RAHA KUWA NA MJOMBA

NA ADELADIUS MAKWEGA

KANISA la Anglikana Tanzania linaundwa na mapokeo ya aina mbili ambayo ni Makanisa ya Kiinjili (Evangelicals) na Mapokeo ya Kikatholiki (Anglo Catholical).
Kutoka kushoto ni John Malecela, Enock Kamuzora, Askofu Yohana Madinda, Mwalimu Julius Nyerere na Job Lusinde.

Mnamo mwaka wa 1970 Kanisa la Jimbo la Afrika Mashariki (CPEA) la makao makuu yake jijini Nairobi, Kenya liligawanyika na kuunda majimbo mawili moja likiwa Kanisa la Jimbo la Tanzania (CPT), jimbo huru ndani ya Ushirika wa Anglikana.

Katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1970 Askofu Mkuu John Mhina Sepeku alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Jimbo la Tanzania na kutawazwa na Askofu Leonard Beecher katika Kanisa la Nikolao Ilala jijini Dar es Salaam.

Dayosisi kongwe za kanisa hili ni ya Zanzibar (1892), Masasi (1926) na Central Tanganyika (1927). Sasa mama wa mwanakwetu alizaliwa katika Dayosisi ya Central Tanganyika ambayo ilijumuisha maeneo yote ya Dodoma na Bonde la Ufa ambayo sasa sehemu ya Manyoni mkoani Singida.(Dayosisi ya Mpwapwa na Dayosisi ya Rift Valley ziliazishwa mwaka 1991).

Askofu Alfred Stanway aliagwa rasmi katika Kanisa la Roho Mtakatifu Dodoma Juni 20, 1971 nafasi yake ikachukuliwa na Askofu Yohana Madinda.

Mwaka 1979 mwanakwetu na mama yake ambaye alikuwa mjamzito walisafiri kutoka Kijiji cha Berege Mpwapwa kuja Dodoma Mjini kumsalimia mjomba wa mwanakwetu aliyekuwa anafanya kazi katika ofisi ya Dayosisi ya Central Tanganyika kama fundi magari.

Huyu mjomba wa mwanakwetu aliyefahamika kama John Mlemeta aliaminiwa sana kwa kazi hiyo na hata akawa anatengeneza magari ya Baba Askofu Madinda huku Baba Askofu huyu aliwasomesha wazazi wa mjomba wa mwanakwetu huko Shule ya Msingi Kilimantinde. (Hezron na Elizabeth) Huyu mjomba wa mwanakwetu-fundi magari alikuwa akiishi katika makazi ya Baba Askofu ili kutimiza majukumu yake kwa uhakika.

Mwanakwetu kumbuka yupo kwa mjomba wake katika makazi ya Baba Askofu wa Kanisa Angilikan na hata kucheza anacheza na watoto wa Baba Askofu michezo kama vile Kula Mbakishie Baba, Baba Kasema, Kombolela na Soka.

Siku moja jioni mjomba wa mwanakwetu akasema kwa kuwa wajomba zake wamefika kwa mara kwanza basi atachinja bata mkubwa kwa heshima yao. Hapo mwanakwetu sikukuu ya Noeli imekaribia wanakula nyama kabla ya sikukuu, raha ya kuwa na mjomba.

Kulipokucha tu katika makazi haya watoto wakawa wanacheza, mwanakwetu akakumbuka maneno ya mjomba wake kuwa leo bata anachinjwa.

Mwanakwetu akachukua kisu akaanza kumkimbiza bata mkubwa ambaye alionekana kila siku anasumbua bata wengine.

Hapo watoto wengine wanamsaidia wakiwamo watoto wa Baba Askofu, Vipi mwanakwetu ? “Mjomba kasema tumchinje bata.” Bata dume mkubwa akakamatwa na kuchinjwa, watoto wanashangilia. Mwanakwetu akambeba bata hadi kwa mjomba kumkabidhi.

Mjomba wa mwanakwetu akasema sawa mjomba umefanya kazi nzuri, lakini huyu bata siyo wangu ni wa Baba Askofu Madinda tunafanyaje mjomba? Mwanakwetu umechinja bata wa mkubwa ! Mjomba nitafukuzwa kazi.

Kweli alifuatwa Baba Askofu Madinda na kuelezwa kuwa bata wake amechinjwa na mjukuu wa mwanafunzi wake aliyemfundisha Shule ya Msingi Kilimatinde wakati wa mkoloni, lakini pia mjomba wa mtumishi wake anayemtengenezea magari.

Baba Askofu Madinda alifurahi mno akataka kumuona mwanakwetu ambaye wakati huo akiwa na umri wa miaka kama mitano tu.

“Bwana Hezron huku mjukuu wako ameshachinja bata wangu wa Noeli, sasa itabidi uje kulipa bata wangu maana baba Askofu sina bata kwa kula sikukuu ya Noeli.” Baba Askofu Madinda mtu mwema na mpole alizungumza kwa simu kwa utani na mwanafunzi wake aliyekuwa mbali na hapo.

Wakiwa nyumbani kwa Baba Askofu mwanakwetu katulia tuli anasikiliza kipi kitaendelea?. Baba Askofu alimuombea mama wa mwanakwetu aliyekuwa mjamzito akatoa jina la mtoto ambaye alikuwa anatarajiwa kuzaliwa “Huyu atakayezaliwa ataitwa Michael.”

Mjomba wa mwanakwetu huku kabeba bata mikononi wa kulipa bata aliyechinywa Baba Askofu akakataa kumpokea akisema , “Kitukuu changu kimechinja bata wangu” Bata akarudi nao kwake na mwanakwetu akala nyama ya bata wa Baba Askofu Madinda.

Siku iliyofuata mama wa mwanakwetu akasafiri na watoto wake wawili kuelekea Kilosa walipo wazazi wake kujifungua.

Walipofika huko mama wa mwanakwetu alijifungua mtoto wa kiume aliyepewa jina la Michael jina ambalo lilitolewa na Baba Askofu Madinda wakati wa kesi ya bata Dodoma.

Mwanakwetu alikaa na mama yake na wadogo zake wawili Chuo Cha Maendeleo Ilonga Kilosa kwa muda. Wakiwa pale Babu wa mwanakwetu kila Jumatatu hadi Ijumaa alikuwa mkutubi wa Chuo cha Maendelo Ilonga, lakini Jumapili alikuwa akiingia kanisani na kusalisha kama mchungaji wa Kanisa la Anglikan hapo hapo Kilosa.

Walikaa hapo na baadaye kurudi Berege Wilaya Mpwapwa ambapo Michael alibatizwa katika Kigango Katoliki cha Berege na wakati huo kulikuwa na kanisa dogo ambalo Padri alikuwa akifika hapo mara chache mno kwa pikipiki. Mwanakwetu hakumbuki Padri huyu alikuwa akitokea wapi, msimamizi wa ubatizo huo alikuwa ni Honesta Fidelis Makwega miongoni mwa Binti Makwega wakati huo akitokea Dar es Salaam.

Mwanakwetu leo hii amekikumbuka kisa hiki, lakini anakuomba sana msomaji wake tilia maanani babu yake huyu mkutubi wa Chuo cha Maelendeo Ilonga na huku akijitolea kama mchungaji Kanisani la Angalikan, mzee huyu mikono yake ilibeba mambo mawili kushoto ukutubi-mshahara na kulia uchungaji–Yule aliyekuwa anampa pumzi.

Je? Leo hii mimi na wewe huyu anayetupa pumzi tunamlipa kitu gani katika kila siku inayokwenda kwake?

makwadeladius@gmail.com
0717649257

MUHIMU

Mwanakwetu anaendelea kukutakia heri ya Noeli na mwaka mpya 2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news