NA DIRAMAKINI
BAADA ya siku chache zilizopita Nabii Mkuu GeorDavie ambaye ni mwanzilishi na Kiongozi Mkuu wa Kanisa la GeorDavie Ministries International-Ngurumo ya Upako jijini Arusha kutuhumiwa kuvunja ndoa ya Bi.Elizabeth Benjamin mkazi wa jiji hilo ambaye aliamua kujichora tatoo ya mtumishi huyo begani mwake, hatimaye Bi.Elizabeth Benjamin amefunguka na kusema huo ni uzushi ambao hauna nafasi katika msimamo wake wa imani.
Mwanamke huyo aliachana na mumewe huyo ambaye yeye anadai kuwa, hakuwa wamefunga naye ndoa baada ya kumshinikiza aifute tatoo hiyo ya jina la GeorDavie.
"Nimekuja kueleza yanayotangazwa mitandaoni. Wanamchafua baba (Nabii Mkuu GeorDavie). Mimi nilikuwa shabiki wa GeorDavie, nilikuwa namsikikiza redioni na mtandaoni nikavutiwa na mahubiri yake.
"Sisali kwake, hanifahamu mimi nilikuwa nasikiliza redio, ninaangalia picha zake mitandaoni nikavutiwa na mahubiri yake nikaamua kutengeneza picha nikaweka ndani kwangu. Ikaenda ikafika kipindi kile 'Cha teleza' nikatengeneza bango langu limeandikwa nyumba yangu ina ulinzi wa Nabii Mkuu GeorDavie."
Teleza
Siku za karibuni jijini Arusha alizuka mtu mmoja mkazi wa Sojema, Kata ya Murieti jijini humo ambaye alizua hofu kubwa kwa wanawake baada ya kujihusisha na vitendo vya kuvamia nyumba zao usiku na kuwaingilia kimiujiza.
Aidha, juhudi za Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi mbalimbali zilifanikisha kumdhibiti katika moja ya nyumba za wakazi wa jiji hilo, hivyo kudaiwa kuuawa.
"Huyu ndiye nabii ninayemuamini nchini Tanzania niliweka pale Ngurumo ya Upako. Niliweka kama ulinzi wangu tu akija mtu mbaya (kama teleza) akifika pale akute kama ulinzi. Kwa sababu Nabii Mkuu GeorDavie anahubiri kupitia Mungu, hivyo nilimtanguliza Mungu kwanza.
"Nabii Mkuu ni Nabii ninayemuamini, na pia ninavutiwa naye sana sijaanza kusali pale nilifika pale tarehe 20 Jumapili iliyopita,"anafafanua Bi Elizabeth.
Aingia Ngurumo ya Upako
Bi. Elizabeth ambaye anaonesha kuwa na upendo wa kipee kutokana na huduma ya kiroho inayotolewa na Huduma ya Ngurumo ya Upako kwa Nabii Dkt.GeorDavie, Novemba 20, 2022 alifika kwa mara ya kwanza kanisani hapo na kusema kuwa,
"Ninafuraha sana kukuona Baba yangu, nakupenda sana, hata nyumbani kwangu kumeenea picha zako, mabango nikaona haitoshi nikaamua kukuchora. Nakupenda japo napitia mengi sana, mume wangu kaniacha akasema unamchoraje Nabii huyo mtu mwingine na mimi nipo ndani. Hata nikisikikiza redio unapokuwa unazungumza kuna kuwa na ugomvi,"alisema Bi.Elizabeth ambaye aliwahi kufanya biashara ya viatu baadaye mgahawa.
GeorDavie
Katika ibada hiyo, Nabii Dkt.GeorDavie ambaye ni mwanamuziki, mwandishi na mfadhili anayesaidia watu mbalimbali na wandishi wa kitabu cha “Keeping Up With God’s Kingdom Government Startdards” alionekana kuguswa na namna ambavyo Bi.Elizabeth ameonesha upendo mkuu kwake.
"Kabla sijaondoka kwenda Burundi nililetewa picha picha ya mama mmoja ambaye amejichora mgongoni aliyejichora jina la kuonesha mahaba mengi mengi sana.
"Nimefurahi sana na kufarijika, mimi nitakusapoti shilingi milioni tano, kitendo ulichokifanya ni kitendo cha kishujaa sana na upendo siku zote unachopanda ndicho utakachovuna.
"Lengo la kukupa sapoti hii ni kukusaidia kusudi uweze kuimarisha biashara zako na pia ukiishiwa usisite kuwasiliana na balozi wangu, umefanya jambo jema sana, hiyo ni heshima kubwa.
"Namuombea mume wako, atambue kuwa jambo alilofanya mwanamke huyu ni jambo la ushujaa. Jambo la kumuinua Mungu. Kuna watu wanaitwa mastaa, wapo wasanii, wanamuziki huwezi sema kwa nini unamchora mfano Beyonce, au mtu mwingine maarufu ukianza kuleta mambo ya uswahili unamchora kwa nini tambua au jua huyo ni staa.
"Tambua Mungu aliwainuaga mastaa usilete taswira ya kitu kingine ambalo sio jambo hilo, nawashauri wanaume tuache wivu.Huyu mama alikuwa hanijui, hajawahi kuja kwenye hii hudumal,sisi tutazidi kutenda mema kwa watu wote,"amesema Nabii Dkt.GeorDavie ambaye pia ni mume wa Anna Davie.
GeorDavie alimuoa Anna Davie mwaka 1988 ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa kanisa lake GeorDavie Ministries International au Ngurumo ya Upako na wakapata watoto akiwemo Nic Davie, Ken Davie na Monica Davie.
Waumini wanasemaje?
Kwa nyakati tofauti, ndani ya makao makuu ya Kanisa la GeorDavie Ministries International au Ngurumo ya Upako jijini Arusha,walitoa maoni mseto kuhudu imani ya Elizabeth Benjamin ya kuchora tatoo ya kiongozi wao mkuu katika mwili wake.
"Huyu mama amefanya jambo jema na la kishujaa sana katika kumtumuza Mungu.Watu wengi wanachora tatoo hata za wachumba zao kwa baadaye wanawaacha, lakini huyu mama kachora tatoo ya mtumishi wa Mungu na Mungu hawezi kukuacha.
"Mwanamke huyu ni kama mwanamke ambaye alimuosha Yesu kwa machozi yake, wapo watu kule nje wanajitoa ufahamu hawatambui wala kuthamini thamani yako Nabii Mkuu ila wako watu wanaumia kwa yale maneno ya watu wanaojitoa ufahamu.
"Mama huyu akaamua kuweka ushahidi kwamba pamoja na kwamba simjui Nabii Mkuu taarifa zake zinatosha kuweka alama maishani mwake.
"Mathalani mimi nimechora tatoo ya nanga, mama amechora tatoo ya Nabii Mkuu ambayo ina faida. Amechora tatoo ya mtu ambaye anamtumikia Mungu. Umechora tatoo ya mtu ambaye jicho la Mungu lipo ndani yake na macho ya Mungu nina hakika yatakuwa yakimuangalia mama huyu.
"Huyu mama ame-take risk ya kuchora tatoo ya Nabii Mkuu kwenye mwili wake, bila kujalisha ndoa yake inaweza kuvunjika. Watoto wake watasema nini na pia jamii itasema nini, ame-take risk kubwa sana ambayo hata wewe Nabii Mkuu ulichompa kinastahili na pia umesema utaweza kumsaidia hata akiyumba kiuchumi tena,"baadhi ya waumini walitoa maoni mseto kwa nyakati tofauti katika huduma hiyo ibadani Novemba 20, 2022.
Imani ya Elizabeth
Wakati huo huo, mama huyo anaendelea kufafanua kuwa, "Kila mtu kuna kitu anachovutiwa nacho kwenye moyo wake, manabii wapo wengi wachungaji na mimi GeorDavie ndiye nabii ambaye nimevutiwa naye sana na ndio maana nimeamua kuchora tatoo yake.
"Kilichonifanya nichore tatoo yake ni imani yangu kwake, kwa hiyo niliona hii tatoo ni kama ulinzi wangu. Mjue kila mtu ana imani yake, watu wengine wameweka chale wanakwenda kwa waganga. Unakuta ni Mkristo, lakini ana chale nyingi tu mwilini mwake. Hii yangu iko begani.
Mapokeo
"Kuhusu mapokeo ya familia, mapokeo mabaya ni kwa mtu niliyekuwa naye karibu ni kama rafiki yangu nipo naye muda mrefu sio mume wangu, amekuwa ananilipia kodi. Ananitunza, sema hatujafunga ndoa, lakini wanasema mtu ukikaa naye miezi sita ni mume wako.
"Yeye hapendi mimi niwe na hii tatoo, ugomvi wake mkubwa na mimi anataka nifute na mimi siwezi, kumbuka nimechora kwa maumivu, nimetumia pesa. Mabango pale ndani hataki, mimi ninamwambia Nabii Mkuu namkubali siwezi kufuta.Nipo tayari lolote na kwa chochote na ndio maana tukaamua kila mtu na hamsini zake, akaachana na mimi."
Maneno
"Kuhusu picha na maneno ya watu mitandaoni huo ni uongo, wanamchafua baba na hawataweza kwa jina la Yesu, Nabii Mkuu watu wanamuelewa, wanampenda ni Nabii wa viwango vingine.
"Mpaka nimeamua kuchora tatoo yake maana yake nampenda na kumuamini, hakuna mtu yeyote aliyewahi kumchora Nabii au mchungaji wake mimi ndiye wa kwanza.
"Wanamchafua baba, sio kweli yule mtu ambaye ni mimi,mimi ni Elizabeth yule ni Pamela ni vitu viwili tofauti. wameunganisha unganisha kumchafua Baba hamna kingine, mimi nitasema ukweli popote, wamenitukana sana mimi mitandaoni, lakini mimi sio mtu wa mitandao.
"Kuna mengi yameongelewa, lakini sio kweli wanamchafua Baba japo baba ni mtu mwenye upendo, mwenye huruma sitokubali Nabii Mkuu achafuliwe au atukanwe nitakwenda popote kusema ukweli. Mungu aliye hai ndiye anajua Nabii Mkuu ni nani.
"Kuhusu wanayosema watu juu yangu mimi hayaniumizi, imani yangu ni imara sana na pia wanayosema sio kweli ingekuwa kweli ningeumia. GeorDavie mara ya kwanza kuniona ni tarehe 20 hanijui kabisa, wanamchafua Baba kwa sasa yule ni viwango vingine kabisa, wanaojaribu kumchafua ni watu hao ambao wengine ni wachungaji au wenye makanisa yao yule ni viwango vingine na anakubalika sana.Baba anasaidia watu wengi sana, ukienda pale kwake anakusaidia.
"Wazo la kuchora tatoo lilinijia usiku nikaamka asubuhi nikaenda kuchora hata ambaye alikuwa ananichora aliniuliza mara mbili mbili ni nani yako. Nikasema simjui wala hanijui, nikasema nasikiliza tu mahubiri yake kwenye radio kwenye simu yamenijenga kiimani ndio maana nimeamua kuchora."
Msimamo
"Na hata ninapozungumza hapa nataka kuwa muumini rasmi na nitabatizwa kwa hiyo mimi ni Mtoto wa GeorDavie, Nabii Mkuu hata wanapozungumza sijui Baba...mapenzi hata siku moja haijawahi tokea hata yeye Baba anaumia sana hicho kitu kwa sababu moyo wake unajua kuonana naye ilikuwa tarehe 20.
Kuhusu tatoo aliyoichora na mitazamo ya kiimani kwamba kuchora tatoo ni dhambi, Elizabeth amesema kuwa, "Nimechora hii tatoo sijaokaka, na pia kila mtu ana maamuzi yake juu ya mwili wake na pia anayehukumu na kutoa hukumu ya kweli ni Mungu wala sio mwanadamu.
"Mungu anajua nimechora hii tatoo kwa nia gani, wanasema nimechora tatoo mwili wote sio kweli hii ndio tatoo ya kwanza kuchora ya Nabii Geor Davie iwe dhambi isiwe dhambi mimi sijaandika jina la msanii au mambo ya kihuni nimeandika tatoo ya GeorDavie ambaye ni mtumishi wa Mungu.
Rai yake
"Niwaambie ndugu zangu Watanzania msisikilize maneno wanayozusha mitandaoni Geo Davi ni Nabii Mkuu ana huruma sana, ana upando na watu wote sio tu wanaosali kanisani kwake bali watu wote. Sitokubali kuona Nabii Mkuu anachafuliwa nipo tayari kwa lolote na kwa chochote nabii anachafuliwa,"amesema Bi.Elizabeth.
Kuhusu huduma
GeoDavie, safari yake ya utumishi ilianza mwaka 1980. Baada ya kumaliza masomo yake alitumika kama mtume Tanzania, Kenya na Uganda. Mwaka 1991 alianza kufanyia kazi maono ya huduma yake ya Global Concert Church/GeorDavie Ministries International-Ngurumo ya Upako.
Aidha, alisajili huduma hiyo mwaka 1994. Mwanzoni huduma ilianza kama huduma ya kuunganisha waimbaji wa muziki wa injili wa Afrika Mashariki, kuhubiri na kufundisha neno la Mungu makanisani na kusaidia watoto wa mtaani.
Mwaka 1995 alipata maono ya kuanzisha redio na mwaka 1997 alipata kisambazaji cha redio kidogo cha wati 100. Kisambazaji hicho cha redio kilimuwezesha kufikia watu waliokuwa karibu na eneo alilokuwa akirusha vipindi vyake.
Mwaka 2012 alisajili rasmi redio yake ya Ngurumo Ya Upako FM. Mwaka 2018 alianzisha televisheni yake ya GeorDavie TV.
Novemba 14, mwaka 1999 ndio ilikuwa mwanzo rasmi wa kanisa la GeorDavie Ministries-Ngurumo Ya Upako ambalo kwa wakati huo lilijulikana kama kanisa la Destiny.
Kanisa hili lilianzia sebuleni mwake. GeorDavie aliwahi kusema kwamba sababu ya kuita kanisa lake Destiny (Uelekeo) ni kwa sababu kwa wakati huo alikuwa hajaamua ataita nini kanisa lake, lakini aliliita Destiny (Kanisa la Uelekeo) akijua na kumaanisha moyoni mwake kwamba kuna mahali anaenda.
Atakapokaribia anapokwenda atajua jina rasmi la kuita kanisa lake. Mwaka 2003 alibadilisha jina la kanisa kutoka Kanisa la Uelekeo (Destiny Church) na kuliita Ngurumo ya Upako.
Kati ya mwaka 2005 hadi 2011 Mungu alimuongoza GeorDavie kufanya mikutano mikubwa na ya kihistoria ya kinabii ndani na nje ya nchi.
Ikiwa ni pamoja na kufungua matawi ya kanisa Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Morogoro, Manyara, Kilimanjaro, Congo na Marekani.
Arusha ikiwa ndio makao makuu ya kanisa Duniani na Ikulu ya Nabii Mkuu. Lengo la mikutano hiyo ilikuwa ni kutambulisha huduma ya kinabii Tanzania kwa sababu ilikuwa ni huduma isiyojulikana. Kwa sasa kanisa lake huhudhuriwa na maelfu ya watu kila wiki na kupata wageni kutoka mikoa mbali mbali Tanzania na duniani kote.
Kumbuka, DIRAMAKINI inajihusisha na machapisho yote ya habari kama yalivyojiri na kusemwa na muhusika au wahusika, tovuti hii inawajibika kuchuja tu, pale ambapo lugha mbaya imetumika au maneno makali, hivyo tunakuletea kile kilichosemwa na kilivyojiri saa 24 kwa wakati husika na hatuwajibiki kwa namna yoyote kuhusu yaliyosemwa iwapo hayajavunja kanuni za maudhui.
Soma Levictus 19:28
ReplyDelete