NA ADELADIUS MAKWEGA
DESEMBA 27, 2022 kuna pahala alikuwapo mwanakwetu ambapo alikuwa anachapa matini yake simulizi yenye kichwa ”Upimaji wa Lolote Kwa Haki”, akiwa hapo aliingia ndugu mmoja akamsalimu akimwambia maneno haya.
“Siku hizi mimi nakaa jirani na wewe chukua namba yangu na kila unapotoka kwako tuwe tunaondoka pamoja.”
Kwa kuwa huyu ndugu ana gari, maneno hayo yalikuwa ni jambo jena sana kwa mwanakwetu. Ndugu huyu akiwa hapo alimuuliza mwanakwetu suala lingine,
“Hivi pale kwako unafuga nini?” Mwanakwetu alijibu kuwa yeye anafuga bata tu, “Vipi mbona haufugi kuku?”.
Mwanakwetu alijibu kuwa kuku alijaribu kufuga sana, lakini jitihada zake ziligonga mwamba kwani kila mara akifuga wanakufa kwa magonjwa mbalimbali. Ndugu huyu akamwambia mwanakwetu,
“Kama unataka kufuga kuku jenga banda ambalo kuku watakuwa wanalala juu ya chanja na kinyesi chao kiwe kinadondoka chini maana kinyesi hicho ndiyo chenye madhara makubwa kwa ndege hawa.”
Mwanakwetu alimsikiliza ndugu huyu kwa makini na moyo wa kurudia ufugaji wa kuku ulirudi wakati huo huo.
“Unajua kuku mmoja akiwa mgonjwa, wenzake wote wanamsogelea na kumzunguka wakimsikitikia kuku huyo kwa kuugua hadi anafariki na hapo wanapokuwa jirani na kuku mwezao ndipo wanapoambukizwa magonjwa. Kaka jambo hili lilivyo kwa ndege hawa ni sawa na binadamu kwa binadamu mwezake anapopata shida wanasikitika naye pamoja.”
Ndugu huyu alitoka na mwanakwetu kuendelea na kazi ya kuiandika matini hiyo hadi kumalizika na kukufikia wewe msomaji mwenye thamani kubwa huko ulipo.
Kwa wale wafuatiliaji wa mambo wanawashauriwa sana kutumia muda ulioutaja katika matini haya kujua nani ni nani wakati huo, japokuwa katika baadhi aya mwanakwetu ameweza kuwataja kwa majina yao ya kweli, vyeo vyao vya kweli na hata majina kificho kwa kiasi kidogo.
Mwanakwetu alimuita Dkt.Abdul akimwambia atayarishe makabidhiano na amuachie Dkt.Easter Bashasha na yeye apate nakala ambayo Dkt.Bashasha atamkabidhi Mganga Mkuu mpya wa wilaya atakapofika hapo kituo chake kipya, watumishi wengine wa Idara ya Afya Wilayani hapo walishikwa na bumbuwazi kama la wale ndege.
“Unajua kuku mmoja akiwa mgonjwa, wenzake wote wanamsogelea na kumzunguka wakimsikitikia kuku huyo kwa kuugua hadi anafariki na hapo wanapokuwa jirani na kuku mwezao ndipo wanapoambukizwa magonjwa. Kaka jambo hili lilivyo kwa ndege hawa ni sawa na binadamu kwa binadamu mwezake anapopata shida wanasikitika naye pamoja.”
Mwanakwetu akiwa na Dkt.Abdul walizungumza mengi ya kutiana moyo likiwamo hili, “Daktari usikate tamaa, sisi sote ni Watanzania, tumejikuta tumezaliwa hapa, usikate tamaa kabisa kabisa, tambua kuwa wewe bado daktari wa binadamu, nenda kaendelee kuwatibu Watanzania wenzetu, kwa moyo wako wote na maisha yanaendelea hayawezi kurudi nyuma na hayupo anaweza kukupokonya udaktari wako wa binadamu, nenda kafanye kazi.”
Dkt.huyu aliaga na kuondoka kuripoti Kilimanjaro na baadaye alirudi kuonana na Mganga Mkuu mpya wa Wilaya ya Mbozi na pia akapita kwa mwanakwetu kumuaga kwa mara nyingine na kuondoka zake Kilimanajaro. Kwa sasa bado mwanakwetu hafahamu alipo Dkt.Abdul.
Kumbuka katika matini ya kwanza mwanakwetu alisimulia alipoonana na Dkt.Zainab Chaula ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya) mwanakwetu ametumia mficho sana mazungumzo haya kwa sababu nyingi, lakini leo mwanakwetu anakupa moja ambalo Dkt.Chaula alimwambia, “Tunafahamu fika namna Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe anavyojitahidi kufanya kazi katika mkoa ule.”Baadaye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe wakati huo yalimkuta kama ya Dkt.Abdul.
Kumbuka mwanakwetu alifika ofisini kwa bwana mkubwa yule aliyepima kwa kigezo kimoja.“Nakwambia mwanakwetu hii nchi ina wenyewe.”
Mwanakwetu akashangaza sana na maneno hayo, akajibu akisema kuwa nchi hii mwenyewe ni bibi na bwana kama unavyowaona katika nembo ya taifa na bibi na bwana hao ni mimi na wewe. Siyo mtu yoyote anayeshika nafasi ya umma, huyo amepewa dhamana kwa niaba ya wengine tu.“Nakwambia mwanakwetu hii nchi ina wenyewe.”
Jamaa aliendelea kusisitiza hilo naye mwanakwetu alisema kuwa wote waliopo katika ofisi za umma iwe mkubwa au mdogo wao wamepewa dhamana katika nafasi mbalimbali kwa muda fulani tu.
Mwanakwetu akasema huyu anayemtaja mwenyewe anaweza kujitokeza hadharani aseme kuwa yeye ndiye mwenyewe? Jibu halikupatikana.“Kwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inyaozingatia misingi ya UHURU, HAKI, UDUGU na AMANI.” Hivyo ndivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyonadi kwetu sote.
Kwa hisani yako msomaji, mwanakwetu anakuomba aifunge hii simulizi ya Dkt.Abdul aliyewahi kuwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe ambaye alijitoa kwa dhati na moyo wake wote katika ujenzi wa vituo vya afya katika eneo hilo.
makwadeladius@gmail.com
0717649257