Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 yatafanyika Januari 2023-Waziri Nape

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Nnauye amewahikikishia wadau wa sekta ya habari nchini kuwa, marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 yatafanyika Januari, 2023.

Taarifa hiyo njema inakuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) kupendekeza maeneo mbalimbali ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebisho kuelekea mabadiliko ya sheria hiyo.

Hii ni miongoni mwa hatua nzuri kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambayo imeonesha kuijali Sekta ya Habari kama injini ya kusaidia kusukuma mbele taarifa chanya kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia ishara hii inatoa mwanga kuwa, huenda sheria nyingine zinazolalamikiwa ikiwemo Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa huenda nazo zikafanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Waziri Nape ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 nchini Tanzania leo Desemba 17, 2022 ambalo linaendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam amesema, mabadiliko hayo ni safari ya kuwezesha kulindwa kwa uhuru wa habari kwa mujibu wa sheria na sio utashi wa viongozi.

Aidha, kongamano hilo kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELERZO), Gerson Msigwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamnhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan la wadau wa vyombo vya habari kukutana ili kujadiliana kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Waziri Nape ameeleza kuwa, wakati hilo likisubiriwa, uhusiano baina ya sekta ya habari na sekta ya umma nchini umeendelea kuimarika katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“Hakuna furaha, amani na maendeleo kama uhuru wa habari katika jamii hiyo haupo, hivyo ni muhimu kulinda uhuru wa habari ili vitu hivi viwepo kwenye jamii. Hilo linawezekana na huo ndio msingi wa kongamano hili ambalo linalenga kuleta maendeleo, furaha na msingi wa taifa letu.

“Sheria na kanuni mbalimbali zinaendelea kufanyiwa mabadiliko kwa mujibu wa sheria. Uhuru wa habari unapswa kulindwa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa viongozi. Kiongozi yeyote atakayekuja atalazimika kuulinda uhuru huu kwa mujibu wa sheria hata kama hataki,"amefafanua Mheshimiwa Nape.

Akizungumzia kuhusu kongamano hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa amefafanua kuwa,hili ni kongamano la kwanza nchini ambalo ni kiashiri chema kwa sekta hiyo nchini tunapojiandaa kuupokea mwaka mpya wa 2023.

"Hii ni siku ya kihistoria katika nchi yetu, tumelianzisha tukio la kihistoria ambalo hatujawahi kuwa nalo tangu nchi yetu izaliwe (ipate Uhuru).

"Kwa sisi wanahabari hii itakuwa ndiyo Krisimasi yetu, ndiyo mwaka mpya wetu, ndiyo funga mwaka yetu. Kwa hiyo ni siku muhimu sana na nina furaha kuona leo tumeungana na Mheshimiwa Waziri wetu kuianza safari hii muhimu katika Sekta ya Habari,"amefafanua Msigwa.

Balile

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amesema, kufanyika kwa kongamano hilo ni hatua njema ya kuendelea kuimarika kwa Sekta ya Habari hapa nchini.

"Mheshimiwa Msigwa amesema vizuri hapa, Msemaji Mkuu wa Serikali. Itakumbukwa kwamba, Mei 3, Mheshimiwa Rais alitoa agizo la kukutana na wanahabari wote hapa nchini.

"Lakini, Machi 9 Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilikuwa na Mkutano wa Sita pale Zanzibar ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

"Moja ya maazimio ya Jukwaa la Wahariri Tanzania ni kwamba, Sekta ya Habari tumeganwanyika, sekta ya habari tumetawanyika. Sekta ya habari pamoja na kwamba tuna wizara, lakini tulikuwa huku chini kama hatuna mchungaji,mheshimiwa Waziri niwie radhi.

"Tukasema, tuwe na mkutano angalau mmoja ambao utatukutanisha wote kama wanavyokutana wafanyabiasha, kama wanavyokutana wanasiasa kama wanavyokutana wanasheria.

"Sasa kidogo mwaka huu nikaenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri nikamwambia kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba tuna mkutano na Mheshimiwa Rais, lakini tunadhani ni vema kama wanahabari tukakutana, kuna maafisa habari,kuna watu wa ICT.

"Ya kwamba tukakutana tunaweza kutoka na jambo jema, (Mheshimiwa Waziri) akasema,sasa tuyaunganishe yote mawili, lakini tusifanye kama Jukwaa la Wahariri, maana itaonekana mmejitenga na wenzenu, akasema tushirikiane wote kama wanataaluma liwe kongamano la wadau wote. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri,"amefafanua Balile.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Balile amesema, licha ya kuwepo kwa uhuru wa habari nchini, ameomba uhuru huo ulindwe kisheria.

“Wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru wa habari uliopo nchini, tunaamini serikali italinda uhuru huu kisheria katika Mabadiliko ya Sheria ya Habari yajayo,"amesema Balile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news