NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuzindua rasmi Taasisi ya ‘Presidential Delivery Bureau (PDB) katika hafla itakayofanyika Ikulu jijini Zanzibar.
Mawaziri wa wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mafunzo ya kuwajengea uelewa viongozi na watendaji kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali yaliyofunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Mhe.Jamal Kassim Ali (hayupo pichani) katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-Wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Hayo yameelezwa Desemba Mosi, 2022 na Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Ikulu,Jamal Kassim Ali katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uelewa viongozi na watendaji kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Sheikh idrissa Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.
Akizungumza na Washiriki wa Mafunzo hayo, Waziri Jamal amesema,taasisi hiyo itakuwa na jukumu la kusimamia masuala yote kuhusiana na utekelezaji wa vipaumbele vya mipango na mikakati ya Serikali.
Amesema, madhumuni ya kuwepo kwa mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa viongozi na watendaji hao ili kufahamu madhumuni, majukumu na kwa namna gani chombo hicho kitafanya kazi zake.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ‘Presidential Delivery Bureau’ Dr. Josephine Kimaro, alisema utekelezaji wa Vipaumbele vya Miradi ya Serikali utahusika katika maeneo Mkuu manne makuu, akiyataja kuwa ni Sekta ya Uchumi wa Buluu, sekta ya Utalii, Miundombinu pamoja na Maendeleo ya kijamii.
Amesema, utekelezaji wa vipaumbele vya miradi ya Serikali kupitia Mawizara kwa kiasi kikubwa vina mnasaba na mikakati mbalimbali ya Serikali, ikiwemo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mtendaji huyo ameeleza umuhimu mkubwa wa kuwepo ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa vipaumbele hivyo kati ya Wizara za Serikali, kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa baadhi ya miradi unahusisha zaidi ya wizara moja.
Ametumia fursa hiyo kuzishukuru Taasisi za Tony Blair, Shirika la Mpango wa Maendeeo la Umoja wa Mataifa (UNDP), pamoja Taasisi ya TBI kwa kufanikisha uanzishaji wa taasisi hiyo pamoja na misaada na utayari wao katika kufanikisha malengo yaliowekwa.
Pia ametoa wito kwa wadau wote,ikiwemo Wizara za Serikali, Taasisi zisizo za Kiserikali pamoja na washirika wa maendeleo kuzungumza dhana hiyo kwa sauti moja ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele ya miradi ya serikali.
Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Ahmeid Said amesema, kuanzishwa kwa taasisi hiyo itakuwa ni chachu kwa watendaji wa Serikali kufahamu uwepo wa taasisi hiyo na kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa weledi.
Amesema, kuundwa kwa chombo hicho kutachochea utekelezaji wa vipaumbele wa miradi mbalimbali ya Serikali kwa viongozi na watendaji wa Serikali na kufanikisha malengo yaliowekwa kwa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa usahihi na kwa weledi.
Pia amesema chombo hicho kipo ili kuhakikisha ufanisi unapatikana katika utekelezaji wa vipaumbele ya miradi ya Serikali katika wizara mbalimbali pamoja na kuondoa vikwazo vinavyotokana na urasimu, ikiwemo vile vya kifedha pamoja na rasilimali watu.
“Chombo hiki hakikuanzishwa kwa ajili ya ku-replace utendaji wa Serikali, utendaji wa serikali upo pale pale,” amesema.
Amepongeza Taasisi ya Tony Blair kwa kusaidia uanzishaji wake, sambamba na kufanikisha utekelezaji wa vipaumbe vya miradi ya Serikali kupitia maeneo yalioainishwa.
Mafunzo hayo ya siku moja yalioandaliwa na Wizara Nchi (OR), Ikulu Zanzibar yaliwahusiha Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zazibar, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wakuu wa taasisi za Serikali.