NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, wauguzi na wakunga katika hospitali za Zanzibar wanatakiwa kutoa huduma nzuri na bora ili kwenda sambamba na juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha sekta ya afya.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 20, 2022 wakati wa sherehe ya kumpongeza kwa kufikisha miaka miwili tangu aingie madarakani.
Ni sherehe zilizoandaliwa na wauguzi pamoja na wakunga wa hospitali za Zanzibar zilizofanyika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi jijini Zanzibar.
Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, jitihada zinapaswa kuongezwa kusomesha wanataaluma zaidi kuhakikisha huduma bora zaidi zinapatikana katika hospitali nchini pamoja na zile mpya zinazoendelea kumaliziwa kujengwa.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi, alisema pia ili kuboresha huduma za afya nchini kuna umuhimu wa kutoa fursa kwa baadhi ya huduma zitolewe na hospitali binafsi.
Wakati huo huo amesema,baada ya hospitali zinazojengwa kukamilika zisiwe na uzuri wa majengo yanayopendeza bali huduma zitakazotolewa ziwe bora zaidi ili kuendana na majengo yenyewe.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameridhia kuanzishwe Kurugenzi ya Afya katika Wizara ya Afya ili kurahisisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Hata hivyo, kuhusu ombi la wauguzi la posho maalum,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameahidi kuzitatua changamoto hizo mara baada ya ukaguzi wa hesabu.
Tags
Habari
Sekta ya Afya Zanzibar
Yajayo Zanzibar Yanafurahisha
Zanzibar
Zanzibar Habari
Zanzibar News