TWASHEREHEKEA UHURU-5:Huyu Rais wa Tano, Niseme mambo matano

NA LWAGA MWAMBANDE

DOKTA John Pombe Joseph Magufuli alikuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi mwanzoni mwa mwaka 2021.

Alichaguliwa Oktoba 2015 na kurithi mikoba ya Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete. Alikuwa mwanasiasa mwenye sifa ya uchapakazi na asiye na mazaha, alishinda uchaguzi wa mwaka 2015 na ule wa mwaka 2020.

Magufuli alifariki Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salam wakati akiendelea na matibabu kutokana na matatizo ya moyo na kuzikwa Machi 26, 2021 huko nyumbani kwake Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, kwa kipindi kifupi kuna mambo mengi pia Magufuli aliyafanya ambayo yaliweka alama na leo Desemba 9, 2022 tunaposherehekea miaka 61 ya Uhuru anakumbukwa, endelea;


1:Huyu Rais wa tano, niseme mambo matano,
Yale alimwaga wino, kwetu yabaki mavuno,
Kwa muda mfupi mno, alitenda mengi mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

2:Huyu John Magufuli, muumini Muungano,
Likuwa mkali kweli, wa mwendo wa konokono,
Liwatumbulia mbali, kweli watu wengi mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

3:Liingia kwa kishindo, Rais wetu wa tano,
Ni kama kwenye mawindo, jinsi alitoa meno,
Wajanja likaa kando, wasijevunjwa viuno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

4:Kwanza hamia Dodoma, na tena haraka mno,
Na endapo ukigoma, kazi serikalini no,
Umestawi Dodoma, mambo yetu ni mswano,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

5:Pili Bwawa la umeme, huko alitia neno,
Tutosheke kwa umeme, wengi tuwape mikono,
Acha watu wajitume, sasa tuko mbali mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

6:Tatu reli ya kisasa, mradi mkubwa mno,
Hakuyafanya makosa, vitendo kwenye maneno,
Sasa ni kubwa fursa, usafiri bora mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

7:Nne nidhamu kazini, ni vitendo si maneno,
Uzembe sasa kapuni, usije kuumwa meno,
Kwa kazi wako mbioni, wala hakuna miguno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

8:UVIKO ilipokuja, aligangamala mno,
Alitujengea hoja, madawa tukasema no,
Jambo wengine uteja, uliwasumbua mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

9:Imani kujifukiza, kwetu lienea mno,
Wengine ilitutunza, walakini wengine no,
Kama alituumiza, nia yake njema mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

10:Katika kipindi chake, waliminywaminywa mno,
Kilitamba chama chake, vingine mingi miguno,
Kingebaki peke yake, muda ungepita mno,
Twashereheka Uhuru, tuseme hapa kazi tu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news