Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa kikanda

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inatarajia kuwa kitovu cha usafiri wa kikanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC) nchini Masanja Kadogosa na Mwakilishi wa Kampuni za ubia za CCECC na CRCC wakibadilishana Hati mara baada ya kutia saini Mkataba wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora kwenda Kigoma (km 506) iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Desemba 20, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla fupi baada ya tukio la utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora kwenda Kigoma (kilomita 506-SGR LOT 6).

Mkataba wa kutekeleza mradi wa kilomita 506 umetiwa saini na pande tatu ambazo ni Shirika la Reli Tanzania (TRC), China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na Kampuni ya Ujenzi ya Reli ya China (CRCC).

Rais amesema kutimia kwa ndoto ya kuwa kitovu cha usafiri katika kanda kutawezekana tu ikiwa watendaji wataweza kusimamia miradi ya kimkakati kwa bidii.

Pia amesema, mradi huo hadi sasa umetoa ajira kwa wafanyakazi zaidi ya 20,000 ambao wamelipwa zaidi ya shilingi bilioni 237.7 huku wazawa wakineemeka zaidi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema, utiaji saini wa ujenzi awamu ya pili wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha kutoka Tabora kwenda mkoani Kigoma utakapokamilika utatimiza ujenzi wa reli ya Kati na kitakachofuata ni ujenzi wa matawi.

Kadogosa amesema ujenzi mwingine utakaofuata ni kujenga matawi ikiwemo Kakiuwa kwenda Mpanda, Uvinza-Msongati na Kisaka kwenda Kigali nchini Rwanda.

“Utiaji saini huu unakamilisha manunuzi ya kilomita 2,102 njia kuu ikiwa ni kilomita, 1,633 na njia za kupishania kilomita 469, kilomita hizi zinafanya Tanzania kuwa nchi yenye ujenzi wa njia ndefu ya SGR barani Afrika,”amesema Kadogosa.

Kadogosa amesema, ununuzi wa tawi la Uvinza hadi Kitega nchini Burundi unaendelea ambapo utakapokamilika utaunganisha na watu wa machimbo ya nikeli.

“Reli hii itakapokamilika itatuunganisha bandari ya Dar es Salaam, Kongo kupitia bandari ya Kigoma na kuweza kufikia Uvira, Bukavu, Goma Kalemie na Lubumbashi na kwa ujenzi huu tutakuwa tumefikia miji mikubwa mitatu ndani ya Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).

“Hii itakuwa fursa kubwa kwa wafnyabiashara ambapo kipande hicho kina kilomita 516, njia kuu ikiwa ni kilomita 416 na njia za kupishania kilomita 15,”amesema Kadogosa.

Pia amesema, ujenzi huo unaotarajiwa kuchukua miaka minne hadi kukamilika na utagharimu shilingi trilioni 6.34 huku Tanzania ikiwa imewekeza shilingi trilioni 23.3 ikijumuisha kipande cha Dar es Salaam hadi Mwanza na kipande cha Tabora hadi Kigoma.

Wakati huo huo, Kadogosa amesema, jumla ya mabehewa 1,430 ya mizigo kutoka China yanatarajiwa nchini Tanzania kuanzia Septemba, mwakani.Aliongeza kuwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya matengenezo vitapokelewa ifikapo Desemba, mwakani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news