NA DIRAMAKINI
MITUME na manabii nchini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametakiwa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano ili kuwezesha injili na neno la Mungu kusonga mbele.
Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania unaongozwa na Rais Nabii Dkt. Joshua Aram Mwantyala ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu Mjini Morogoro.
Kupitia hotuba ya Naibu Msemaji wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania,Balozi Nabii Dkt.Richard Godwin Magenge aliyoitoa leo Desemba 5,2022 amefafanua kuwa;
"Yapo mambo ambayo nimesema nitayazunguma, mambo haya ni kama ifuatavyo. Jambo la kwanza ni umuhimu wa umoja wetu na jambo la pili umuhimu wa ushirikiano na tatu ni viongozi na nafasi zao, na nne ni mkutano wa pili wa mitume na manabii utakaofanyika jijini Dodoma.
Kuwahusu
"Mitume na manabii ndio taasisi pekee iliyoletwa na Mungu wetu kwa ajili ya ukombozi na imani kwa watu wampendao Bwana. Huduma hii ni msingi au mama katika mwili wa Kristo.
"Maandiko yanasema imani yenu imejengwa katika ya msingi wa mitume na manabii kwa hiyo tuna kazi ya kujenga watu kiimani katika huduma ya kitume na kinabii.
"Inapokea huduma zote tano kitume, kinabii, kichungaji, kiinjilisti na huduma ya kialimu. Huduma hii ina umuhimu sana katika taifa letu."
Mosi
"Jambo la kwanza lazima tufahamu kwamba huduma hii inapigwa vita sana katika nchi yetu, ndio huduma ambayo ina makando kando katika nchi yetu na ndio huduma yenye mlengo chanya kwa Mungu wetu ndio ukombozi wa watu wanaompenda Mungu nao anawapenda.
"Katika taifa letu huduma ya kitume na kinabii ndio huduma yenye kuleta mabadiliko makubwa ya imani, ukombozi wa fikra na kuleta mabadikiko katika ufumbuzi wa neno la Mungu lililojaa kweli.
"Ndugu zangu mitume na manabii,huduma hii inaongoza kwa kufanya makubwa yahusuyo imani, tunaongoza na baadhi ya mitume na manabii wanaofanya vizuri katika nchi yetu, wanafundisha vizuri, tunaona ukombozi dhahiri miujiza na mambo mengi yale ambayo tumekuwa tukiyaona kwenye Biblia.
"Na sasa yanatendeka kwa uhalisia wake kwa baadhi ya mitume na manabii katika Taifa letu. Nchi yetu sisi inakumbwa na adha moja kubwa sana ya kiroho kwamba taifa letu halina dini, Taifa letu halina Mungu kwa maana kwamba Serikali yetu haina dini,tunakubali kwamba Serikali haina Mungu.
"Sasa Mungu anafanya kazi na Serikali, kama nchi haina serikali maana yake Serikali yetu kikatiba haina Mungu na hivyo ni ngumu sana Mungu kufanya kazi katika taifa ambalo limekiri halina Mungu taifa letu ukiangalia katiba yetu inasema serikali haina dini,lakini watu wake wana dini.
"Nchi zote ambazo zinatuzunguka ambazo zimeweka imani ya Kikristo kama ndio imani ya kiserikali zinafanikiwa, manabii wanafanikiwa, mitume wanafanikiwa, wainjilisti, wachungaji lakini hata huduma nyingine za ulimu zinafanikiwa.
"Kwa sababu Mungu amekuwa akijidhihirisha, katika Taifa letu la Tanzania Mungu amekuwa akijidhihirisha kwa tabu sana, kuomba sana na kuteseka sana kwa sababu Mungu anafanya kazi na serikali na kama Mungu anafanya kazi na serikali na nchi haiamini juu ya dini,juu ya imani ya kwamba haifungamani na upande wowote wa dini kwamba Mungu hafanyi kazi na watu hapana, Mungu anafanya kazi na viongozi wa nchi.
Msisitizo
"Ndugu zangu mitume na manabii, huduma yetu ina umuhimu sana katika taifa letu, sababu nchi yetu haina dini na Serikali yetu imekiri haina dini.
"Kama hakuna serikali inayomwamini Mungu basi hakutakuwa na Mungu katika nchi hii, basi tunayo kazi mitume na manabii ya kumdhihirisha Mungu kwa nguvu zetu zote, hivyo basi hatuwezi kumdhihirisha Mungu pasipo ushirikiano, mshikamano, pasipo umoja Mungu hawezi kujifunua.
"Umoja huu una umhimu sana kwetu mitume na manabii, wapo manabii Mungu amewaita, mitume amewaita lakini hawana malezi wanapokosa malezi inawapelekea wao kupotea katika kutafuta chakula na hatimaye wanapata chakula ambacho si cha kweli.
Ushuhuda
"Nimeshuhudia kijana mmoja ambaye amepewa neema na Mungu ameitwa na Mungu, lakini kwa sababu ya kufundishwa mafundisho yasiyo sahihi ameipoteza huduma yake, mshikamano wetu,umoja wetu masikilizano yetu yana uwezo wa kutusaidia katika maelewano yetu ya kutembea katika huduma zetu.
"Katika Biblia wapo watu wanaitwa wana wa manabii walikuwa pamoja, katika Biblia tunaona wako mitume waliinuliwa walikuwa pamoja, walitenda kazi pamoja hata huko mbele kulitokea kutofautiana kwa mafunuo, wapo waliopewa mafunuo na wengine neema.
"Wale waliopewa mafunuo ya neema walitembea katika neema. Kutoafautiana kupo katika wito, lakini masikilizano yakiwemo utofauti utakuwa ni mdogo sana."
Pili
"Ndugu zangu jambo la pili ushirikiano baina ya mitume na manabii hivi karibuni kulitokea na kuwepo sintofahamu kubwa sana tunakosa ushirikiano. Na hii inasababishwa na vitu vikubwa vitatu.
"Kila nabii au mtume anajiona ni bora kuliko mwenzake, kila mtu anapojiona ni bora kuliko mwenzake kunakosa ushirikiano.
"Kama ukiondoa wewe kujiona bora ukaona mwenzako anastahili mahali pake na wewe unastahili mahali pake ushirikiano ukiwepo baina yetu tutaujenga mwili wa Kristo.
"Jambo la pili linalosababisha kusiwe na masikilizano ni kiburi cha uzima, mitume na manabii wengi tumekuwa na kiburi cha uzima vitu vingi hatujui.
"Lakini ikitokea mtu anasema kitu basi wote inaonekana tunajua kiburi kimetufanya tukose ushirikiano kila mmoja amekuwa ni simba katika eneo lake na hataki kujishusha.
"Moja kati ya jambo litakalofanya tukafanikiwa ni umoja na ushirikiano. Hivyo tuondoe kiburi cha uzima."
Tatu
"Jambo la tatu ni kuwepo kwa kiburi kisichokuwa na tija, mitume na manabii wengi tunamakundi yaani magroup ya WhatsApp kila group lina mifumo yake na namna yake ya kutembea kila group na namna yake ya uongozi,hivyo tumejikuta tunachanganyikiwa na kushindwa kuwa na uelewano wa pamoja na kushindwa kujua tunakwenda wapi kiongozi, gani tumfuate na tumsikilize na hivyo kutuyumbisha.
"Kwani kila group linapoibuka yanaleta namna yake utaratibu wake vitu vyake na jinsi ya kutembea tunakosa ushirikiano.
"Jambo la tatu ni viongozi na nafasi zao siwezi kulizungumzia hapa hadharani. Sisi Kama viongozi tuna vikao vyetu tukiongozwa na Kiongozi wetu Rais wetu mahiri Nabii Joshua kutoka Morogoro kiongozi aliyepewa neema ya uvumilivu, kujitoa, kujali Mungu ametusaidia kutupa kiongozi wa namna hii ana uwezo kumsikiliza kila mtu, ana uwezo wa kumfuata kila mtu na kutatua shida ya kila mtu anayemwendea.
"Ndugu zangu chini ya uongozi wake tukisema tumtie moyo kiongozi huyu, tumsaidie kiongozi huyu chini ya utawala wake tuna uwezo wa kulifikisha gurudumu hili mahali patakapo stahili.
"Niwaombe mitume na manabii na viongozi wenzangu tumtie moyo kiongozi wetu, Rais wetu ni mpweke amekuwa akipigwa mawe kila siku anafanya kazi na watu ambao amewateua na wale waliochaguliwa na mitume na manabii lakini hawatoshi.
"Sisi mitume na manabii wote tukiheshimu utawala wake huyu nabii amepewa neema na Mungu, hakuna nabii aliyepewa huduma asipeleke huduma yake mbele hata wewe ungekuwa umeteuliwa usingeacha huduma yako bali ungetembea na huduma yako.
"Nabii Joshua ukiacha huduma anayoiongoza iliyopo Morogoro ametembea katika mikoa mingi akihubiri umoja wa mitume na manabii, akifundisha kuonya na kukemea kwa dhamiri yake safi akiongozana na baadhi ya viongozi wa mitume na manabii nchi nzima.
"Ndugu zangu mitume na manabii tunaye Rais wetu huyu kwa sasa, tunao wajibu wa kumpa heshima kama kiongozi wetu, kumtetea na kumpigania katika hali zote ili alifikishe gurudumu letu mahali panapo stahili.
"Rais wetu amekuwa akitoa fedha zake sio milioni moja mbili au tatu akitembea kuongea juu ya umoja huu pasipo malipo yoyote, akitumia fedha zake lakini tupo viongozi kupitia fedha zake tumekuwa tukisafiri, kula, kuvaa ndugu zangu tunayo sababu ya kumpa heshima kiongozi huyu Mungu ambariki kiongozi Nabii Joshua.
"Tumtie moyo, viongozi wote tukishirikiana tukashikamana na kuthaminiana mambo yatakwenda. Cha msingi kila kiongozi aishike nafasi yake na kuitekeleza moja kati ya jambo ambalo tunakutana nalo viongozi ni kujimwambafai,hatuwezi kufika popote bali unyenyekevu ndio silaha pekee itakayotusaidia kuufikisha umoja wa mitume na manabii mahali panapo stahili.
Nne
"Jambo la nne ni la mkutano Mkuu wa pili la mitume na manabii huko Dodoma, kamati kuu imeshakaa kikao cha siri na taarifa yake imeshatolewa na Naibu Msemaji ya kwamba kila kiongozi anatakiwa kuchagia mkutano huo, achilia tu kuchangia bali kufikia maandalizi ya mkutano wa pili utakaofanyika mwakani mwezi wa Nane hapo sio mbali tayari tuko mwezi wa 12 tumebakiza miezi nane tu kufika muda huo, nitoe rai kwa mitume na manabii kuanza maandalizi ya kishindo katika mkutano huo utakaoshangaza ulimwengu, niwaombe mitume na manabii tujiandae kushiriki tulipie ada.
"Ni muhimu sana mitume na manabii tukafanya jambo hili kwa umoja wetu sote, lakini Mungu ataachilia neema hiyo akiona tumeshikamana itatolewa namba ya jinsi ya kuchangia na kutoa ada zetu na pia ambao bado hawajasisajili wajisajili.
"Umoja ndio jambo la muhimu la kutuunganisha kufanikisha jambo hili. Tumeona Rais wetu akienda Dar es Salaam, Songea na mikoa mbalimbali umoja wa mitume na manabii ndio chama ama kikundi ambacho ni muhimu kuwa kitu kimoja.
Tano
"Jambo la tano, kazi za wana umoja cha kwanza kuilinda katiba na kuitekeleza kila mtume aisome na kuitekeleza soma Katiba na uitekeleze, kazi ya pili kutangaza umoja wetu na kuundeleza uwe umesoma Katiba na kupata nafasi ya kuufafanua kwa wengine wajiunge ambao bado hawajajiunga. Pia kuhubiri umoja wetu harusini, kanisani kuhusu umoja wetu na kazi nyingine ni kulipa ada suala la fedha lina umuhimu sana."
"Kuna watu ni wadanganyifu wanahubiri kushindwa kujua ni wana umoja na wengine wanajitwalia madaraka kinyume na utaratibu. Jambo hili litasababisha umoja kukwama. Kazi yetu ni kuhubiri umoja nikiwa kama Naibu Msemaji tusizimie moyo tuwe wamoja na tushirikiane mwanzo ni mgumu...tuko mwanzoni tunapekecha kijiti inakuwaga ngumu kidogo.
"Ndugu zangu lazima niwasisitize kila mmoja wetu aujue umuhimu wa mitume na manabii, pili lazima kuwe na ushirikiano baina ya mitume na manabii nchini, tatu Viongozi waliopewa nyadhifa zao kuzishika na kuzitekeleza kwa wakati, nne ni kuhusu mkutano Mkuu kila mmoja ahakikishe anachangia na kufika na kila mwana umoja afike yatakayofanyika ni makubwa na kila mwana umoja lazima azingatie kujua kazi yake yeye,"amefafanua Naibu Msemaji wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania,Balozi Nabii Dkt.Richard Godwin Magenge .