Nsokolo:Rais Dkt.Samia ni rafiki wa wanahabari

NA DIRAMAKINI

“Rais Samia (Dkt.Samia Suluhu Hassan) tangu alipoingia madarakani, alikuwa karibu na sekta ya habari na kutoa matumaini ya kufanyiwa marejeo kwa sheria hii ya mwaka 2016. Na tayari matokeo yake ni wadau wa habari na serikali kukaa kwa pamoja na kuainisha vipengele gani tungependa viondolewe;

Hayo yamesemwa na Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Deogratius Nsokolo leo wakati akitoa maoni yake kuhusu mwenendo wa mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini
Pia amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani amekuwa ni rafiki wa waandishi wa habari huku akisisitiza kuwa, maendeleo ya mchakato huo yanatokana na kuridhiwa na Serikali ya Rais Samia.

Nsokolo amesema, utayari huo umeoneshwa wazi hasa baada ya wasaidizi wa Rais Dkt.Samia kuanza kwa vitendo hatua kwa hatua katika kukutana na wadau kwenye vikao vya pamoja.

“Upande wa serikali na wadau umeshamaliza kazi yake ya kuainisha vipengele hivyo, kilichotarajiwa ni mwaka huu mwezi wa tisa mapendekezo hayo kupelekwa bungeni, lakini kwa bahati mbaya haikuwezekana.

“Serikali kwa uwazi kabisa ilieleza kuhusu mkwamo huo, Waziri (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) alisema, mapendekezo hayo hayakufikishwa bungeni kwa kuwa kuna hatua zilikuwa hazijakamilika. Hii ni dhamira ya wazi kabisa ya serikali hii,” amesema.

Amesema, kazi iliyobaki sasa ni upande wa serikali kukamilisha mchakato na kisha mapendekezo hayo kupelekwa bungeni kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Wito wangu, mchakato huo uende kwa kasi ile ile kwa sababu mabadiliko hayo yatawezesha waandishi wa habari kuwa huru zaidi, pia kufanya kazi zao kwa weledi kwa sababu, vile vitu ambavyo tuliviona ni vikwazo, vitakuwa vimeondolewa.

“Mambo hayo yanayokwaza uhuru wa habari yakiondolewa, yatasaidia sana maendeleo ya nchi yetu kwa sababu, habari ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, mchakato huu unakwenda kwa kuwa, rais aliyepo madarakani ana dhamira njema na sekta ya habari.

Na kwamba, baada ya wadau wa habari kufanya vikao serikali, wadau wanasubiri matunda ya vikao hivyo kwa kupelekwa mapendekezo ya wadau wa habari bungeni.

“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na waziri husika ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” amesema Balile na kuongeza:

“Tulifanya mkutano wa mwisho mwezi Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni.”

Hivi karibuni, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari ili wabunge wakiridhia utekelezaji wake ufanyike.

“Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia, tuendelee na utekelezaji wake,” alisema Msigwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news