Rais Samia anavyoivusha Sekta ya Habari kutoka madhila ya miaka kadhaa

NA GODFREY NNKO

MWAKA 2015, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu ambao ulimuweka madarakani Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, kwa sasa ni marehemu.

Kwa muda mfupi, Rais Dkt.Magufuli alikubalika na wengi kutokana na jitihada zake za kupambana na rushwa ikiwemo aina ya uongozi wake ambao ulijipambanua kwa Hapa Kazi Tu, hali iliyosababisha maofisa wengi wa Serikali kutolewa katika nafasi zao na kuingiza sura mpya.

Utawala huo mpya pia ulichukua hatua madhubuti kuongeza nidhamu katika utumishi wa umma. Hata hivyo, mtindo wa utawala wa Rais Dkt.Magufuli na hasa kuhusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari ulikuwa chanzo cha madhila makubwa katika tasnia hiyo.

Kwa kiasi kikubwa, Rais Dkt.Magufuli alijiimarisha kiutawala,haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza iliathirika kwa kiwango kikubwa.

Aidha, ingawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Katiba ambayo imeeleza haki za msingi za kiraia na za kisiasa, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kujieleza, haki hizi kwa kiwango kikubwa ziliminywa.

Ingawa haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza ni mambo yaliyojumuishwa na yanayolindwa na Katiba ya Tanzania na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu

Sheria kadhaa

Mathalani, katika kipindi cha miaka ya awali tangu aingie madarakani,Rais Dkt.Magufuli kwa maana ya 2015, sheria kadhaa za vyombo vya habari zilipitishwa.

Miongoni mwa sheria hizo ni ile Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ambayo inatajwa kuwa na mianya na madhaifu mengi yanayominya uhuru wa kujieleza.

Nyingine ni Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa na ile Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 ambayo inamtaka mtu yeyote au taasisi kupata idhini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kabla ya kutoa takwimu kwa matumizi ya Watanzania.

Ingawa, Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 ilibadilishwa mwaka 2019, hivyo kuondoa zuio la kuchapisha taarifa ya kitakwimu bila kupata idhini ya serikali,lakini bado takwimu rasmi zimeendelea kuhitaji kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, mara nyingi imetajwa kuipa serikali mamlaka makubwa juu ya maudhui ya habari na utoaji leseni kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari na wadau wanadai walianza kuilalamikia siku moja tu baada ya kupitishwa.

Aidha,sheria hii pia inaweka adhabu kali, ikiwemo kifungo gerezani, endapo chombo cha habari kitachapisha habari za kuikashfu serikali, uchochezi, au maudhui mengine yasiyozingatia sheria.

Machi mwaka 2018, Serikali iliweka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Mtandaoni), ambazo ziliweka muongozo juu ya gharama za kusajili leseni za maudhui ya mitandaoni.

Kupitia kanuni hizo wamiliki wa mitandao ya kijamii (blogu) na waendeshaji wa mijadala kupitia majukwaa ya mtandaoni walipaswa kulipa zaidi ya shilingi milioni moja kwa mwaka kama ada ya kujiandikisha.

Aidha, kanuni hizi zilitolewa chini ya Kifungu cha 103(1) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010.

Hali hiyo ilisababisha mazingira ya vyombo vya habari na waandishi wa habari kusambaratika ama kudorora kwa kiasi kikubwa katika miaka ya karibuni.

Ni kipindi ambacho magazeti kadhaa ikiwemo Mwanahalisi, Mawio, Tanzania Daima na Mseto (2017) yalifungiwa kwa tuhuma za kukiuka sheria za vyombo vya habari na maadili ya kitaaluma nchini.

Aidha, wengi walionekana kuelekeza vilio vyao juu ya kile ambacho walidai ni sheria kandamizi, matumizi ya adhabu kubwa na kukamatwa bila kushtakiwa ikiwa ni baadhi ya mambo yaliyowakuta waandishi wa habari katika kipindi hicho hadi mwishoni mwa mwaka 2020.

Awamu ya Sita

Baada ya kuapishwa Machi 19, 2021, Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha ghafla Machi 17, 2021 cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye alikuwa akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 61 kutokana na maradhi ya moyo, mambo mengi yalianza kubadilika.

Samia akiwa ni mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, licha ya kufanya mageuzi makubwa ikiwemo ya kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi, pia uongozi wake ulionesha mwanga mpya katika Sekta ya Habari nchini.

Tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana, Mheshimiwa Rais Samia aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wafunguliwa

Baada ya maagizo ya Rais Samia,magazeti manne ya Mwanahalisi, Mawio, Tanzania Daima na Mseto yalifunguliwa, hatua ambayo ilirejesha tabasamu kubwa katika sekta hiyo.

Uamuzi wa kuyafungulia magazeti hayo ulitangazwa Februari 10, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa leseni za magazeti hayo.

"Agizo la Rais ni sheria, natoa leseni kwa Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima, kwa sababu mambo haya ni vizuri tutoke kwenye maneno twende kwenye matendo, tufungue ukurasa mpya.

"Ili tumalize maneno, mwenye maneno yake aanze yeye, ukikutana na jiwe unarudi nyuma, unalipisha, kikubwa kazi iendelee,” Waziri Nape alibainisha.

Akizungumza baada ya kupokea leseni za magazeti yake ambayo ni Mwanahalisi na Mseto, Said Kubenea ambaye ni mmiliki wa magazeti hayo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa kufungua ukurasa mpya na vyombo hivyo vya habari huku akisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali.

Hatua nyingine

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa Habari na Changamoto za Kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais  Samia.

Upekee

Pia wadau wa habari wanasema, Serikali inapaswa kuiangalia kwa namna ya kipekee Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ili baadhi ya vipengele ambavyo vinaonekana kuwa kikwazo vifanyiwe maboresho, kwa kuwa kufanya hivyo watasaidia Sekta ya Habari kustawi kwa kasi.

Hatua ambayo itawezesha kuchangia kukuza pato la Taifa, kufungua fursa za ajira kwa makundi mbalimbali zikiwemo rasmi na zisizo rasmi nchini.

Wamesema, dhamira ya Serikali ya kutunga sheria na kanuni za kusimamia sekta ya habari ina nia njema kwa lengo la kuongeza ufanisi na ustawi bora, lakini kupitia sheria nne zinazosimamia habari zinahitaji maboresho katika baadhi ya vifungu ili kuepuka migongano ya maslahi, upendeleo, urasimu na wakati mwingine manyanyaso kwa wadau wa habari nchini.

Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016, Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 ambayo inasimamia radio, runinga na mitandao ya kijamii, Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 zikiwemo kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 zilizogawanywa katika vipengele mbalimbali.

TEF

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile anasema, licha ya dhamira njema ya Serikali kutunga sheria ambazo zinalenga kuviongoza vyombo vya habari na wadau wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kumekuwepo na changamoto au ukakasi katika baadhi ya vifungu ambavyo vikifanyiwa maboresho mambo yatakua mazuri.

"Kifungu cha 5 cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016, kipengele hiki kina vifungu viwili ambavyo vinaleta shida kidogo. Kuna kifungu cha 5( l) na kifungu cha 5 (e) kifungu cha 5(e) kinampa Mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kusajili magazeti na hapa tumeona tatizo kubwa katika kusajili magazeti.

"Tulisema mwaka 2014, 2015 na mwaka 2016 wakati sheria hii ipo kwenye mchakato wa kupitishwa kwamba kifungu hiki kina nia ovu hatukueleweka.

"Lakini tumeshuhudia jinsi magazeti ya Mawio, Mwanahalisi, Mseto na Tanzania Daima yalivyofungiwa na wakati mwingine kunyang'anywa leseni kabisa yasifanye biashara na hapa tunasema kwamba kifungu hiki kifutwe kirejeshwe kama ilivyokuwa zamani ambapo mtu akisajili gazeti linakuwa la kudumu isipokuwa asipochapisha ndani ya miaka mitatu ndipo leseni yake inakuwa inajifuta.

"Sasa kwa kufanya hivi unapofuta leseni au unasitisha unakuta unaathiri mawasiliano kati ya wasomaji na chombo cha habari kilichofungiwa, lakini sio hiyo tu kuna wafanyakazi wengi ambao wanfanya kazi kwenye magazeti kwenye radio na kwenye TV nao pia wanaathirika,"anasema Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile.

Bw. Balile anasema kuwa, leseni inapokuwa imeondolewa inaleta shida kwa sababu wale watu ambao walitegemea chombo husika kama sehemu ya ajira wanataabika.

"Wengine wanaishi maisha ya dhiki sana. Lakini kunakuwepo mikataba mbalimbali, mfano mikataba ya matangazo, mikataba ya huduma kwa jamii, gazeti linaponyang'anywa leseni au ikafutwa kwa utaratibu huu wa kusajiliwa kunakuwa kuna shida."

Kifungu cha 5 (1)

Pia, Balile anasema, katika maboresho hayo kuna umuhimu wa kipekee wa Serikali kukifuta Kifungu cha 5 (l) ambacho anasema pia kina kasoro.

"Kifungu hicho nacho kifutwe kwa maana kinaweka mamlaka au madaraka ya kukusanya, kuchakata na kusambaza kwa vyombo vya habari matangazo yote ya Serikali na taasisi zake kwa mtu mmoja ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

"Kifungu hiki, kinaleta urasimu na kinaleta hatari ya mtu mmoja kuwa na madaraka makubwa ambayo ama kitaleta urasimu ama mazingira ya rushwa, kwamba kama mtu atakuwa hafahamiani naye atakuwa hajazungumza naye vizuri atajikuta kwamba ananyimwa matangazo,"amesema Balile.

"Kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia tarehe 28 Juni,2021 kwamba vyombo vya habari vipewe matangazo kwa njia ya ushindani, tunapenda sana vyombo vya habari vipewe matangazo kwa njia ya ushindani na sio kwa njia ya upendeleo au kwa njia ambazo zinaleta mashaka, kwa hiyo tutaendelea kuzungumza.

"Na tunamshumuru waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye amesema mara zote tutaendelea kuzungumza, tutaelewana mpaka vifungu vipi vifike hatua ipi kwa ajili ya kuwa na sheria iliyo bora kabisa, sheria zilizo bora kabisa zinazo ruhusu uhuru wa vyombo vya habari, lakini zinaweka wajibu kwa watendaji na waandishi wa vyombo vya habari kwa maana kwamba kila uhuru, kila haki inakuja na wajibu wake,"amesema Balile.

Wakili

Wakili na mwanahabari, James Marenga anasema, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ikiwemo Sheria ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kuna baadhi ya vifungu au vipengele ambavyo vina changamoto ambavyo vikifanyiwa mabadiliko vitawezesha sheria hizo kuleta ufanisi na afya katika tasnia hiyo.

"Kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki za vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi na ni jambo lisilohitaji msisitizo mkubwa sana kwa sababu umuhimu wake unajulikana.

"Hivyo,kutungwa kwa sheria rafiki kwa vyombo vya habari kutawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya Serikali na umma,"amefafanua.

Amesema, miongoni mwa vifungu ambavyo vina mapungufu katika sheria hiyo ni pamoja na 4 (1), 5 (1), 6(1),7(1), 7(3), 9, 11, 22(1) na 22(2) ambavyo vinazungukwa na neno “Intentionally" (kwa kudhamiria).

"Kuna umuhimu wa kurekebisha sheria na kufuta neno "kwa kudhamiria". Haiwezekani kuthibitisha nia ya kufanya uhalifu kwa maneno ya kubahatisha,"amesema.

Marega ametolea mfano vifungu vya 4(2), 5(2), 6(2), 7(1) (g), 7(2)(b), 7(3)(b), 8(2), 9(b), 10(2), 11(2), 12(2), 13(2),14(2)(a), 14(2)(b), 15(2), 16, 17(2), 18(2), 19(2), 20(2), 21(2), 22(1), 22(2), 23(2), 24 (2)(a), 24(2)(b), 26(3), 27, 29 na 45(3) ambavyo amesema kuwa, vimebebwa na neno "Not Less Than" likimaanisha 'Si Chini Ya' ambavyo kwa tafsri ya haraka vinaonekana kuwa ni changamoto.

"Mapungufu haya ya kutumia 'not less than' yanafungua milango kwa wale ambao wanatoa maamuzi kwa mfano mahakimu au majaji wakati mwingine kuweka adhabu kubwa zaidi na asiweze kutoa adhabu ambayo inalingana na kosa lililotendwa, au adhabu zingine wanazoona, tunasema sheria inapaswa ioneshe ukomo wa adhabu, mfano maneno kama 'not more than' (si zaidi ya) yanaweza kutumika ili kutenda haki na usawa,"amesema.

Pia Wakili Marenga amesema kuwa, muda wa mwandishi kupewa taarifa anazohitaji, unapaswa kupunguzwa kama ilivyo katika nchi zingine ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Hapa Tanzania, mwandishi anapoomba taarifa, anasubiri kwa siku 30 huku Sudan Kusini akisubiria ndani ya siku saba, Rwanda ni siku tatu, Uganda siku 21 na Kenya ni siku 21,"amesema.

Balile tena

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile amesema kuwa,Juni 28, 2021 jukwaa hilo lilipata fursa ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika mkutano uliofanyikia Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema, TEF ilimweleza Mheshimiwa Rais Samia umuhimu mkubwa wa kurekebisha sheria zinazohusiana na vyombo vya habari ili kuendana na viwango vya Kimataifa.

Balile amesema, Rais aliagiza iliyokuwa Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni kukaa pamoja na wadau ili kufanya marekebisho muhimu ambayo yatawezesha sheria kutabirika na kuwa wazi.

Amesema, Mheshimiwa Rais pia alichukua hatua ya kuihamisha Idara ya Habari Maelezo kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni kwenda Wizara ya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari, kwa sasa inajulikana kama Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Balile amefafanua kuwa, TEF ilishauriana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari chini ya Mkataba wa Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) ulifanya mapitio ya sheria za vyombo vya habari ambayo yalisababisha mapendekezo ya marekebisho katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (Media Services Act), 2016,Balile amesema kuwa, katika sheria hiyo wanapendekeza maeneo zaidi ya 20 kufanyiwa maboresho.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Kifungu cha 3 sheria ambacho kinatoa ufafanuzi usiyojitosheleza kuhusu ni nani mwandishi wa habari kwa kuwatenga wanahabari raia kupitia mchakato wa kibali.

"Ukienda kifungu cha tatu, sheria inatoa tafsri juu ya mwandishi wa habari ambapo inatambua waandishi wa habari ambao wamekwenda vyuoni wakapata mafunzo, lakini haiwatambui wale ambao wanaandika katika media za jamii. Tunapendekeza, sheria itambue waandishi wa habari katika makundi mawili, mosi waandishi wa habari waliofunzwa nyumbani (kupitia ushauri) na waliofunzwa kitaaluma,"amesema.

Ametaja maeneo mengine ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho kuwa ni Kifungu cha 5 (e) kinachoangazia utoaji wa leseni za magazeti, Kifungu cha 5 (1) kuhusu Uratibu wa Matangazo kutoka Serikalini.

"Hiki kipengele 5(1) tunapendekeza kifutwe, idara zote za Serikali zinapaswa kuwa huru kutoa matangazo kwa vyombo vya habari pasipo kusubiria kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo. Serikali inazo halmashauri 185, wizara 23, mikoa 26 ya Tanzania Bara na mitano Tanzania Zanzibar na mashirika zaidi ya 300, ni jambo lisilowezekana kwa matangazo yote ya taasisi za serikali kusimamiwa na mtu mmoja,"amesema.

Wahariri

Aidha, hatua ya mhariri wa chombo cha habari kuelekezwa na serikali taarifa za kuchapisha, kama ilivyolekezwa na kifungu cha cha 7 (2) (b) cha sheria hiyo, inaingilia moja kwa moja uhuru wa mhariri katika kutoa ama kuchapisha habari.

Wakili James Marenga ameeleza kuwa, kifungu hicho cha sheria kinapoka mamlaka ya mhariri katika kuamua habari gani ya kuchapishwa.

“Kifungu cha 7 (2) (b) (iv) cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016, kinatoa maelekezo kwa vyombo vya habari binafsi kuchapisha habari zenye umuhimu kwa taifa kwa maelekezo ya Serikali.

"Kifungu hiki cha Sheria kinaingilia uhuru wa uhariri na hasa kwenye vyombo vya habari vya binafsi. Kifungu hiki kidogo hakiwezi kufanyiwa marekebisho, tunapendekeza kifutwe,”amesema.

Amesema, mapendekezo yanakusudia kuwezesha maamuzi ya kihariri kuzingatia vigezo vya taaluma bila kuathiriwa na maamrisho yasiyo ya kitaaluma. Uhuru wa uhariri (editorial independence) utalindwa.

Akifafanua zaidi amesema, kifungu cha 7 (3), (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j) vya Sheria hiyo, vinatoa udhibiti wa aina fulani ya habari ama maudhui.

“Mamlaka hii ya kisheria inatoa mwanya kwa serikali kudhibiti taarifa zinazotolewa na vyombo binafsi vya habari. Kifungu hiki na vifungu vyake vidogo vinakiuka uhuru wa wa kujieleza bila ya kuwa na sababu za msingi. Hii pia ni kwa mujibu wa maamuzi ya Mahakama ya Haki ya Afrika ya Mashariki (EACJ),"amesema.

Amesema,wanapendekeza kifungu hicho na vifungu vyake vidogo vifutwe kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).

Ukakasi

Kwa upande mwingine, waandishi wa habari nchini, wameeleza hofu yao kutokana na kifungu cha 35, 36, 50 (1)(a)(ii) kueleza kwamba, kosa la kashfa ni jinai.

Vifungu hivyo vilivyopo katika Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari 2016, vimeelekeza kosa la kashfa kuwa jinai badala ya madai.

Maregesi Paul, Mhariri wa Tanzania Daima jijini Dar es Salaam amesema, kipengele hiki kinalenga kukomoa wanahabari kwa kuwa, uzito wake ni mkubwa tofauti na kosa la kashfa.

ITAENDELEA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news