NA DIRAMAKINI
SERIKALi imewahimiza waumini wote na wasiokuwa na dini nchini kuzidi kushiriki kikamilifu katika kufanya kazi za uzalishaji kwa bidii ili kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia na taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini ameyasema hayo Deesemba 17, 2022 wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa katika Kanisa la Waadventista Wasabato lililopo Mtaa wa Mwembe Chai Kata ya Ndugumbi Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Sagini amesema, ni jukumu la waumini wa dini zote za Kikristo,Kislamu na hata wasio kuwa na dini kuwajibika kikamikifu kufanya kazi kwa maarifa, bidii, malengo na tija ili kujiletea maendeleo yao na kuzidi kuwezesha taifa kupiga hatua za kimaendeleo.
Pia Mheshimiwa Sagini amewasihi viongozi wa madhehebu yote ya dini nchini, kuwasisitiza waumini wa dini zao na jamii kwa ujumla kujiepusha na michezo ya kubaatisha wakiamini kwamba watakuwa matajiri kupitia njia hiyo.
Amesisitiza kutojihusisha pia na kushabikia mapenzi ya jinsia moja pamoja na vitendo viovu katika jamii ikiwemo kuwanajisi watoto wadogo, vitendo vya ubakaji, utumiaji dawa za kulevya pamoja na matukio ya kikatili ambayo ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu na pia ni makosa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mheshimiwa Sagini amesisitiza Watanzania wote kuendelea kuishi kwa amani, kupendana, kujaliana na kuthaminiana sambamba na kushirikiana na serikali katika ajenda ya maendeleo na kuwaombea viongozi wazidi kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi wa kuwatumikia wananchi katika maeneo yao kwa ufanisi.