Rais Dkt.Mwinyi asema...

NA DIRMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, tatizo la mfumko wa bei za bidhaa na huduma kwa wananchi ni suala mtambuka ambalo huchangiwa na sababu nyingi zikiwemo mfumuko wa bei ulimwenguni kutokana na mabadiliko ya Dunia ikiwemo vita vya Urusi na Ukraine sambamba na changamoto zinazobasabishwa na ufinyu wa bandari ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali ikiwa ni kawaida yake kukutana nao kila mwisho wa mwezi, mkutano huo umefanyika leo Desemba 31, 2022 katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Amesema, kupanda kwa bei za bidhaa sio tatizo lililopo Zanzibar pekee, lakini ametolea ufafanuzi kwa sababu zilizo ndani ya mamlaka za Serikali kuchukuliwa hatua za haraka ili kupunguza ukali wa maisha ikiwemo kuboresha ufanisi na utendaji wa utoaji huduma kwenye bandari ya Zanzibar ili kupunguza athari kali kwa wananchi.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 31, 2022 wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano wake na waandishi hao anaoufanya kila mwisho wa mwezi kwa kuzungumza nao pamoja na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
“Kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa, nataka niseme kwamba ziko sababu nje ya uwezo wa Serikali hatuna jinsi, zikiwemo kupanda kwa bei za bidhaa huko zinakotoka, kuna baadhi ya mataifa wamezuia kuuza bidhaa zao nje ya nchi kwa ajili ya kujiwekea akiba kutoka na vita wa Urusi na Ukraine, hali iliyochangia kupungua kwa uingizwaji wa bidhaa nchini, hayo na mengine ndio yanayosababisha bidhaa za chakula duniani kupanda sio Zanzibar peke yake” amefafanua Rais Dkt.Mwinyi.

Akizungumzia mfumuko wa bei kwa bidhaa za Zanzibar, Dkt.Mwinyi ameeleza bidhaa nyingi za vyakula zinatoka Tanzania Bara ambako pia bidhaa zimepanda bei kutokana na ukame ulioikumba baadhi ya mikoa na kuongeza kuwa ukame umepunguza uingizwaji wa bidhaa na kusababisha bidhaa chache zilizopo kupanda bei.

Bandari

Pia amesema, changamoto nyingine ni ufinyu wa mazingira ya Bandari ya Malindi, hali aliyoielezea kuchangia kuzorotesha zoezi la kushushwa kwa mizigo bandarini hapo.
“Bandari yetu ufanisi wake ni mdogo sana, sababu ina gati moja, meli zinakuja zinakaa sana, zikifuatana meli tatu nne, wa mwisho atashusha mzigo baada ya mwezi mmoja,”amebainisha Rais Dkt.Mwinyi.

Amesema, Serikali imechukua hatua ya kupunguza baadhi ya changamoto ikiwemo kutumia Bandari ya Mangapwani ili kupunguza msongamano kwenye Bandari ya Malindi na kutoa wepesi wa bidhaa nyingi kushushwa kwa wakati na kuwafikia wahitaji ambao ni wananchi.

Miaka 59

Akizungumzia suala la Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar,Rais Dkt.Mwinyi amesema, kwa mwaka 2023 hakutakua na sherehe kubwa badala yake gharama zilizopangwa kuadhimisha sherehe hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ambapo Dkt. Mwinyi alieleza fedha hizo zimepelekewa kuongeza nguvu Wizara ya Elimu.
Alieleza, awali sherehe za Mapinduzi zilipangwa kutumia shilingi milioni 700 licha ya gharama kupunguzwa hadi kufikia shilingi milioni 450 ambazo fedha hizo Rais Mwinyi amesema Serikali imezielekeza kuongeza nguvu kwenye miradi ya sekta ya elimu ikiwemo kuongezwa kwa madarasa, madawati, maabara na huduma nyingine za elimu.

Afya

Kuhusu Sekta ya Afya, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza katika kuboreshwa huduma za afya kwenye vituo vya afya, Serikali imekuja na utaratibu mpya wa kutoa huduma kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuboresha huduma bora kwa wananchi na kuongeza kuwa Serikali kupitia hospitali za wilaya na mikoa zitatoa huduma zote na suala la huduma za maabara zimeelekezwa kwenye sekta binafsi ili kuipa wepesi serikali kuwahudumia zaidi wananchi.
“Sekta ya afya tumekuja na utaratibu mpya wa kutoa huduma zifanywe na sekta binafsi (outservices), kwa hivyo maabara za hospitali hizi mpya za wilaya na mikoa huduma zitatolewa na sekta binafsi, lile suala la mashine imeharibika sasa hivi hakuna tena, huduma zote za vipimo vya X -ray, MRI na huduma nyingine za kimaabara zimepelekwa huko,”amefafanua Dkt.Mwinyi.

Ajira

Kuhusu kutatua changamoto ya ajira nchini, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza tayari Serikali imezungumza na balozi zake zilizo nje ya nchi ili kuangalia uwezekano wa kuwapata mawakala wa ajira na kuweka taratibu rasmi za ajira ili kukwepa lawama za baadae na ukiukwaji wa haki za binadamu zinazovunjwa na baadhi ya waajiri kwa baadhi ya nchi.
“Tumeshazungumza na mabalozi wetu, watutafutie wale watu wanaoajiri tuwaunganishe na mawakala wa huku ili vijana wetu waweze kufanyakazi nje,”amefafanua Rais Dkt.Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi amekuwa akitumia utaratibu wa kuzungumza na waandishi na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwa ni utaratibu wake wa kusikiliza na kutatua moja kwa moja changamoto zinazowakabili wananchi ambao baadhi yao humfikishia Mhe.Rais kupitia vyombo hivyo, na huu ni mkutano wa mwisho kwa mwaka 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news