Shoti ya umeme yaua wanandoa nchini Guyana

NA DIRAMAKINI

MAKACHERO wa Jeshi la Polisi nchini Guyana wanachunguza vifo vya wanandoa ambavyo vinahusishwa na shoti ya umeme.

Sorajanie Hansraj na Prahalad Jagnarine. (Picha na Stabroek).

Sorajanie Hansraj mwenye umri wa miaka 32 na mumewe Prahalad Jagnarine mwenye umri wa miaka 39 vifo vyao vilitokea kati ya saa 7 jioni na saa 6 asubuhi ya Desemba 5, 2022 katika eneo la Success Squatting, East Coast Demerara.

Kwa mujibu wa Gazeti la Guyana,polisi wanasema miili hiyo ilifanyiwa uchunguzi wa awali na alama za kuungua zilionekana kwenye shingo, kifua na kiganja cha mkono wa kulia cha Jagnarine na alama za kuungua kwenye kifundo cha mkono wa kushoto na upande wa kushoto wa mgongo wa Hansraj.

Aidha, upekuzi zaidi ulifanyika ambapo waya nyekundu na nyeusi zilionekana karibu na miili hiyo. Waya hizo inadaiwa ziliunganishwa kwenye nguzo ya umeme inayoelekea nyumbani kwao.

Shirika la Umeme nchini Guyana (Guyana Power and Light-GPL) na madaktari wa dharura waliitwa kwenye eneo la tukio. GPL ilikata waya kwenye nguzo, na wanandoa hao wakatangazwa na Dkt.Dourga kuwa wamekufa, hivyo kupelekwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Demerara.

Awali mwanaume wa miaka 29 wa Kijiji cha Good Hope alikufa baada ya kupigwa shoti na umeme alipokuwa akiweka mti wa Krismasi wa futi 27 huko Lusignan.

Marehemu alitambuliwa kwa jina la Deepak Ramdeen, ambaye ni mbobezi katika masuala hayo ya mapambo huko Good Hope Mashariki ya Pwani ya Demerara.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi nchini Guyana, inadaiwa Ramdeen alinaswa na umeme usiku wa kuamkia Desemba 2, 2022 akiwa na vijana wengine watatu wakiweka mti wa Krismasi wa chuma wenye urefu wa takribani futi 27 mbele ya makazi ya mwananchi wa huko Lusignan.

Loop ilieleza kuwa, inadaiwa mtaalamu huyo aliyekuwa akiweka mti huo alikutana na waya wa juu ambao ulisababisha kupigwa kwa shoti ya umeme.

Ripoti ya Jeshi la Polisi inasema, Ramdeen na wengine wote walikuwa wakiweka mti wa Krismasi wa chuma kwa kutumia crane iliyounganishwa kwenye gari, ingawa bado uchunguzi unaendelea ili kufahamu chanzo zaidi za tukio hilo.

Guyana ni nchi iliyopo kwenye Pwani ya Atlantiki ya Kaskazini ya Amerika Kusini ambapo mji mkuu wake ni Georgetown, unajulikana kwa usanifu wa majengo ya kikoloni ya Uingereza, ikijumuisha Kanisa Kuu la Kianglikana refu la St.George's Anglican Cathedral.

Utafiti wa hivi karibuni wa National Library of Medicine ambao uliangazia kuhusu ajali zinazotokana na matukio ya umeme ulibainisha kuwa, vyanzo vikubwa ambavyo vimekuwa vikisababisha majanga hayo ni kuwatumia mafundi ambao hawana ujuzi kwa ajili ya kusuka mifumo ya umeme katika nyumba na ambao hawajaidhinishwa.

Sambamba na kujiunganishia umeme kiholela, ujenzi wa makazi katika maeneo ambayo si salama na kulikuwa na mwingiliano wa miti,  hali ambayo imekuwa ikisababisha majanga pindi inapoangushwa na mvua au kukatwa vibaya bila taarifa kwa mamlaka husika.

Aidha, uchunguzi huo wa visababishi vya ajali za umeme za mara kwa mara zinazotokea ulionesha wazi kuwa ipo haja ya kutilia mkazo uendelezaji wa utamaduni wa usalama katika maeneo mbalimbali ya kijamii, hasa miongoni mwa wafanyakazi wanaojishughulisha na kazi zinazohusiana na umeme, ujenzi na elimu kwa watoto wa shule ili kupunguza kasi ya ajali.

Pia walipendekeza kuwa, kuna umuhimu wa kutambua maeneo hatarishi kama jukumu la wafanyakazi wote, hasa mamlaka zinazohusika ili kuwapa elimu wananchi.

Sambamba na kuwajibika mara moja kwa mamlaka husika pale ambapo inapewa taarifa kuhusiana na hitilafu yoyote ambayo inahusiana na kesi za dharura ambapo marekebisho yanahitajika.

Vilevile kuongeza ufahamu kwa umma kuhusu hatari zinazohusiana na nyaya za umeme na mitandao ya umeme kwa kutoa vipeperushi vya elimu na ujumbe wa usalama kupitia matangazo ya moja kwa moja mitaani, vyombo vya habari ikiwemo redio na mitandao ya kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news