Rais wa CAF: Timu ya Afrika inaweza kutinga fainali za Kombe la Dunia 2026

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Afrika, Patrice Motsepe amesema timu mojawapo ya Afrika itafika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Bosi huyo wa CAF aliwaeleza waandishi wa habari jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumatano kwamba, anaamini hivyo, na Morocco ilishafungua milango.

"Morocco ilifungua milango kwa kutinga nusu fainali mwezi huu na nina imani taifa moja wapo la Afrika litaenda mbali zaidi kwenye Kombe lijalo la Dunia," alisema bilionea huyo wa Afrika Kusini.

"Lengo kuu la CAF (Shirikisho la Soka la Afrika) ni kwa taifa la Afrika kushinda Kombe la Dunia na lengo hilo linaweza kufikiwa."

Aidha, Patrice Motsepe ambaye ni raia wa Afrika Kusini aliyechukua nafasi ya Ahmad Ahmad anaamini mafanikio ambayo Morocco imeyapata kwenye fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022 ni dalili kuwa kuna mambo mazuri yanakuja mbeleni.

Kwenye fainali za Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 nchini Qatar, Morocco walivunja rekodi ya Ghana waliofika robo fainali kwa wao kufika nusu fainali ya mashindano hayo.

Bosi huyo wa CAF anasema, timu ya Morocco kufanya vizuri kwao kutazipa ari timu nyingine barani humo kuamini zinaweza kusonga mbele.

“Ninaamini moja ya timu ya Afrika itafika kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026”, alisema Motsepe Rais mwenye miaka 60.

“Mafanikio ya Morocco yametufanya Waafrika wote tujione wa kipekee na wenye uwezo. Mwanga wa soka la Afrika una nuru mbele yetu.”

Motsepe anasema inashangaza kuona taifa kama Croatia lenye watu milioni 3 hadi 4 linakuwa na uwezo wa kupambana na timu ya Brazil na kuitoa wakati Afrika ina watu wengi zaidi, akisema hatamani kuona hilo likitokea.

Pia amehimiza uboreshwaji wa miundombinu ya viwanja na maandalizi mengine ya kisasa akisema mafanikio ya Morocco siyo bahati mbaya ni matokeo ya uwekezaji.

Simba wa Atlas iliishangaza Ubelgiji katika hatua ya makundi, kisha kuzitoa timu mbili zenye nguvu zaidi za Ulaya, Hispania na Ureno, katika hatua ya mtoano kabla ya kufungwa na Ufaransa katika nusu fainali.

"Kuna angalau mataifa 10 ya Afrika ambayo yanaweza kushindana katika kiwango cha juu na kushinda Kombe la Dunia,"aliongeza Motsepe.

Pia alizipongeza Cameroon na Tunisia kwa ushindi wa makundi dhidi ya washindi mara tano wa Kombe la Dunia Brazil na mabingwa mara mbili wa Ufaransa.

"Tunapaswa kujivunia kile ambacho Cameroon na Tunisia zilifanikisha. Hizi na nchi nyingine za Afrika lazima zijifunze kutoka kwa Morocco,"alisema rais huyo wa CAF.

Ushindi huo wa kushtukiza haukutosha kuzifanya Cameroon na Tunisia kupita raundi ya kwanza, lakini Senegal ilitinga hatua ya 16 bora kabla ya kuondolewa baada ya kushindwa vibaya na England.

Mabingwa watetezi wa Afrika, Senegal walipata pigo kubwa kabla ya mchuano huo wakati mshambuliaji nyota Sadio Mane alipoondolewa kutokana na jeraha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news