NA DIRAMAKINI
NAHODHA John Bocco na kiungo Said Ntibazonkiza wa Simba SC wamefunga magoli matatu (hat trick) kila mmoja katika ushindi mnono wa mabao 7-1 waliopata dhidi ya Tanzania Prisons.
Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao umepigwa Desemba 30, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Bocco alitupatia bao la kwanza dakika ya 14 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Said Ntibazonkiza.
Mlinzi wa kati Henock Inonga alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 24 baada ya kuumizwa na Samson Mbangula ambaye alioneshwa kadi nyekundu.
Aidha, Prisons ilisawazisha bao hilo dakika ya 30 kupitia kwa Jeremiah Juma kufuatia mpira wa krosi uliopigwa na Salum Kimenya kuokolewa na Aishi Manula kabla ya kumkuta mfungaji.
Dakika ya 47 Bocco alitupatia bao la pili baada ya kupokea mpira wa krosi uliopigwa na Pape Sakho ambaye alimzidi ujanja mlinzi wa Prisons kabla ya kutoa pasi.
Saido Ntibazonkiza alitupatia bao la tatu dakika ya 60 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Clatous Chama na kupiga shuti kali la chini chini akiwa ndani ya 18.
Bocco alikamilisha hat trick kwa kufunga bao la nne 63 kwa kichwa kufuatia mpira wa krosi uliopigwa na Clatous Chama kuokolewa na mlinda mlango Hussein Abel kabla ya kumkuta.
Dakika moja baadaye, Ntibazonkiza alitupatia bao la tano baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo mkabaji Mzamiru Yassin.
Ntibazonkiza naye alikamilisha hat trick yake dakika ya 70 baada ya kufunga bao la sita akipokea pasi kutoka kwa Chama.
Wakati huo huo, mlinzi Shomari Kapombe alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga la saba dakika ya 88 kwa kichwa kufuatia mpira wa krosi uliopigwa na Gadiel Michael.
Kocha Juma Mgunda aliwatoa Henock, Bocco, Sakho, Mohamed Hussein na Sadio Kanoute na kuwaingiza Kennedy Juma, Augustine Okrah, Habib Kyombo, Victor Akpan na Gadiel.
Kwa matokeo hayo Simba SC inafikisha alama 44 baada ya mechi 19 hivyo kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na Yanga SC kwa alama 47 baada ya mechi 18.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Azam FC ambayo tayari imecheza mechi 18 ikiwa na alama 37 huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Singida Big Stars FC ikiwa na alama 37 baada ya mechi 19 huku Namungo FC ikishika nafasi ya tano kwa alama 25 baada ya mechi 18.