PELE:Hebu cheza kama Pele...

NA LWAGA MWAMBANDE

DESEMBA 29,2022 gwiji wa soka duniani, Edison Arantes do Nascimento (Pele) ambaye ni raia wa Brazil amefariki.
Pele ndiye anayechukuliwa kuwa mchezaji bora zaidi wa soka ambaye ujuzi wake uwanjani ulisaidia kuutangaza kama mchezo mzuri, amefariki kufuatia mapambano ya mwaka mzima dhidi ya saratani ya utumbo.

Binti yake, Kely Nascimento alithibitisha kifo hicho kwenye Instagram yake,"Kila kitu tulichonacho ni kwa sababu yako. Tunakupenda sana. Pumzika kwa amani," Kely Nascimento aliandika.

Nyota huyo ambaye alizaliwa Oktoba 23, 1940 amefariki akiwa na umri wa miaka 82 katika Hospitali ya Israeli ya Albert Einstein huko São Paulo, Brazil.

Pele anahesabiwa na wengi wakiwemo wachambuzi mahiri wa soka duniani na mashabiki, kuwa mchezaji bora zaidi wa wakati wote.

Wakati wa uhai wake, kabla ya kustaafu soka, alicheza kama mshambuliaji wa kati. Aliisaidia Brazil kutwaa Kombe la Dunia 1958, 1962 na baadaye tena mwaka 1970.

Gwiji huyo aliweka rekodi mwaka 1958 ya kuwa mchezaji mdogo kuliko wote duniani kucheza katika fainali ya Kombe la Dunia alipocheza akiwa na umri wa miaka 17. Alivuma sana katika miaka ya 1970 duniani kote.

Mwaka 1999 alichaguliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa mchezaji bora wa karne. Kwa mujibu wa FIFA, Pele alikuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga magoli 1281 kati ya mechi 1363. 

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasema shujaa wa soka ameondoka akiwa ameacha kumbukumbu njema duniani. Endelea;

1. Hebu cheza kama Pele,

Hebu cheza kama Pele,

Ni maneno yako mbele,

Ameshatutoka Pele.


2. Kweli hapa duniani,

Fikiri ya mpirani,

Hajatokea dimbani,

Maarufu kama Pele.


3. Miongoni wachezaji,

Walojaliwa kipaji,

Na miguuni mtaji,

Hakuwepo kama Pele.


4. Kwenye kombe la dunia,

Jinsi alivyowania,

Mara tatu jitwalia,

Hapo peke yake Pele.


5. Sasa ndio kaondoka,

6. Uhai umekatika,

Vizuri tamkumbuka,

Huyu mfalme Pele.


7. Leo hapa duniani,

Waendao viwanjani,

Watashusha vichwa chini,

Wakimkumbuka Pele.


8. Huyu nyota wa dunia,

Mwafrika asilia,

Ambaye twajivunia,

Ndiyo kafariki Pele.


9. Mshambulia hatari,

Kukutana jihadhari,

Alifanya kazi nzuri,

Ameshatutoka Pele.


10. Brazil ilitamba,

Duniani kuwa mwamba,

Sababu ya huyu mwamba,

Ameshatutoka Pele.


11. Kuna simulizi hii,

Isikie uitii,

Kutoka kwa timu hii,

Ameshatutoka Pele.


12. Ile timu ya Santos,

Na Pele kwenye kikosi,

Ilivyopaa kwa kasi,

Ameshatutoka Pele.


13. Ikaja Inter Milan,

Fedha zao mkononi,

Pele awe wa Milan,

Ilishindikana Pele.


14. Mara ya pili wakaja,

Na pesa nyingi za haja,

Santos kujenga hoja,

Wala hakuuzwa Pele.


15. Inter Milan wabishi,

Na wala hauwachoshi,

Na walikuwa na keshi,

Hawakumpata Pele.


16. Sema kiasi chochote,

Ili Pele tumpate,

Waache Inter wagote,

Hawakumpata Pele.


17. Kwa Santos huyo Pele,

Jina lilikuwa mbele,

Na utambulisho tele,

Wasingemuuza Pele.


18. Kwamba kumuuza Pele,

Ingelileta kelele,

Santos ifie kule,

Huyu hasa ndiye Pele.


19. Brazil nchi yake,

Ndiye Pele peke yake,

Balozi aina yake,

Ameshatutoka Pele.


20. Kweli wako wachezaji,

Ubora si wa kuhoji,

Kwa nchi zao mitaji,

Lakini si kama Pele.


21. Kulikuwako na watu,

Wale walifanya vitu,

Ambavyo kwetu ni kuntu,

Mmojawapo ni Pele.


22. Tazidi kumbukwa Pele,

Ametangulia mbele,

Tunalia kwa kelele,

Hatunaye tena Pele.


23. Wengi hatukumuona,

Ila yake tumeona,

Na yake twatambiana,

Ameshatoweka Pele.


24. Vipi waliomuona,

Ni vipi wanajiona,

Wamepungukiwa sana,

Ameshatutoka Pele.


25. Brazil wanalia,

Wachezaji wanalia,

Hata FIFA inalia,

Ameshatutoka Pele.


26. Vyombo vya habari vyote,

Wapenda michezo wote,

Kwa jumla watu wote,

Wanamlilia Pele.


27. Ingawa ameondoka,

Jina lake latukuka,

Vile aliwajibika,

Ndio kaondoka Pele.


28. Kwetu huyo ni fundisho,

Tusifanye ya michosho,

Iliyojaa mipasho,

Kamaliza kazi Pele.


29. Dunia yaomboleza,
Pele ngwe kamaliza,

Miaka amekoleza,

Ndiyo kaondoka Pele.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news