NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Watu wa China imeeleeza matumaini kuwa, Marekani itashirikiana na Taifa hilo ili kutafuta njia sahihi ya kuishi pamoja.
Hivi karibuni kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mheshimiwa Antony Blinken alisema marais wa nchi hizo mbili walikuwa na mkutano wenye tija mjini Bali mwezi Novemba,mwaka huu.
Rais wa Marekani Joe Biden akisalimiana na mwenzake Rais wa China, Xi Jinping kando ya mkutano wa wakuu wa mataifa ya G-20 uliofanyika Bali, Indonesia, Novemba 14, 2022. (Picha na Reuters).
Katika mkutano huo uliofanyika mchana wa Novemba 14, 20222 kwa saa za huko, Rais Xi Jinping alikuwa na mkutano na Rais wa Marekani, Joe Biden huko Bali, Indonesia.
Marais hao wawili walikuwa na mazungumzo ya wazi na ya kina kuhusu masuala yenye umuhimu wa kimkakati nchini China na Marekani ikiwemo mipango ya kuimarisha mahusiano na masuala makubwa ya kimataifa na kikanda.
Aidha, Waziri Blinken alisema safari yake ijayo nchini China inahusu kuendeleza mawasiliano hayo, kuhakikisha kunakuwa na njia za wazi za mawasiliano ili nchi hizo mbili ziepuke mzozo wowote na kushirikiana katika masuala ambayo yanawahusu si Wamarekani na Wachina pekee bali watu duniani kote.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Zhao Lijia.
Katika mkutano wa kawaida na waandishi wa habari uliofanyika Desemba 2, 2022 jijini Beijing nchini China, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Zhao Lijian amesema Rais Xi Jinping na Rais Joe Biden walikuwa na majadiliano ya wazi, ya kina, yenye kujenga na ya kimkakati kuhusu masuala makubwa yanayohusu China na Marekani.
Pia namna ya kuimarisha uhusiano na matarajio ya amani na maendeleo ya ulimwengu huko Bali na viongozi hao wawili walikubali kuimarisha mawasiliano na kubadilishana, na kuendeleza ushirikiano wa vitendo.
"Timu hizo mbili zinahitaji kufanyia kazi maelewano ya pamoja yaliyoafikiwa kati ya wakuu hao wawili wa nchi," Zhao amesema.
Kwa mujibu wa vipaumbele vilivyoainishwa na wakuu hao wa nchi, timu hizo mbili zinahitaji kudumisha mazungumzo na mawasiliano.
"Na kudhibiti mivutano na tofauti, na kuendeleza mazungumzo na ushirikiano, ili kuongeza misingi chanya na kudumisha usalama kwa China na Marekani, kujenga mahusiano, na kuleta utulivu wa uhakika katika ulimwengu huu wenye misukosuko na mabadiliko mbalimbali,"amesema.
"Waziri Blinken anatarajia kufuatilia mkutano wa marais hao wawili. China inakaribisha hili," amesema Zhao.
Ameongeza kuwa, upande wa China daima unatazama na kukuza uhusiano wake na Marekani kwa mujibu wa kanuni tatu za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano wa kushinda kama ilivyopendekezwa na Rais Xi.
"Tunatarajia kuwa, Marekani itafanya kazi na China katika mwelekeo huo huo na kutimiza kikamilifu maelewano muhimu ya pamoja yaliyofikiwa kati ya wakuu hao wawili wa nchi, kutayarisha kwa pamoja kanuni elekezi, au mfumo wa kimkakati wa uhusiano kati ya China na Marekani, ili kutafuta njia sahihi,"Zhao amesema.
Msemaji huyo amesema, njia sahihi ya nchi hizo mbili kuu ni kupatana na kurudisha uhusiano kati ya China na Marekani kwenye mkondo wa ukuaji wa kudumu kwa manufaa ya nchi hizo mbili na dunia kwa ujumla.