NA DIRAMAKINI
MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema,Serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya vipengele vya Sheria ya Habari ili wabunge wakiridhia, utekelezaji wake ufanyike.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), uliofanyika katika Ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.
Msigwa amesema, anatambua kuwa katika tasnia ya habari kuna changamoto na miongoni ni kuhusu sheria zinazohitaji kurekebishwa.
“Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia, tuendelee na utekelezaji wake,” amesema Msigwa.
Msemaji huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) amesema, mchakato wa kukutana na wadau kwa ajili ya majadiliano ya vipengele vya sheria hiyo ya mwaka 2016, umekamilika.
“Niwahakikishie kuwa, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari kufanya kazi bila bughudha yoyote.
"Tayari Mheshimiwa Rais ameshamuagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kukutana na wadau wa sekta ya habari na kujadili namna ya kuziboresha sheria ambazo siyo rafiki kwa tasnia ya habari,” amesema.
Amesema, miongoni mwa sheria hizo ni ile ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016, ambapo tayari vikao kadhaa kati ya serikali na wadau vimefanyika.
Pia amesema, serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa habari nchini katika kukabili changamoto zilizopo.
“Niwahakikishie kuwa, serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa habari katika kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili waandishi wa habari zikiwamo kutatua sheria zisizo rafiki, zinafanyiwa kazi na kuwa na sheria zinazotokana na pande mbili kukubaliana yaani serikali na wadau,”amesema Msigwa.