NA JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa hundi za mamilioni ya fedha kwa wadau waliokidhi kukopa kwenye Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.


Aidha, wakati wa uzinduzi huo wadau wa tano kati ya kumi na tisa waliowasilisha maombi yao walipatiwa fedha za mfuko huo.Amefafanua kuwa dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samiaa ni kuona kuwa kila Mwananchi (msanii au mdau wa sanaa) mwenye sifa ya kukopa kwenye mfuko aweze kupata fedha ya kuboresha kazi zake.
“Naomba nieleweke vizuri fedha hizi ni za kila mtanzania, kila mwana sanaa, kila Kijiji, kila kata, kila wilaya, kila mkoa, yule ambaye anaamini ana kazi yake ameitengeneza, yule ambaye anaamini ameandaa muswada wake vizuri, awe Tanga awe Dodoma awe songea, awe Mtwara atazipata ikiwa tu ana sifa,” amefafanua Waziri Mchengerwa.
Amelielekeza Baraza la Sanaa nchini kuandaa utaratibu wa kutengeneza mfumo ya kimtandao ambao utawafanya waombaji kutoka sehemu mbalimbali nchini kuweza kuomba wakiwa huko huko na kupatiwa huduma badala ya kusumbuka kuja Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hassan Abbasi alimtambulisha Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni Sanaa, Bi.Nyakaho Mturi Mahemba.