NA OR-TAMISEMI
MKUU wa Programu na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya nchini, Dkt.Catherine Joachim amewasihi waganga wafawidhi wa vituo vya afya na hospitali za halmashauri kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha wanayafikia malengo yao.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa ufungaji wa kikao kazi cha waganga wafawidhi wa vituo vya afya na hospitali za halmashauri, lengo likiwa ni kutaka kukumbushana kuweka nguvu kazi katika suala la utoaji wa huduma bora.
Dkt.Joachim amesema, Serikali kwa kiwango kikubwa imewekeza katika vituo vya afya, wamejenga vituo vingi pia wameendelea kuajiri japo kwa uhaba, lakini pamoja na kufanya yote hayo bado wananchi wana kilio kikubwa kwa jinsi ambavyo watoa huduma wanatoa huduma zao.
Amesema, Serikali imefanya jitihada kuhakikisha huduma zinaanzishwa,imeweka huduma za mama na mtoto katika vituo vyote vya afya, huduma za meno, macho, upasuaji na zingine nyingi ili tu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ila kwenye suala la hutoaji huduma bora bado ni changamoto kubwa.
"Tukumbushane kama tulizingatia zaidi katika masuala ya ujenzi, kununua vifaa, kufanya DHFF, tulizingatia katika masuala ya mifumo yaani tumefanya vitu vingi, lakini tumesahau nguvu kazi katika kutoa huduma bora,"amesema.
Aidha, mtoa neno la shukrani ambaye ni Mwenyekiti wa Waganga Wafawidhi Tanzania Bara, Dkt.Florence Hilari amesema, wanakubaliana na Dkt.Joachim kwamba pamoja na jitihada nyingi za Serikali katika sekta ya afya bado kuna malalamiko katika utoaji huduma bora, hivyo ameahidi kwa niaba ya waganga wafawidhi wenzake watakwenda kuhakikisha malalamiko yanapungua.
"Sisi kama wasimamizi wa kuhakikisha malalamiko haya yanapungua kwa kiasi kikubwa tutakwenda kuhakikisha yote yanaboreka kwa kubeba dhana ya kuboresha huduma zetu za afya na kusimamia kuona kweli ubora unaonekana na hatimae malalamiko kwa wateja wetu ambao ndio watanzania wengi kwa asilimia 85 ambao wanaopata huduma katika vituo vyetu wanapata huduma bora.
"Lakini pia tutakwenda katika vikao vyetu vya HMT kuwaambia kwa umakini timu zetu za maboresho, kwa sababu ninaamini timu ndio kiungo cha kuleta ubora wa huduma,"amesema Dkt.Hilari.