NA LWAGA MWAMBANDE
KILA mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kuwa wazalendo, kujenga,kuiendeleza na kuilinda nchi yetu na watu wake kwa ajili ya maslahi ya maendeleo ya Taifa na jamii kwa ujumla.
Ni kutokana na ukweli kwamba mustakabali wa familia, jamii na maendeleo ya Taifa lolote duniani unategemea nguvu ya uzalendo ukizingatia bidii, umoja, mshikamano na weledi ambao ndio chachu ya kuleta mageuzi ya kifikra na maendeleo jumuishi na endelevu kwa jamii.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, mzalendo mwenye bidii ndiye licha ya kuwa na mchango kwa jamii na Taifa lake, pia ana fursa kubwa ya kufurahia mema ya nchi, anza safari. Endelea;
1.Mzalendo jilipue, mbele tutakuipua,
Ndiyo njia utusue, na mapene kuyajua,
Wachache uwasumbue, wengi tuotee jua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
2.Wenye nazo wabinue, sisi tupate wajua,
Usiache watanue, wakati wanatuua,
Wewe fanya watifue, kuwachambuachambua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
3.Sasa acha waugue, muda wao kuungua,
Na kilio waangue, yaja tumbuatumbua,
Na kitanzi wachukue, nguo hatujawavua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
4.Wako wapi tuwajue, makubwa waloibua?
Ni vipi tuwatambue, na medali kuchukua?
Ni wapi tuwachukue, mengi wazidi pumua?
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
5.Hujasema tukujue, upate kujiinua,
Au kwamba utibue, kwa kusumbuasumbua,
Ni lengo utuinue, wengi tuzidi tanua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
6.Ni watu tuwatambue, ambao wajilipua,
Siyo wao watusue, pale wanapojiua,
Wachache wasisumbue, wengi tunapougua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
7.Wachache tuwaumbue, wale wanaosumbua,
Ya kwamba wakichukue, kile chetu kitumbua,
Njaa sisi tuugue, wenyewe wakikamua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
8.Pazia tulifungue, uzalendo weze kua,
Na watu wote wajue, kwamba tutawaumbua,
Wakirogwa watibue, wajue twawatimua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
9.Ili nchi tupindue, uje mwangaza wa jua,
Ni lazima tuchague, wabaya kuwararua,
Viuno tuvitengue, hilo wapate kujua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
10.Ngoja chai nichukue, nitafune kitumbua,
Mto kichwa niinue, raha yangu naijua,
Chafya isinichefue, imalize kuugua,
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
11.Chuma na tukutambue, wajue wasokujua,
Visiki visisumbue, tumekwishavitambua,
Tuache vijianue, au ni vya kuchimbua?
Inahitajika moyo, na tena moyo wa chuma.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602