Rais Samia anavyoivusha Sekta ya Habari kutoka madhila ya miaka kadhaa-3

NA GODFREY NNKO

Wameeleza kuwa, iwapo bodi hiyo ya kitaaluma haitaingizwa mkono wa serikali katika uundwaji wake, Serikali itapata sehemu ya kwenda kupeleka malalamiko yake pale itakapokwazwa na habari ama mwanahabari. Endelea...
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye tangu aingie madarakani, Serikali yake imekuwa rafiki mwema na Sekta ya Habari nchini na tayari ametoa nafasi kwa ajili ya kufikia hatua za maboresho ya sheria ambazo zinadaiwa ni kandamizi katika sekta hiyo nchini.

ZINAZOHUSIANA



Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam wameeleza kwamba, kuundwa kwa chombo hicho, kutakuwa mwarobaini wa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwenye vyumba vya habari mbalimbali nchini.

Nevile Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Katibu Mstaafu wa taasisi hiyo amesema, iwapo serikali itaamua kuunda Bodi ya Ithibati ya Habari, basi bodi hiyo itakosa uhuru wa kufanya uamuzi pale malalamiko yatakapoihusu yenyewe Serikali.

Amesema, ili kukwepa hilo na kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, hakuna budi kwa Bodi ya Ithibati ya Habari kuundwa na kusimamiwa na wanataaluma wenyewe ambao ndio wanahabari.

“Bodi ya Ithibati ya Habari ikisimamiwa na serikali, itakosa uhuru wa kuamua. Hiyo, bodi inapaswa kuundwa na Wanataaluma na kazi yake ni ya kitaaluma. Serikali ikiwa na malalamiko nayo inakwenda kulalamika kwenye bodi na wala haipaswi kutoa maelekezo,” ameeleza Meena.

Mashaka

Joseph Kulangwa, Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema ameonesha wasiwasi iwapo serikali itasimamia uundwaji wa bodi hiyo akisema “serikali itataka wanaowaandika vizuri tu, ndio wahalalishwe kufanya kazi hiyo.”

Amesema, tasnia mbalimbali nchini zimeunda na kusimamia bodi zao wenyewe bila maelekezo ama kuingiliwa na serikali, amehoji sababu za serikali kupendekeza kuunda bodi hiyo badala ya kuwaacha wanataaluma wa habari kuunda na kusimamia bodi hiyo.

“Tasnia inatakiwa kujidhibiti yenyewe kama wanavyofanya wanasheria na wengine. Serikali ikiwa ndiye mdhibiti wa bodi hiyo, kutakuwa na upendeleo kwa magazeti so called (yanayoitwa) ya umma,” amesema Kulangwa.

Jimmy Charles, Mhariri wa Jarida la Tz & Beyond pia PANAROMA amesema, iwapo serikali itaunda bodi hiyo, itajihakikishia uhuru wa Habari kutuama mikononi mwake.

“Serikali ikiundwa bodii kama inavyoelekezwa na sheria, basi uhuru wa habari utaendelea kutuama kwenye mikononi yake (serikali).

“Ikumbukwe kuwa, kwa sasa serikali ndio mwamuzi wa mwisho kwa maana ya kuwa ndio mlalamikaji, msikilizaji na hakimu kwa wakati mmoja. Na ukitaka kujua hilo, utaona pale tu utakapogusa kile isichopendezwa nacho (serikali).

Jimmy amesisitiza kuwa, “Tasnia ya Habari inahitaji bodi huru isiyosimamiwa na Serikali.”

Mei 31, 2021 aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kabla tasnia ya Habari kuhamishiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tasnia ya Habari) alisema, serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati itayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

Bashungwa alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha makadiro ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, inaelekeza kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari pamoja na mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.

“Kwa sasa wizara inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi hii,” alisema na kuongeza Baraza Huru la Habari litaundwa baada ya Bodi ya Ithibati kuanza kazi.”

Mwanasheria Mkuu

Kwa upande wa Jaji Dkt.Eliezer Mbuki Feleshi ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema ni vizuri kwa Bodi ya Ithibati ya Habari ikaundwa na kusimamiwa na wanahabari wenyewe.

Jaji Feleshi alitoa maoni hayo hivi karibuni wakati alipokutana na wadau wa habari ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.

Wadau hao waliongozwa na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF na James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA-TAN, ambapo walimkabidhi Jaji Feleshi mapendekezo ya mabadiliko ya sheria zinazominya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

"Sina tatizo, naona muwe na 'regulator', bodi yenu moja, ili mmoja wenu akienda kinyume na maadili (ya uandishi wa habari), mnamshughulikia nyinyi wenyewe.

"Nipo nanyi na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) katika hatua ya kuelekea mabadiliko ya sheria za habari,"amesema Mhe.Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Juni 13,2022, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma alipokutana na wadau wa habari nchini.

Waziri Nape

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewahakikishia wadau wa habari kuwa, Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari nchini hayatapelekwa bungeni bila pande zote kukubaliana na kuridhika.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Alifafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.

"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana.

"Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona, kwa hiyo Serikali ipo tayari...mwishowe tutakubaliana, nchi ni yetu wote,"alisema Mheshimiwa Nape.

Mbunge

Kwa upande wake,Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga mkoani Dar es Slaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kushirikiana na wabunge wenzake katika kuhakikisha tasnia ya habari inakuwa na sheria rafiki zinazotekelezeka.

‘‘Mimi na wabunge wenzangu tutashirikiana. Dunia imebadilika na hatuwezi kubaki hapa tulipo,"amesema Jerry na kuongeza, ‘‘nitazungumza na wenzangu na kisha tutaona namna ya kufanya.’’

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 imeweka mazingira makubwa ya kumuhofisha mwandishi wa habari.

Na kwamba, ndani ya sheria hiyo kuna vipengele mbalimbali kwa undani wake, vinaua tasnia ya habari akitolea mfano kipengele kinachompa nguvu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kufungia chombo cha habari kwa namna anavyoona inafaa.

‘‘Katika safari ya mabadiliko haya, tumeungana na taasisi zote za habari ili kuwa na kauli moja. Tumeunganisha nguvu ili kufikia lengo,"amesisitiza.

James Marenga, Mjumbe wa CoRI kutoka Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania amesema,tasnia ya habari haina tofauti na tasnia nyingine nchini katika utendaji kazi.

Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea amesema, ikiwa mawakili wanatengeneza taratibu zao na kuzifanya kuwa rejea katika kazi zao, inashindikanaje wanahabari nao wakajiwekea utaratibu wa ‘kujihukumu’ kama ilivyo tasnia nyingine?.

‘‘Mimi ni mwanasheria, katika taasisi yetu tulitengeneza cord of conduct wenyewe na hizo ndio zinatuongoza, ni busara na wanahabari wakawa na utaratibu wao kisheria unaosimamiwa na wenyewe katika kuhakikisha maadili ya uandishi wa habari yanafuatwa,’’ amesema.

Jessy Kwayu, Mkurugenzi Mkuu wa Media Brains Inc Ltd amesema, Sheria ya Habari ya mwaka 2016 ilipitishwa katika mazingira ambayo si rafiki.

‘‘Vipengele 19 vya sheria hiyo vilijaribiwa kwenye sheria za nchi, vikaonekana kutoingia katika mizani ya kisheria,’’ amesema Kwayu.

Rose Reuben, Mkuu wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) amesema, kwa mazingira ya sasa, waandishi wanashindwa kuandika habari kwa uhuru.

Wanahabari

Kwa nyakati tofauti, waandishi na wadau wamesema kuwa, panapotokea tofauti baina ya wamiliki wa vyombo vya habari na Serikali, hadi kusababisha vyombo husika kufungiwa, waathirika wakubwa ni wafanyakazi ambao sehemu hiyo imekuwa ikiwapa kipato cha kuendesha familia zao.

"Awali ya yote, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameonesha kutujali sana wanahabari na tasnia hii kwa ujumla, ule moyo tu wa kuonesha utayari wa tasnia hii kuthaminiwa zaidi katika Serikali yake inatupa majibu kuwa, hata kasoro ndogo ndogo ambazo zinaonekana katika vifungu vya sheria hizo zitafanyiwa maboresho na tutafanya kazi kwa uhuru na vyombo vya habari thamani yake itarudi kwa kasi,"anasema mmoja wa wadau wa habari kutoka mkoani Mara, Fresha Kinasa.

Amefafanua kuwa,panapotokea hatua ya vyombo vya habari kukosa biashara au kunyimwa matangazo kunachangia wamiliki wengi kuamua kusitisha biashara na hata wakati mwingine wanashindwa kulipa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi na kodi mbalimbali za Serikali.

"Ni shauku yetu kuona siku moja kila chombo cha habari ambacho kina leseni halali nchini, kinapewa biashara na taasisi yoyote ya umma au binafsi bila kujali ukubwa au udogo wake, hii inamaanisha nini? Wakipata biashara inachochea kasi ya uwekezaji, fursa za ajira na hata kuwa na mwamko wa kulipa kodi kwa wakati serikali, hivyo kuwezesha ustawi wa uchumi wetu. Sekta ya habari ni muhimu sana,"amesema.

Elimu muhimu

Pia kwa nyakati tofauti wadau mbalimbali wa habari wamesema kuwa, suala la elimu kwa waandishi wa habari nchini halikwepeki kwa kuwa, elimu itawezesha taaluma ya habari iheshimike, kuwa na weledi na kuzingatia maadili kwa manufaa ya taaluma, jamii na Taifa kwa ujumla.

Wadau hao wamesema, baadhi ya vituo zikiwemo redio inaonekana watu wengi ambao wanafanya kazi huko, walienda kwa vipaji hivyo kusababisha ule weledi wa uandishi wa habari na utangazaji kukosekana, jambo ambalo halina afya katika tasnia ya habari.

Pia wamesema kuwa,majina mengi ya vipindi unakuta yanafanyika kwa lugha mchanganyiko kwa Kiingereza na Kiswahili, jambo ambalo ni changamoto.

"Suala la elimu ni jambo ambalo linapaswa lisisitizwe, lakini pia wakati wa msisitizo huo nasi waandishi wa habari tutumie muda huo kujiendeleza kielimu, tujisisitize wenyewe wakati tuna mambo mengine tunaomba Serikali ifanye, tunaziomba mamlaka zingine zifanye au taasisi zingine.

"Lakini sisi wenyewe, suala la elimu litusaidie sisi wenyewe, itatusaidia kwa sababu tunahudumia jamii, na hiyo jamii inayohudumia ikipata vitu visivyo maana yake inakuwa ni tofauti, mimi ninaunga mkono sana hoja ya elimu,"amesema mwanahabari Dkt.Tumaini Msowoya.

Naye mwanahabari, Bw.Godfrey Monyo amesema kuwa, elimu kwa wanahabari haikwepeki. "Wakati jitihada mbalimbali zikifanyika za kuhakikisha tunaboresha taaluma ya habari nchini, ninaomba suala la elimu lisisahaulike,watu wahakikishe kwamba maboresho yanakwenda, lakini waandishi wa habari wanasoma.

"Maboresho yawepo lakini, suala la elimu likaziwe mkazo. Mbona taaluma zingine zinajulikana kuwa, kiwango cha elimu ni hiki, naomba suala hili likaziwe mkazo,"amesema Bw.Monyo.

Kwa nini?

Wadau wa habari wanaeleza licha ya nia njema ya Serikali kuja na sheria hizo,Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016 inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 5, 2016 na kuridhiwa na Rais Novemba 16, 2016.

Wanadai kuwa, baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza, pia vinakiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi.

Ibara ya 18 inatoa haki kwa kila mtu kuwa na uhuru wa maoni na kueleza fikra zake, kutafuta, kupokea habari bila ya kujali mipaka ya nchi, uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano hayo.

Aidha, Katiba pia inatoa haki kwa kila mtu kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu katika jamii.

Wamesema, dhamira ya Serikali ya kutunga sheria na kanuni za kusimamia sekta ya habari ni njema kwa lengo la kuongeza ufanisi na ustawi bora, lakini kupitia sheria nne zinazosimamia habari zinahitaji maboresho katika baadhi ya vifungu ili kuepuka migongano ya maslahi, upendeleo, urasimu na wakati mwingine manyanyaso kwa wadau wa habari nchini.

Mbali na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016,pia kuna Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 ambayo inasimamia radio, TV na Mitandao ya Kijamii, Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 zikiwemo kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 ziliyogawanywa katika vipengele mbalimbali.

Waziri wa Katiba

Hayo yalijiri ikiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro alipokutana na uongozi wa TEF na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) hivi karibuni jijini Arusha alisisitiza wakati ni sasa.

Mheshimiwa Waziri alisema, kama kuna wakati mzuri wa kulisukuma suala la kubadili sheria za habari ni sasa.

“Rais tuliye naye sasa, Mheshimiwa Samia (Suluhu Hassan) ameonesha moyo na nia kubwa ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini.

“Kwa sasa mazingira ni mazuri na yanaruhusu. Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, maana mkisubiri miaka 10 ijayo, huwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,”amesema Dkt.Ndumbaro.

Kikao

Akizungumza katika kikao cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI), kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 21,2022,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa, Serikali imepokea mapendekezo hayo na sasa wanayafanyia kazi.

“Serikali inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria na sasa tunayafanyia mapitio ya mwisho ya mapendelezo ya marekebisho ya sheria,”amesema Mheshimiwa Nape.

Pia Mheshimiwa Waziri Nape amesema kuwa, hatua inayofuata baada ya kikao hicho, ni uandishi wa mapendekezo hayo na kisha kupelekwa kwa watunga sheria.

”Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili.Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua.

…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,” amesema Mheshimiwa Nape.

Aidha, baada ya kikao hicho Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alikiri wazi kuwa, kuna muelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Kikao kilikuwa kizuri,Serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.

‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi Serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’amesema Balile.

Aidha, miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa Serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Pia wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Aidha, wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.

Suluhu

Wakati huo huo, Desemba 17, 2022 zaidi ya wadau 1,000 wa habari nchini wakiwemo viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali,wanahabari, wamiliki wa vyombo vya habari, mabalozi na sekta binafsi walikusanyika jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 nchini Tanzania.

Kongamano hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamnhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan la wadau wa vyombo vya habari kukutana ili kujadiliana kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Akizungumzia kuhusu kongamano hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa alifafanua kuwa,hili ni kongamano la kwanza nchini ambalo ni kiashiri chema kwa sekta hiyo nchini tunapojiandaa kuupokea mwaka mpya wa 2023.

"Hii ni siku ya kihistoria katika nchi yetu, tumelianzisha tukio la kihistoria ambalo hatujawahi kuwa nalo tangu nchi yetu izaliwe (ipate Uhuru).

"Kwa sisi wanahabari hii itakuwa ndiyo Krisimasi yetu, ndiyo mwaka mpya wetu, ndiyo funga mwaka yetu. Kwa hiyo ni siku muhimu sana na nina furaha kuona leo tumeungana na Mheshimiwa Waziri wetu kuianza safari hii muhimu katika Sekta ya Habari,"amefafanua Msigwa.

Desemba 1961, Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza na kuendelea kuwa sehemu ya Jumuiya ya Madola na mwaka 1962 Tanganyika ikawa Jamhuri. Tanganyika iliungana na Zanzibar tarehe 26 Aprili 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa zaidi ya miaka 60 sasa,Sekta ya Habari Tanzania inaonekana kuchanua zaidi licha ya changamoto za hapa na pale ambazo Serikali hususani hii ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi hasa upande wa sheria ambazo zinaonekana kuwa na utata.

Lengo likiwa ni kuiwezesha sekta hii muhimu ambayo ni muhimili wa nne wa Serikali ambao si rasmi uweze kukidhi matarajio yake ya kuhudumia wananchi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.

Ikumbukwe, mwaka 1993 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuona umuhimu wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, iliamua kufungua milango na kuruhusu kuanzishwa kwa runinga, redio na magazeti ya binafsi.

Kamisheni ya Utangazaji ilianzishwa Novemba 1993 chini ya Mwenyekiti wake,Mark Bomani na kuanza majukumu ya kupokea maombi na kutoa leseni za redio na televisheni, kufuatilia na kusimamia urushaji wa matangazo ya redio na televisheni pamoja na kufuatilia na kutoa masafa kwa vyombo vya utangazaji vya binafsi.

Mafanikio hayo ndiyo yalifungua safari ya kuikuza sekta hiyo ambayo mpaka sasa hapa nchini kuna mamia ya magazeti/machapisho, redio, runinga na blogu zilizosajiliwa rasmi.

Hivi karibuni Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) kuelekea mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 walipendekeza mambo mbalimbali.

Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Pia wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Aidha, wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2) (b) (lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.

Katika hatua nyingine, Msigwa amefafanua kuwa,kongamano hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Kongamano hili linawakutanisha watu takribani 1000 wanaotoka katika taasisi na maeneo mbalimbali yanaohusiana na vyombo vya habari, tumekutana kwa nia moja la kujadili maendeleo ya Sekta ya Habari.

"Kongamano hili ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa katika wakati wa Maadhimiso ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani,ambapo kwa hapa nchini yaliadhimishwa kwa mkutano wa wadau wa habari uliofanyika Arusha, Mei 3, 2022.

"Mheshimiwa Rais alituagiza kukutana na wadau wote wa vyombo vya habari kujadiliana kuhusu maendeleo ya Sekta ya Habari nchini. Ninayo furaha kwamba tumelitekekeza agizo hili kabla ya mwaka kuisha,"amefafanua Msigwa.

Mwelekeo mpya

Katika kongamano hilo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Nnauye amewahikikishia wadau wa sekta ya habari nchini kuwa, marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 yatafanyika Januari, 2023.

Hii ni miongoni mwa hatua nzuri kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambayo imeonesha kuijali Sekta ya Habari kama injini ya kusaidia kusukuma mbele taarifa chanya kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia ishara hii inatoa mwanga kuwa, huenda sheria nyingine zinazolalamikiwa ikiwemo Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa huenda nazo zikafanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Waziri Nape ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam amesema, mabadiliko hayo ni safari ya kuwezesha kulindwa kwa uhuru wa habari kwa mujibu wa sheria na sio utashi wa viongozi.

Waziri Nape ameeleza kuwa, wakati hilo likisubiriwa, uhusiano baina ya sekta ya habari na sekta ya umma nchini umeendelea kuimarika katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“Hakuna furaha, amani na maendeleo kama uhuru wa habari katika jamii hiyo haupo, hivyo ni muhimu kulinda uhuru wa habari ili vitu hivi viwepo kwenye jamii. Hilo linawezekana na huo ndio msingi wa kongamano hili ambalo linalenga kuleta maendeleo, furaha na msingi wa taifa letu.

“Sheria na kanuni mbalimbali zinaendelea kufanyiwa mabadiliko kwa mujibu wa sheria. Uhuru wa habari unapswa kulindwa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa viongozi. Kiongozi yeyote atakayekuja atalazimika kuulinda uhuru huu kwa mujibu wa sheria hata kama hataki,"amefafanua Mheshimiwa Nape.

Balile

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amesema, kufanyika kwa kongamano hilo ni hatua njema ya kuendelea kuimarika kwa Sekta ya Habari hapa nchini.

"Mheshimiwa Msigwa amesema vizuri hapa, Msemaji Mkuu wa Serikali. Itakumbukwa kwamba, Mei 3, Mheshimiwa Rais alitoa agizo la kukutana na wanahabari wote hapa nchini.

"Lakini, Machi 9 Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilikuwa na Mkutano wa Sita pale Zanzibar ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

"Moja ya maazimio ya Jukwaa la Wahariri Tanzania ni kwamba, Sekta ya Habari tumeganwanyika, sekta ya habari tumetawanyika. Sekta ya habari pamoja na kwamba tuna wizara, lakini tulikuwa huku chini kama hatuna mchungaji,mheshimiwa Waziri niwie radhi.

"Tukasema, tuwe na mkutano angalau mmoja ambao utatukutanisha wote kama wanavyokutana wafanyabiasha, kama wanavyokutana wanasiasa kama wanavyokutana wanasheria.

"Sasa kidogo mwaka huu nikaenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri nikamwambia kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba tuna mkutano na Mheshimiwa Rais, lakini tunadhani ni vema kama wanahabari tukakutana, kuna maafisa habari,kuna watu wa ICT.

"Ya kwamba tukakutana tunaweza kutoka na jambo jema, (Mheshimiwa Waziri) akasema,sasa tuyaunganishe yote mawili, lakini tusifanye kama Jukwaa la Wahariri, maana itaonekana mmejitenga na wenzenu, akasema tushirikiane wote kama wanataaluma liwe kongamano la wadau wote. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri,"amefafanua Balile.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Balile amesema, licha ya kuwepo kwa uhuru wa habari nchini, ameomba uhuru huo ulindwe kisheria.

“Wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru wa habari uliopo nchini, tunaamini serikali italinda uhuru huu kisheria katika Mabadiliko ya Sheria ya Habari yajayo,"amesema Balile.

Mahakama

Hivi karibuni imeelezwa kuwa, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa demokrasia na uhuru wa kutoa habari, vyote vinapaswa kutolewa katika misingi yenye kufuata sheria na haki, ili kusiwepo na uvunjifu wa amani.

Hayo yalisemwa na Rais Mahakama ya Afrika, inayoshughulika na haki za binadamu,Jaji Imani Daud Aboud, katika mafunzo ya wiki moja ya Majaji wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha. Ni mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Alisema, vyote vikifuatwa haoni kama kutakuwepo na uvunjifu wa amani katika nchi za Afrika na kusisitiza kila mmoja kukumbuka wajibu wake wenye lengo la kulinda amani ya nchi husika.

Rais huyo alitoa wito wa kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu, akisema bado haki hizo zinavunjwa na kuuweka mashakani uhuru wa demokrasia katika nchi nyingi Afrika.

Pia alisema uhuru wa vyombo vya habari na usalama wao ni jambo muhimu, linaloheshimu misingi ya utawala wa kisheria na demokrasia, hivyo majaji wana wajibu wa kuhakikisha wanahabari wanakuwa na uhuru wa kupewa habari na usalama wao katika nchi za Afrika.

Alisisitiza kwa wanahabari kuhakikisha wanafuata misingi ya uandishi wa habari zinazoeleza uhalisia na ukweli wa jambo, ili kuepuka kuleta mfarakano na machafuko ya ndani ama nchi kwa nchi.

“Mahakama za nchi katika Umoja wa Afrika, zinaweza kushirikiana na vyombo vya habari kutoa habari zinazohamasisha amani kuliko habari zenye kuleta mtafaruku,”alisema Rais Jaji Imani Daud Aboud.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news