MGENI AU MWENYEJI?

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWAKA 1996 hadi miaka ya 2000, mwanakwetu alikuwa akiishi Magorofani Keko Block D vyumba vya juu kabisa katika gorofa hili. Ndugu wa damu wa mwanakwetu aliyekuwa anakaa hapo alipata safari ya Ughaibuni akasema vijana mkakae pale kwa kuwa mnasoma hapo ni jirani na mjini kuliko kutokea Mbagala.
Katika hayo Magorofa kulikuwa na Block A mpaka D. Hadhi za Maghorofa hayo zilitofautiana kidogo Block A, C na D zilikuwa za makabwela kwani mandhari yake ilisadifu hilo kwa mfano mabomba ya maji machafu yalikuwa yanapasuka huku maji hayo yakitiririka hovyo bila ya matengenezo muda mrefu.

Block B pekee ndiyo ilikuwa ghorofa la hadhi ya juu na miongoni mwa wakazi wake alikuwepo tajiri mmoja wa Kimakonde anayefahamika kama Achimwene.

Maisha ya magorofani yanahitaji uzoefu maana muda wote upo chumbani au umekaa sebuleni unatazama runinga, unacheza gemu au unasoma vitabu hasa kwa siku za mapumziko.Unapotaka kuongea na mtu basi unawajibu wa kumfuata kwake au yeye aje ulipo.

Ndani ya Block D alipokuwapo mwanakwetu, lilikuwa gorofa lililochangamka mno wakiwapo wasanii wa muziki na sanaa za maonesho. 

Kundi mojawapo katika jingo hilo ambalo halikuwa maarufu sana ni Morgan Familly, hili ni kundi moja la muziki wa Reggae, kundi hili halikuweza kufaya vizuri katika ulimwengu wa muziki wa Reggae ambao nyimbo nyingi zilikuwa za ukombozi zikakosa mvuto na ndugu zake mwanakwetu hawa kidogo waligoma kubadilisha maudhui ya nyimbo zao.

Vijana wa Keko Magorofani walipokuwa na sherehe kama ya kukaribisha mwaka mpya kundi hili lilialikwa na kufanya maonesho yake, wakati huo kumbuka vijana wa Bongo Flavour kama Solo Thang–Ulamaa–Msafii Kondo walialikwa pia kwani walikuwa wakianza harakati za muziki wao. Kundi hili likapotea katika ulimwengu wa muziki huku baadhi ya vijana wa bendi hii walifariki dunia.

Nakuomba msomaji wangu fahamu kuwa eneo la Keko, Temeke na Chang’ombe ni maeneo yaliyokaliwa na watumishi wa serikali wa zamani wakiwamo watumishi wa mkoloni na Tanganyika huru kwa hiyo wengine walifariki na huku vizazi vyao vikibaki katika maeneo hayo na wengine kununua maeneo kando kando yake.

Yakumbuke yale Magorofa A, B, C na D sasa kando ya Block C na D palikuwepo na Ofisi ya NCCR MAGEUZI na baadaye ikawa ofisi ya TLP ya Wilaya ya Temeke. 

Katika ofisi ya NCCR/TLP ya Wilaya ya Temeke nyumba hii iliweza kufikiwa na wanasiasa wengi wa upinzani wa wakati huo na hilo liliwapa bahati kubwa wakazi wa eneo hili kuwafahamu wanasiasa hao tabia zao za jukwaani na nje ya majukwaa akiwamo Charles Makongoro Nyerere (Mkuu wa Mkoa wa Manyara).Makongoro yule ni kadhaa kadhaa wa kadhaa , hayo yalisemwa wazi wazi.

Wakati huo mwanakwetu ni mwanachuo wa Chuo Cha Ualimu Kasulu huku akiishi hapo Block D kila ikifika jioni wakati wa likizo alikuwa anashuka gorofani anakwenda kukaa jirani na maegesho ya magari ya ofisi hii ya NCCR/TLP hapo walikutana vijana wengi waliosoma shule za sekondari za Dar es Salaam kama Tambaza, Azania, Kibasila na Forodhani na wakati huo wengi wao walikuwa vyuoni.

Siku moja mjadala ulikuwa juu ya mwanakwetu kusomea ualimu, mjadala uliongozwa na ndugu wawili kati ya mwaka 1990-1994 Doto alisoma Tambaza na Kurwa alisoma Azania.

“Mwanakwetu unakwenda kuwa mwalimu lakini usituchapie watoto wetu, uwe mwalimu bora.” Mwanakwetu alicheka sana siku hiyo na akiungama mbele yao kuwa atakuwa mwalimu bora.

Wakiwa hapo kwenye maegesho ya magari, kwa kando mlingoti wa bendera ya TLP ukiwa umesimama isipokuwa bendera tu ya chama hiki iliyokuwa imeshushwa saa 12 kamili ya jioni, kwa mbele mwanakwetu na wenzake wanayaona magari yanayopita katika barabara ya Chang’ombe kushoto Block D na kulia Block C, mara akapita mwanasiasa mmoja wa Tanzania.

Vijana hawa wakawa wanamwambia mwanakwetu, yule ni msomi na mwanasiasa mzuri lakini angeenda CHADEMA au NCCR angefanya vizuri sana siyo huko CUF.Wakiwa hapo mwanakwetu siku hiyo akauliza je mwanasiasa huyu anatoka wapi na anakwenda wapi? Kijana mmoja wa Kingoni anayeitwa Tomson Luena akamjibu mwanakwetu kuwa alikuwa anatoka kazini kwani anaishi Block B pamoja na Mzee Achimwene.

Maisha yaliendelea na mwanasisa huyu hadi akaja kushika nyadhifa kadhaa ndani ya CCM na hadi leo hii ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maisha yanasonga , Oktoba 2022 mwanakwetu alikuwa katika jumuiya ya imani yake ukifanyika uchaguzi wa viongozi wa dini, katika uchaguzi huo mama mmoja alichaguliwa kushika nafasi mojawapo, mama huyo alinyoosha mkono na kuomba kuwa yeye aondolewe katika nafasi hiyo kwa hoja kuwa hana uwezo wa kuifanya kazi hiyo maana yeye ni mgeni katika imani hiyo. 

Kiongozi aliyekuwa anasimamia uchaguzi huo alisema wazi kuwa katika imani suala la ugeni siyo sahihi ilimradi tu ametimiza taratibu zote za imani, hivyo lazima awe kiongozi wa jumuiya na hilo siyo kigezo cha kukwepa.

Mwanakwetu alikaa kimya na kutafakari sana suala la mama huyu na akikukumbuka kuwa katika ulimwengu wa imani kuna wakati kanisa liliwatangaza baadhi ya wafia dini kuwa watakatifu kwa kutumia baptismus sanguinis/ubatizo wa damu kwani hadi wanakufa hawakuwa wamebatizwa.

Mama huyu kwa maelezo ya msimamizi wa uchaguzi huo alikubali na kuwa miongoni mwa viongozi wa jumuiya hii huku akiifanya kazi hiyo vizuri sana hadi Disemba 10, 2022 alipopata uhamisho na kuhamia Mwanza yeye na mumewe.

Mwanakwetu anaiweka kalamu chini akisema kuwa ubora wa mtu yeyote pale alipo hauwezi kutegemea tu namna alivyoweza kuwepo kwa muda mrefu, inawezekana mgeni akawa na mchango bora kuliko hata mwenyeji la msingi ni namna mtu huyo alivyo na dhamira njema hapo alipo, mwenyeji na mgeni wote wapewe nafasi tu na katika siasa ni kuungwa mkono na walio wengi huko ndiko kunakoleta ushindi.

0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news