Makamu wa Pili wa Rais aitaka ZAWA kufuta mkataba wa kampuni iliyodanganya

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuisimamisha mara moja Kampuni ya Ms/Sapphire Engineering (T) Limited pamoja na kufuta mkataba baada ya kuidanganya Serikali kwa kuchelewesha kufikisha tenkila maji eneo la Raha Gando Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mhe. Hemed ameeleza hayo katika kikao kazi cha kujadili maendeleo ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kilichofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Mayugwani jijini Zanzibar.

Amesema, kitendo cha kuidanganya mamlaka hiyo kuhusu kuchelewesha kufikisha tenki hilo ni kitendo cha kuonesha udhaifu wake katika kazi hizo na kueleza mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria.

Amesema, Serikali imetenga fedha nyingi kwa kuwafikishia huduma ya maji safi na salama wananchi wake kwa muda wote na kushangazwa kuona baadhi ya watu kwenda kinyume na juhudi hizo.

Mhe. Hemed ameitaka mamlaka hiyo kupitia mikataba ya usambazaji wa vifaa na kuwachukulia hatua za kisheria wasambazaji wote ambao hawaheshimu mikataba hiyo kwa manufaa yao binafsi.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameukumbusha Uongozi wa ZAWA kuongeza uwajibikaji ili kuzidisha mapato na hatimaye waweze kujiendesha pamoja na kufikia kutoa gawio kwa Serikali.

Amesema, ili kuzidisha upatikanaji wa mapato kwa Mamlaka hiyo ni vyema kuhakikisha kila mtumiaji wa maji anapata mita itakayoweza kusaidia kujua kiwango cha maji wanachotumia.

Aidha, amesema kuwepo kwa Mita za Maji kutasaidia kuweka heshima ya matumizi ya maji kwa wananchi na kuwajua wote wanaotumia maji kwa Israfu.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed amesema huduma ya Maji safi na Salama ni ya lazima kwa kila mtu hivyo juhudi za kusaidia kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo zinahitaji uharaka ili kumaliza kabisa ukosefu wa Maji nchini.

"Suala la Malipo ya Maji si la hiari, Shilingi 4,000 kutoa ni lazima na mujue Mamlaka hii ni njia moja wapo ya kukusanya mapato kwenu, na pia mubuni mbinu nyengine ya kukusanya ili muweze kujiendesha na hatimae mutoe Gawio kwa Serikali " amesema

Aidha ameikumbusha Mamlaka hiyo kuendelea kuelimisha Jamii kujua namna ya kufanya malipo kwa huduma hiyo pamoja na kuwa na lugha nzuri wanapowahudumia.

Mhe. Hemed ameutaka Uongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini kukaa pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar ( ZAWA) pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa kujadlili pamoja kujua aina za pampu za kusambazia Maji ambazo hazitoathirika pale umeme unapopungua kasi na kupunguza kuungua Pampu za Maji mara kwa mara.

Wakitoa ufafanuzi Uongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar wamemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa watashirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar kupitia Mikataba iliyopo na kuhakikisha kuwa Kampuni haipewi zaidi ya Mkataba Mmoja.

Aidha wameeleza kuwa watasimamia nidhamu ya uwajibikaji ili kuleta Mabadiliko katika Mamlaka hiyo kwa lengo la kuboresha huduma zao kwa Maslahi ya Wananchi.

Kwa upande wao wakuu wa Idara mbali mbali za Mamlaka hiyo wamemueleza Mhe. Hemed kuwa watakuwa wamoja katika majukumu yao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Maji safi na Salama kwa wakati wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news