NA LWAGA MWAMBANDE
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Benjamin William Mkapa aliwaongoza Watanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia Novemba 23, 1995 hadi Desemba 21, 2005 alipohitimisha muhula wake wa pili.
Hayati Benjamin William Mkapa.
Mkapa alifariki dunia katika usiku wa kuamkia Julai 24, 2020 akiwa jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu na kuzikwa Julai 29, 2020 huko Lupaso katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Wakati wa uongozi wake, anatajwa kuwa ni kiongozi aliyesimama imara kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma huku akikazia utawala bora.
Pia alitekeleza sera ya ubinafshaji wa Mashirika ya Umma nchini Tanzania ili kuongeza tija na uzalishaji na alihimiza uchumi wa soko huria na kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania kuwekeza zaidi ili kukuza uchumi wa Tanzania.
Sera na Mikakati ya Uchumi na Maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Tatu iliungwa mkono na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hali iliyopelekea Tanzania kufutiwa madeni yake ya nje.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, wakati tunasherehekea miaka 61 ya Uhuru leo Desemba 9, 2022, hayati Mkapa ni miongoni mwa viongozi wa Tanzania walioacha alama njema, endelea;

1:Ni Uwazi na Ukweli, Rais wetu wa tatu,
Maneno yake halali, alotuambia watu,
Na aliyaishi kweli, huyo kiongozi wetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
2:Rais Ben Mkapa, wa kwanza chaguzi zetu,
Vyama vingi kuja hapa, kwa hii miaka yetu,
Kazi kweli alichapa, alama zake ni zetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
3:Kurekebisha uchumi, hata mashirika yetu,
Alikufanya kisomi, kwa ustawi wa kwetu,
Na mengine hatusemi, yalikuwa kwazo kwetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
4:Lililoumiza wengi, haya mashirika yetu,
Kuyauza mengi mengi, hata ya faida kwetu,
Tena jambo la msingi, naye hakukana katu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
5:Yale mambo ya umeme, mikataba ile butu,
Kipindi kile tusome, ibaki elimu kwetu,
Vinginevyo tumseme, alifanya mengi kwetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
6:Mtandao barabara, zosambaa hapa kwetu,
Zilizokuwa za kera, hata kwao watu wetu,
Yeye aliona bora, kuwekeza fedha zetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
7:Mkapa pia sifika, kukusanya kodi zetu,
Vile aliwajibika, lileta heshima kwetu,
Ni pazuri tulifika, yale makusanyo yetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
8:Hata kwenye kanda yetu, alifanya mengi yetu,
Akiwa Rais wetu, hata mstaafu wetu,
Kusuluhisha wenzetu, Amani yao ni yetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
9:Kuna vitu vyatajika, alivyovileta kwetu,
Viwili vinahusika, ni kama mfano kwetu,
Daraja linahusika, kusini kwa ndugu zetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
10:Na uwanja wa kisasa, pale Dar jiji letu,
Hata samba la kisasa, sasa lapigika kwetu,
Umeleta hadhi hasa, timu na taifa letu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
11:Amekwishatangulia, kwa Mungu nyumbani kwetu,
Mema yake yasalia, hayo ni urithi wetu,
Jina tutajitajia, mekuwa fahari yetu,
Twashereheka Uhuru, na maendeleo yetu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602