MWANYUMBA!!!: Sisi kuoa pamoja, na yetu yawe mamoja

NA LWAGA MWAMBANDE

JULAI 7, 2022 Audrey Azoulay ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika ujumbe wake wa siku ya Kiswahili duniani, ambayo maadhimisho ya kwanza yalifanyika siku hiyo, aliudhirishia ulimwengu kuwa, Kiswahili ni lugha ya Kimataifa ambayo inaendelea kukuwa kwa kasi.

Akitoa salamu ya Habari gani!!! kupitia ujumbe wake kwa njia ya video,Azoulay alisema anajisikia furaha sana kusherehekea siku ya lugha ya Kiswahili huku UNESCO ikiwa inajivunia pia kuwa kitovu cha maadhimisho hayo kufuatia kupitishwa kwa azimio mwezi Novemba, mwaka jana.

“Zaidi ya yote ni kwa sababu Kiswahili ni zaidi ya lugha ya mawasiliano. Kiswahli ni dirisha la kupitia kuelekea tamaduni tofauti tofauti, mawazo, aina za ufahamu wa elimu na pia ina kitu pekee katika mtazamo wake kwa Dunia. Mapinduzi ya lugha hii yamesheheni karne za mabadilishano,"alifafanua Azoulay.

Kwa kuliona hilo, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, lugha ya Kiswahili imesheheni utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, methali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Endelea;

1:Mwanyumba nakutafuta, tupange yetu mwakwetu,
Mbona kama unasita, tusifanye mambo yetu?
Ni nini kimekupata, hata mambo yawe butu?
Sisi kuoa pamoja, na yetu yawe mamoja.

2:Wakwe walivyotuita, kule kuna jambo letu,
Pengine wanatafuta, suluhu kwa wake zetu,
Wajua kuna utata, hawaelewani katu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

3:Mwanyumba wajua vita, ni ile safari yetu,
Sehemu tuliyokuta, vyauzwa vingi viatu,
Uliibuka utata, wa kugombea viatu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

4:Mkeo aliokota, na kujaribu kiatu,
Mke wangu kumkuta, kamshauri si kitu,
Badaye kupitapita, kabeba kile kiatu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

5:Huo ni mwanzo wa vita, wajunja undugu wetu,
Wamegombana kupita, kufika kwa wakwe zetu,
Twatakiwa kuchakata, tuwe na majibu yetu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

6:Mwanyumba sijakupata, huoni simufifi tu?
Bora ukanitafuta, tuyajenge haya yetu,
Ikibidi kuwaita, hawa ndugu wake zetu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

7:Mke wangu nitamwita, alete vile viatu,
Na mkeo utamwita, tuamue mambo yetu,
Naamini hutasita, tumalize mambo yetu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

8:Ili suluhu kupata, tuvichukue viatu,
Asiwepo wa kupata, kati yao wake zetu,
Hadi tutakapopata, vifananavyo viatu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

9:Wazazi walotuita, twende kwa umoja wetu,
Tuseme ule utata, wao hawa wake zetu,
Suluhisho tumepata, tunaishi kiutatu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

10:Mwanyumba umenipata, au maelezo butu,
Unalo lingine teta, kama sivyo twende zetu,
Wake zetu kuwaita, tuyamalize kivyetu,
Sisi kuoa kumoja, na yetu yawe mamoja.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news