NA LWAGA MWAMBANDE
HIVI karibuni, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alisisitiza kuwa, maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, hivyo mwanadamu anapaswa kuwa hadithi nzuri ili watu waweze kukusimulia.
Wito wa Mzee Mwinyi unakuja katika kipindi ambacho ulimwengu wa sasa unakabiliwa na wingi wa watu ambao iwapo litatokea jambo lolote, muda wowote na kuondoka duniani hana la kusimuliwa kwa vizazi vijavyo kutokana na namna ambavyo tumejitengenezea mazingira yasiyompendeza Mungu na hata mwanadamu.
Ni kutokana na ukweli kuwa, wengi wetu tumepungukiwa na hekima, tumekuwa na roho ya ubinafsi na choyo, chuki na hata wakati mwingine tunatamani mwingine aanguke ili sisi tuweze kuendelea kusonga mbele.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, jipe nafasi ya kujisahihisha, jitafakari na anza kuandaa mazingira ambayo yatakuwezesha kuwa na hadithi nzuri ambazo watu watapata kukusimulia. Endelea;
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, jipe nafasi ya kujisahihisha, jitafakari na anza kuandaa mazingira ambayo yatakuwezesha kuwa na hadithi nzuri ambazo watu watapata kukusimulia. Endelea;
1:Maisha ya mwanadamu, hadithi ulimwenguni,
Sasa ewe mwanadamu, uishie duniani,
Kwako kweli ni muhimu, soni siwe mgongoni,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
2:Hekima hii adhimu, yatujia akilini,
Toka aliyehitimu, kufikia uzeeni,
Kaishi anafahamu, yajengayo maishani,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
3:Mzee twamfahamu, na kiongozi makini,
Yake tunayafahamu, Ruksa tulibaini,
Atuonya wanadamu, maisha yasiwe duni,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
4:Wajibu wako jihimu, uyafanye ya amani,
Kwako watu wajikimu, wabakie furahani,
Hadithi yako tadumu, inasemwa midomoni,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
5:Uko hai jifahamu, ukiwapo duniani,
Ufanyayo yanadumu, huko kwa watu moyoni,
Watasema humuhumu, ukienda kaburini,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
6:Kuliza watu kidumu, machozi kwao shavuni,
Au kuwalisha sumu, hadi hospitalini,
Kesho yako jua ngumu, hapa na hata mbinguni,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
7:Sauti ya wanadamu, ni ya Mungu wa mbinguni,
Kwake wale wanadumu, kila siku ibadani,
Ndio watasema humu, livyoishi duniani,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
8:Acha watu walaumu, haki ikiwa enzini,
Mwenyewe unafahamu, uko huru nafsini,
Na Mungu akufahamu, kufika ndani moyoni,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
9:Kama ujana wadumu, una siku duniani,
Mema yafanye kwa zamu, usitopee dhambini,
Mzee Mwinyi salamu, zikufikie nyumbani,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
10:Kama mzee elimu, ikuingie kichwani,
Wala usijilaumu, uliyoyafanya ya chini,
Unao mwili na damu, uingie magotini,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
11:Mwisho mwema unadumu, ambao una thamani,
Wewe anza kuhudumu, yaandikwe kitabuni,
Ya zama hayatadumu, haya yakiwa kichwani,
Uwe ni hadithi nzuri, watu wakusimulie.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602