NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha wanawake kwa kuhakikisha inatanua mtandao wa wanawake katika sekta mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Ethiopia Mhe. Sahle-Work Zewde pamoja na viongozi mbalimbali Wastaafu wa Afrika wakiwa kwenye Mkutano wa Mtandao wa Viongozi Wanawake wa Afrika uliofanyika Zanzibar leo Desemba 3, 2022. (Picha na Ikulu).
Rais Samia amesema hayo leo katika Kongamano la Nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (African Women Leaders Network - AWLN) lililofanyika Zanzibar.
Aidha, Rais Samia amesema lengo la kuwashirikisha wanawake ni kuweza kufikia Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025.
Rais Samia pia amesema maendeleo ya wanawake yamekuwa yakiathiriwa na changamoto mbalimbali kama kutokupata rasilimali, kutengwa, kutokupata haki zao na kutokupewa nafasi katika kufanya maamuzi.
Vile vile, Rais Samia amesema takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2021 idadi ya wanawake walioajiriwa ilishuka ambapo wanawake milioni 45 duniani waliondoka katika ajira mwaka 2021 na hivyo kuwafanya kuwa maskini zaidi.