NA MWANDISHI WETU
CHUO cha Tehama VETA Kipawa kimesema kuwa Sekta ya Tehama nchini inakua kwa kasi, hivyo vijana wana fursa ya kupata mafunzo na ujuzi katika eneo hilo na kuweza kutoa mchango kwa taifa na kwa mtu mmoja mmoja.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Tehama Kipawa, Mhandisi Sospeter Mkasanga wakati wa mahafali ya 11 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye viwanja vya VETA Kipawa jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Tehama VETA Kipawa, Mhandisi Sospeter Mkasanga akitoa maelezo kuhusiana mafunzo yanayotolewa na chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Mkasanga amesema kuwa, chuo hicho kimeanzisha kozi bobevu kwa ajili ya Tehama kwa wanafunzi kusoma kitu kimoja tu ambapo inafanya kuwa mahiri kwenye ujuzi wa eneo husika.
Mhandisi Mkasanga amesema kuwa, wakati wa sasa ni fursa kwa vijana wa kitanzania kosoma kozi bobevu kutokana na uchumi unabadilika ambao unahitaji kuwa na mifumo ya Tehama katika kurahisisha kufanya kazi za watu 100 basi kufanya watu 50 na soko la Tehama liko wazi.
Mmoja wa wazazi katika Mahafali ya 11 ya Chuo cha Tehama VETA Kipawa, Everister Ndunguru akitoa Rai kwa wahitimu wa chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo amesema kuwa, vijana wanaosoma Chuo cha VETA Kipawa asilimia 70 wanahitimu wakiwa na kazi ya mkononi na hiyo inatokea pale tu wanapokuwa wamekwenda kwenye mafunzo ya vitendo.
Aidha, amesema kuwa chuo kinaendelea kutafuta mashine ya za kisasa za kujifunzia kutokana na teknolojia yake kubadilika kila wakati hivyo kunahitaji kwenda sambamba na Teknolojia.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Angelus Ngonyani akizungumza katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Tehama VETA Kipawa yaliyofanyika kwenye chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mgeni rasmi katika mahafali ya 11 ya Chuo cha VETA Kipawa Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Angelus Ngonyani amesema kuwa VETA Kipawa wanahitaji kufanya tafiti katika soko la Tehama pamoja na kufanya kozi bobevu kuwa na vijana wengi zaidi kutokana mahitaji yaliyopo katika nchi.
Ngonyani amesema kuwa VETA kipawa katika kufikia maendeleo kunatakiwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo na wenye viwanda ambao vijana waliopata elimu ya ufundi wanatakiwa kwenda huko
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kipawa, Albert Otieno akizungumza kuhusiana na umhimu wa chuo hicho kwa wakazi wa Kipawa kwenye mahafali ya 11 Chuo cha Tehama VETA Kipawa jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa katika eneo la kilichopo chuo, Albert Otieno amesema kuwa wananchi wanapaswa kutambua chuo VETA Kipawa ni mkombozi kwa vijana katika kupata elimu ambayo kwa sasa ndio mahitaji kwenye soko.