NI KIZAZI CHA KATUNI:Katuni hizo katuni, tuweni nazo makini kwa watoto

NA LWAGA MWAMBANDE

SIKU za karibuni kizazi hiki cha kidigitaji kimejikuta kikiwa na nafasi ya kupokea bidhaa na huduma nyingi ambazo kwa upande mmoja zina manufaa makubwa ikiwa zitatumika kwa kusudio lililotarajiwa, huku kwa upande mwingine zikiwa na athari hasi kubwa hususani kwa watoto.

Ni kipindi ambacho wazazi wamekuwa mstari wa mbele kujinunulia simu za kisasa au vishikwambi, ambazo zina uwezo wa kupata maudhui ambayo mwenye runinga anaweza kuyapata, hivyo mwenye simu au runinga ni sawa tu. Na vifaa hivyo, vimekuwa vikitumika kuwafurahisha watoto wao.

Bidhaa za kidigiti ni bidhaa zinazopatikana katika mtindo wa sauti,picha,picha mnato au kurasa. Aidha,mara nyingi bidhaa hizi huwa ni za kufundishia, hivyo waandaaji wanapokaa chini na kutayarisha vipindi vyao huwa wanakusudia kuwalenga watu fulani.

Miongoni mwa kundi ambalo limekuwa likilengwa kupewa elimu kupitia huduma hizo kwa njia ya katuni ni watoto. Ambao, vipindi vingi vimekuwa vikiandaliwa na kurushwa katika runinga mbalimbali vikiwahusu watoto wetu.

Ingawa kwa upande wa waandaaji dhamira yao si mbaya, bali wanawaza kupandikiza tamaduni na mila zao, kulingana na vipindi vinakorekodiwa na kurushwa, hali hiyo imesababisha wengi wao kucheza baadhi ya vipengele ambavyo kwa namna moja au nyingine vimekuwa si rafiki na havina tija kwa watoto hususani wa Kitanzania.

Ni sehemu ya maudhui ambazo zinahamasisha lugha za kigeni, tamaduni za kigeni ambazo ukizichuja kwa jicho la kipekee utagundua kuwa,unamwandalia mwanao aina fulani ya maisha ambayo siku za mbeleni atajikuta katika hali ya kushangaza na kustaajabisha.

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, hakuna anayekuzuia kuwafurahisha watoto wako kupitia katuni, lakini yafaa kutumia akili ya kuzaliwa na kuwapa watoto wako stadi za maisha ambazo zinaendana na mila na tamaduni za Kitanzania, kuliko kuwapa fursa ya kushinda kwenye katuni, labda kama zingekuwa zinajikita katika maisha ya Kitanzania, endelea:

1:Ni kizazi cha katuni, kinalelewa nyumbani
Asubuhi na jioni, simu ziko mikononi,
Siyo simu mikononi, runinga ziko hewani,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu,

2.Kweli wako likizoni, wasiishi ka shuleni,
Lakini hata nyumbani, wasishindie katuni,
Zipo kazi za nyumbani, ziwaingie kichwani,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

3.Wanachezea katuni, anayedhibiti nani?
Wanajificha vyumbani, mfwatiliaji nani?
Twawajenga akilini, au twaenda porini?
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

4.Zingekuwa za nyumbani, wanazocheki katuni,
Zionyeshe ya nyumbani, yale ya kitamaduni,
Tungekuwa na amani, na mioyo ahueni,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

5.Katuni ni za kigeni, hata lugha za kigeni,
Utamaduni mgeni, tena hatuuamini,
Lakini twaona nyumbani, wawe huru na katuni,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

6.Hata wawe likizoni, wasiwe majaribuni,
Wasahau ya shuleni, wakumbate ya katuni,
Kesho wawe wa kigeni, tuhangaike kwanini,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

7.Bora wazazi nyumbani, simu ziko hadharani,
Wakihitaji katuni, usimamizi makini,
Kikija kilicho duni, hicho wakipiga chini,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

8.Acha waende jikoni, wajifunze ya mekoni,
Na asubuhi vyumbani, wao waende kazini,
Nguo chafu kabatini, waziloweke majini,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

9.Katuni hizo katuni, tuweni nazo makini,
Zisiingie vichwani, watoto wafanywe duni,
Simu zetu mikononi, zisiwatie jangwani,
Wenzao wanayofanya, ubunifu ubunifu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news