazi masuala hayo kwa kuzingatia mpango kazi na hatua za mapitio ya ngazi za maamuzi ndani ya Serikali.

e) Uhusiano wa Kimataifa

Ndugu Mwenyekiti, tangu uingie madarakani, umeimarisha uhusiano na mataifa mengine zikiwemo nchi jirani hususan za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Kutokana na juhudi zako, baadhi ya Marais na Wakuu wa Nchi waliotembelea Tanzania ni Waheshimiwa Yoweri Museveni (Uganda), Felix Tshisekedi (Jamhuri Kidemokrasia ya Congo), Filippe Nyusi (Msumbiji), Evariste Ndayishimye (Burundi), Hakainde Hichilema (Zambia) na William Ruto (Kenya). 

Aidha, wewe binafsi umefanya ziara katika nchi za Marekani, Ubelgiji, Ufaransa, Qatar, Uganda, Ghana, Uingereza, Msumbiji, China, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Scotland, Malawi, Rwanda na Burundi.

8. Ndugu Mwenyekiti, maelezo ya kina kwa maeneo yote haya yamewasilishwa kwenye makala fupi ambayo ninaomba wote sasa tuitazame:-

A. UCHUMI

Ukusanyaji wa Mapato

Ndugu Mwenyekiti, ukusanyaji wa mapato umeongezeka ambapo kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 wastani wa mwezi ulikuwa ni shilingi trilioni 1.74 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.46 kwa mwaka 2020/2021.

Uwekezaji na Viwanda

Ndugu Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia uwekezaji katika viwanda vitakavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini ili kukuza pato la mwananchi, kupunguza umasikini na kuongeza ajira. 

Baadhi ya viwanda vilivyozinduliwa hivi karibuni ni kiwanda cha kuzalisha sukari cha Bagamoyo, kiwanda cha kusafishia madini ya dhahabu cha Geita, na kiwanda cha kuchambua pamba cha NGS, Ifukutwa, kilichopo wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi.

Uzalishaji wa Ajira

Ndugu Mwenyekiti, moja ya ahadi ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020 ni kuzalisha ajira zipatazo milioni nane katika kipindi cha miaka mitano. 

Katika kutekeleza Programu ya Kukuza Ajira kwa Vijana ambayo ni jumuishi katika sekta zote, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kutekeleza miradi ya kimkakati, kutoa mafunzo ya ujuzi na kutoa mikopo yenye masharti nafuu, ajira 1,381,618 zimezalishwa kwa Watanzania kupitia sekta ya umma na binafsi.

Ndugu Mwenyekiti, vilevile, Serikali imehakikisha miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini inatoa ajira, kuwanufaisha wazawa na kuwajengea uwezo ili kukidhi vigezo vya ajira hizo. 

Jitihada hizo zimewezesha miradi ya kimkakati kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana 97,832 na zisizo za moja kwa moja 377,000 kwa vijana wenye ujuzi mahiri, ujuzi wa kati na wasio na ujuzi.

B. MIUNDOMBINU

Barabara na Madaraja Makubwa

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha barabara na ujenzi wa madaraja makubwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji. 

Kipindi cha Novemba, 2020 hadi Oktoba, 2022 Serikali imejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 950.29. 

Aidha, Serikali iliendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara mijini na vijijini zenye urefu wa kilomita 50,373.23 ambapo barabara za kiwango cha changarawe ni kilomita 9,989.36 na matengenezo ya kawaida na sehemu korofi ni kilomita 22,045.68.

Ndugu Mwenyekiti, vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa madaraja makubwa ya Kitengule (Kagera), Daraja Jipya la Wami (Pwani), Daraja la Msingi (Singida) na Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza). Ujenzi wa Daraja la Tanzanite (Dar es Salaam) na Daraja la Kiyegeya (Morogoro) umekamilika.

Reli

Ndugu Mwenyekiti, mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) unaendelea na hadi kufikia Novemba, 2022 kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (Km 300) kimefikia asilimia 97.49 na Morogoro – Makutopora (km. 422) asilimia 90.07, Mwanza – Isaka (km. 341) asilimia 14.2 na Makutupora – Tabora (km. 368) asilimia 1.92 ilhali ujenzi wa kipande cha Tabora - Isaka chenye urefu wa km. 165 umeanza. 

Utengenezaji wa mabehewa unaendelea vizuri. Kati ya mabehewa 81, mabehewa 36 yamekamilika na 14 kati ya hayo yaliwasili bandari ya Dar es Salaam tarehe 22 Novemba, 2022. Mabehewa 45 yaliyobakia, yanategemewa kukamilika Machi, 2023.

Bandari

Ndugu Mwenyekiti, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za upanuzi wa bandari za Dar es Salaam na Tanga na katika Ziwa Tanganyika kwenye bandari za Kibirizi (Kigoma), Karema (Katavi) na Kabwe Mkoani Rukwa ili kuongeza ufanisi katika huduma. 

Hadi Oktoba 2022, ujenzi wa gati 1-7 katika Bandari ya Dar es Salaam unaohusisha kuongeza kina, kujenga Gati Maalumu (RoRo berth) ya kuhudumia meli za magari na kujenga yadi ya kuhudumia makasha (container yard) umekamilika. 

Vilevile, Serikali imeboresha bandari ya Tanga kwa kuongeza kina cha lango la kuingilia na kugeuzia meli.

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea na upanuzi wa bandari ya Kibirizi (Kigoma) ili kuchochea biashara na nchi jirani za Congo (DRC), Zambia na Burundi. Pia ujenzi wa bandari ya Kabwe Mkoani Rukwa umekamilika, na utakuwa kivutio kikubwa cha biashara baina ya Wilaya ya Nkasi na eneo la Moba nchini Congo.

Ndugu Mwenyekiti, pia ujenzi wa bandari ya Karema iliyopo mkoani Katavi umekamilika na imeanza kutumika. 

Ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 47.9, ukihusisha ujenzi wa kivunja mawimbi, mlango bandari na gati ya meta 150 zenye uwezo wa kulaza meli zenye urefu wa mita 75 na upana wa mita 15, uchimbaji na uwekaji wa kina wa mlango wa bandari, jengo la ofisi, jengo la abiria na shehena ya jumla.

Usafiri wa Anga

Ndugu Mwenyekiti, katika sekta ya anga, Serikali imeendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Songea mkoani Ruvuma na Nduli mkoani Iringa. 

Kwa uwanja wa ndege wa Songea, ujenzi na ukarabati wa jengo la kuongozea ndege upo katika hatua za mwisho na wanakamilisha uwekaji wa taa ili kuwezesha ndege kutua usiku. Katika kiwanja cha ndege wa Nduli, upanuzi wa kiwanja hicho unahusisha ujenzi wa barabara za kutua na kurukia ndege.

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili liweze kutoa huduma bora ya usafiri wa anga ndani na nje ya nchi. Hivi sasa limefanikiwa kuanza safari za Arusha, Geita, na kurejesha safari za Mtwara na Songea. 

Pia, limerudisha safari za kikanda katika vituo vya Bujumbura, Entebbe, Harare, Lusaka na Hahaya pamoja na kuanzisha vituo vipya vitatu katika miji ya Lubumbashi, Nairobi na Ndola. 

Vilevile, Shirika limerejesha safari ya kimataifa kwenda Mumbai - India pamoja na kuanzisha safari za mizigo na abiria kuelekea Guangzhou – China.

Ujenzi wa Meli

Ndugu Mwenyekiti, ili kuboresha usafiri wa majini, Serikali inaendelea na ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ambao umefikia asilimia 73. Pia ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika na meli mpya ya kubeba mabehewa (wagon ferry) katika Ziwa Victoria unaendelea.

C. NISHATI

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua madhubuti kuimarisha sekta ya nishati ili kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Hatua hizo zilijumuisha kuendelea na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project - JNHPP) ambao umefikia asilimia 77.15 na unatarajia kuzalisha MW 2,115.

D. KUKUZA UTALII

Uzinduzi wa filamu ya ROYAL TOUR

Ndugu Mwenyekiti, utalii ni sekta muhimu ya uchumi yenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kulinda na kuhifadhi rasilimali na kuendeleza utalii nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza na kutangaza vivutio vya utalii.

Ndugu Mwenyekiti, takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa sekta ya utalii inazidi kuimarika zaidi hususan baada ya uzinduzi rasmi wa programu maalumu ya The Royal Tour uliofanyika tarehe 19 Aprili, 2022 nchini Marekani. 

Na hadi kufikia Septemba 2022, takwimu zinaonesha kuwa watalii wanaokuja nchini Tanzania wameongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 na kufikia 1,034,180. 

Pia, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka dola za Marekani milioni 714.59 (sawa na shilingi trilioni 1.6) kwa mwaka 2020 na kufikia dola za Marekani bilioni 1.3 (sawa na shilingi trilioni 3) katika mwaka 2021.

Ndugu Mwenyekiti, Novemba 2022, Tanzania ilipokea meli kubwa ya kitalii ya Zaandam kutoka Florida, Marekani ikiwa na watalii 1,060 kutoka mataifa ya Marekani na Ulaya na wafanyakazi 520 kutoka mataifa 35 duniani. 

Vivutio vya utalii tulivyonavyo vimeifanya sekta hii kuwa mhimili muhimu wa uchumi na sasa Tanzania imeanza kuwa kitovu cha utalii wa mikutano (conference tourism) ambapo hivi karibuni tumeweza kuwa wenyeji wa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani - Kamisheni ya Afrika. 

Pia tulikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Mikutano hii ilifanyika jijini Arusha.

Ndugu Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa na kuibua masoko mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini hadi kufikia watalii milioni tano na mapato ya dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.

Kulinda Hifadhi ya Ngorongoro

Ndugu Mwenyekiti, ili kulinda ikolojia na uoto wa asili katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), Serikali imefanikiwa kuwaratibu wakazi wanaohama kwa hiari katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga. 

Zoezi la kuandikisha wakazi wanaoomba kuhama kwa hiari linaendelea vizuri. Aidha, hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2022 jumla ya kaya 1,524 zenye watu 8,715 na mifugo 32,842 zilikuwa zimekwishajiandikisha. 

Aidha, kati ya tarehe 16 Juni, 2022 na tarehe 15 Novemba, 2022 makundi 16 yenye kaya 489 zenye watu 2,629 na mifugo 14,132 zilikuwa zimeshahamia katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni. 

Katika maeneo ambayo wakazi hao wamehama kwa hiari, uoto umeanza kurejea katika hali ya awali huku wanyama wakiongezeka na watalii wanaotembelea eneo hilo pia wameongezeka.

E. MAJI

Miradi Mikubwa Mitano

Ndugu Mwenyekiti, katika kuimarisha sekta ya maji nchini, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama. Hadi kufikia Oktoba 2022, ujenzi wa miradi mikubwa mitano ya Tabora-Igunga-Nzega; Orkesumet; Kagongwa-Isaka; Longido na Misungwi ilikuwa imekamilika. Aidha, vijiji 171 vilivyopo kandokando ya miradi hiyo, vilikuwa vimeunganishwa na huduma ya maji.

Miradi ya Maji katika Miji 28

Ndugu Mwenyekiti, tarehe 6 Juni 2022, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji ya miji 28. Miji itakayonufaika na miradi hiyo ni Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa-Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Chunya, Rujewa, Wangingo’mbe, Makambako, Njombe, Kiomboi, Singida, Manyoni na Chemba. 

Miji mingine ni Chamwino, Mugumu, Kasulu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga pamoja na ukanda wa Makonde. Utekelezaji wa miradi hiyo ni mojawapo ya mikakati ya Serikali ya kusambaza maji safi na salama maeneo ya mijini na vijijini. 

Aidha, kiwango cha upatikanaji wa majisafi na salama mijini kimeongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2020 hadi asilimia 86 mwaka 2022 na vijijini kutoka asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 74.5 mwaka 2022.

Ujenzi wa Bwawa la Kidunda

Ndugu Mwenyekiti, mwaka huu, umeandika historia mpya kwa kuridhia zitolewe shilingi bilioni 100 kati ya shilingi bilioni 329 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu muhimu unaotarajiwa kuchukua miezi 36 hadi kukamilika. 

Pamoja na mradi huu, Serikali inaendelea na taratibu za awali za ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwa gharama ya shilingi bilioni 292 ili kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma na miji ya Bahi, Chemba na Chamwino.

F. KUHAMIA DODOMA

Awamu ya Pili ya Ujenzi wa Mji wa Serikali

Ndugu Mwenyekiti, Serikali ilifanya uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma. Ili kutimiza azma hiyo, shilingi bilioni 300 zilitolewa kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa Mji wa Serikali unaohusisha majengo ya ofisi yenye urefu wa ghorofa kuanzia sita hadi 11 ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha Serikali inahamishia shughuli zake Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma.

Ndugu Mwenyekiti, ujenzi huo ambao umefikia asilimia kati ya 50 na 70, unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2023 na utaenda sambamba na uwekaji wa miundombinu ya maji, umeme, mawasiliano, usalama, gesi, TEHAMA, zimamoto na uokoaji na programu za upandaji miti. 

Lengo ni kuwa na mji wa Serikali wa kisasa utakaozingatia dhana ya mji wa kijani na mji rafiki ili kudhibiti gharama za uendeshaji. Ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 51.2 katika eneo hilo umekamilika kwa asilimia 99.

Ndugu Mwenyekiti, sambamba na hatua hizo, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Jiji yenye urefu wa kilomita 112.3 ambapo sehemu ya Nala -Veyula – Mtumba - Ihumwa Dry Port ni kilomita 52.3 na sehemu ya Ihumwa Dry Port -Matumbulu - Nala ni kilomita 60. Ujenzi huu utakapokamilika, utakuwa umegharimu shilingi bilioni 230.4.

Ndugu Mwenyekiti, ili kuboresha Jiji la Dodoma kwa mawasiliano ya anga, Serikali imeanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambapo barabara ya kuruka na kutua ndege imeanza kujengwa.

Ndugu Mwenyekiti, katika kuhakikisha shughuli zote za Serikali zinafanyika makao makuu ya nchi, kwa dhamira ya dhati kabisa, Serikali iliamua kujenga Ikulu mpya ya Chamwino, Dodoma. Na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

G. UKAGUZI WA MIRADI YA NDANI

Ndugu Mwenyekiti, ili kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi unaenda sambamba na maono yake, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akifanya ziara za kukagua miradi ya ndani na kuzungumza na wananchi ili kutatua kero zao papo kwa papo. 

Kutokana na ziara hizo, miradi mingi ya maendeleo imezinduliwa na kuwasaidia wananchi kupata huduma za msingi zikiwemo maji, umeme, barabara na afya.

H. Sensa

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imekamilisha kwa mafanikio makubwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022. Sensa hiyo ni ya kihistoria katika nchi yetu kwa kuwa ni ya kidigitali na ilijumuisha Sensa ya Watu, Majengo na Anwani za Makazi. Taarifa ya awali ya matokeo ya Sensa iliyozinduliwa tarehe 31 Oktoba, 2022 inaonesha kuwa idadi ya watu ni 61,741,120. 

Kati ya hao, watu 59,851,347 wapo Tanzania Bara na 1,889,773 wapo Zanzibar. Kwa upande wa majengo, taarifa inaonesha yapo majengo 14,348,372. Kati ya hayo, 13,907,951 yapo Tanzania Bara na 440,421 yapo Zanzibar.

I. MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19

Ndugu Mwenyekiti, mnamo tarehe 10 Oktoba, 2021 Serikali ilizindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19. Mpango huo uliotokana na mkopo nafuu wa shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) na ulilenga kuiwezesha Tanzania kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika uchumi na maisha ya Watanzania. 

Ndugu Wajumbe, tofauti na nchi nyingi, maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais yameiwezesha nchi yetu kutumia fedha hizo kuinua na kuendeleza sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya, elimu na maji.

i. Afya

Ndugu Mwenyekiti, katika sekta ya afya, Serikali ilitoa shilingi bilioni 466.9 kuimarisha huduma za afya na hadi sasa ujenzi wa vituo vya afya 394 na zahanati 763 umekamilika na huduma zinatolewa. 

Aidha, shilingi bilioni 136.51 zilitolewa kununua vifaa na vifaa tiba ambavyo vinaendelea kusambazwa maeneo mbalimbali nchini. 

Wakati Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, ni hospitali mbili tu za mikoa zilikuwa na mashine za CT Scan, sasa hivi hospitali 34 zina mashine hizo zikiwemo hospitali zote za mikoa. Kila mashine inanunuliwa kwa shilingi bilioni 2.4. Pia magari ya wagonjwa 720 yatanunuliwa ili kuimarisha huduma za wagonjwa nchini.

Ndugu Mwenyekiti, leo hii, hospitali zote za rufaa nchini zina mashine za MRI, tofauti na hapo zamani wakati nchi nzima ilikuwa na MRI moja tu. Hii imesaidia kusogezwa karibu na wananchi huduma za kibingwa badala ya kwenda Muhimbili, Nairobi au India kama ilivyokuwa awali.

ii. Madarasa na Mabweni

Ndugu Mwenyekiti, katika kufikia azma ya kuboresha sekta ya elimu, Serikali ilitoa shilingi bilioni 304 kwa ujenzi wa miundombinu ya elimumsingi katika Halmashauri zote 184. 

Fedha hizi zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 12,000 katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa 3,000 katika vituo shikizi na mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. 

Utekelezaji wa mpango huo umepunguza uhaba wa miundombinu ya shule katika shule za msingi na sekondari. 

Pia umewezesha wanafunzi wote 907,803 waliofaulu mtihani wa darasa saba mwaka 2021 kupata nafasi ya kuanza kidato cha kwanza Januari, 2022 bila kuwa na chaguo la pili.

iii. Uchimbaji Visima na Mabwawa

Ndugu Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji nchini, Serikali ilitenga shilingi bilioni 139.4 ili kutatua matatizo ya maji. 

Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 104.2 zimepangwa kutekeleza miradi 218; shilingi bilioni 17.5 kununua seti 25 za mitambo ya kuchimba visima; shilingi bilioni 17.6 kununua seti 5 za mitambo ya ujenzi wa mabwawa pamoja na seti 4 vifaa vya utafiti wa maji. 

Mwezi Novemba, mwaka huu, Wizara ya Maji ilikabidhiwa mitambo ya kuchimbia maji yenye thamani ya shilingi bilioni 35 ili ikafanye kazi ya kuchimba mabwawa siyo tu kwa ajili ya wanadamu lakini pia kwa ajili ya mifugo.

J. USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Ndugu Mwenyekiti, ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, Serikali imeboresha mahusiano na kukuza diplomasia ya siasa na uchumi kwa kufungua balozi mbili ambazo ni Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Vienna - Austria na Ubalozi wa Tanzania Jakarta, Indonesia. 

Pia imefungua Konseli Kuu mbili ikiwemo jiji la Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na jiji la Guangzhou, China na kuratibu mikutano 25 ya ubia wa maendeleo baina ya Tanzania na nchi za Afrika, Ulaya, Amerika, Asia, Australasia na Mashariki ya Kati. 

Vilevile, lugha ya Kiswahili imetambulika na kuidhinishwa kama lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika na Umoja wa Afrika na tarehe 7 Julai ya kila mwaka imetangazwa kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. 

Aidha, katika kuimarisha diplomasia, Serikali iliratibu ziara 36 za viongozi wa kitaifa nje ya nchi na ziara 11 za viongozi wa nje ya nchi waliotembelea nchini.

K. MUUNGANO

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea kulinda na kuthamini Muungano ili kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu kwa wananchi wa pande zote mbili. 

Katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba 2022, Serikali iliratibu vikao vitatu vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ na vikao 30 vya ushirikiano baina ya sekta zisizo za Muungano za SMT na SMZ. 

Aidha, hoja 18 zilijadiliwa na kati ya hizo, hoja 14 zilipatiwa ufumbuzi ikiwemo wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili na gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.

L. MICHEZO

Ndugu Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha timu za Taifa ili ziweze kushiriki katika mashindano ya Kimataifa na zimepata mafanikio makubwa. 

Timu hizo ni Tembo Warriors iliyofika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu na Serengeti Girls iliyofika robo fainali ya Kombe la Dunia katika michuano ya wanawake iliyofanyika nchini India.
 
Aidha, katika ngazi ya klabu, mafanikio hayo yanajumuisha timu za Simba Queens ambayo imefanikiwa kufika hatua ya nusu fainali ya Mashindano ya Klabu Bingwa ya Wanawake kwa upande wa Mpira wa Miguu barani Afrika, Simba Sports Club imefika hatua ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika na Dar Young Africans iliyofika hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Ndugu Mwenyekiti, baada ya kuangalia clip hiyo ninaomba sasa nihitimishe maelezo yangu:

MATARAJIO

9. Ndugu Mwenyekiti, katika miaka mitatu iliyobaki ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea na utekelezaji wa programu na miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na maeneo yote yalioainishwa katika Ilani ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii.

10. Ndugu Mwenyekiti, tunaendelea kuzingatia maelekezo yako ya kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji. 

Aidha, maeneo yenye changamoto yataainishwa na kufanyiwa kazi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuendelea kupitia tozo, ada na taratibu zote za uwekezaji. Lengo ni kuifanya nchi yetu kuwa na mazingira shindani ya uwekezaji na biashara.

HITIMISHO

11. Ndugu Mwenyekiti, mafanikio yote tuliyoyapata katika kipindi hiki cha miaka miwili ya utekelezaji wa Ilani yamechagizwa na juhudi zako binafsi pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuiongoza nchi yetu na kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma bora. Vilevile, ni kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Chama na Serikali.

12. Ndugu Mwenyekiti, nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mwenyekiti na viongozi wote wa Chama katika ngazi zote kwa kazi kubwa mliofanya na mnayoendelea kufanya.

13. Ndugu Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news