NA DIRAMAKINI
LICHA ya Serikali kutumia zaidi ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Msingi Mwisenge iliyopo Manispaa ya Musoma bweni hilo halijaanza kutumika kutokana na kukosekana kwa vitanda na magodoro.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwisenge, Sigawa Thomas wakati akipokea msaada wa magodoro na runinga kutoka kwa wafanyakazi wa Benki ya NMB kutoka matawi yote ya Mkoa wa Mara.
"Hili bweni ni la wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalum lina uwezo wa kulaza wanafunzi 80 halijaanza kutumika kutokana na kukosekana kwa vitanda na magodoro,"amesema.
Amesema kuwa, kutokana na bweni hilo kutokutumika wanafunzi wote 120 wenye mahitaji maalum wanalazimika kutumia mabweni ya zamani ambayo mengine yamechakaa, hivyo kuwashukuru wafanyakazi hao kwa msaada huo ambao amesema umekuja muda muafaka.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi hao,Meneja wa NMB tawi la Tarime, Victorin Kiamrio amesema kuwa, msada huo umetolewa na wafanyakazi hao ikiwa ni sehemu ya ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika.
Amefafanua kuwa, wafanyakazi hao waliamua kuchanga fedha na kununua magodoro 80, runinga ya kisasa pamoja na king'amuzi vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.2 kwa ajili ya wanafunzi hao ambao ni wasioona, wenye mtindio wa ubongo, wenye ualbino pamoja na wenye ulemavu wa viungo.
"Tukiwa tunaadhimisha miaka 61 ya Uhuru sote kwa umoja wetu tuliamua kufanya jambo japo kidogo kwa ajili ya jamii ambapo tuliona ni vema tukalikumbuka kundi hili la watoto wenye mahitaji maalum ingawa tumetoa kidogo lakini tunafurahi kuwa tumeweza kuwafikia watoto hawa na hiki tulichokitoa kina mchango katika kufikia malengo yao ya kielimu,"amesema.
Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo amewashukuru wafanyakazi hao kwa msaada huo ambao amesema kuwa umetolewa wakati muafaka.
"Tulikuwa tunawaza namna ya kupata vifaa vya humu ndani na nipende tu kutoa taarifa kuwa baada ya nyie kutoa taarifa juu ya kusudio lenu la kutupatia magodoro tayari kuna mdau naye ameahidi kutupatia vitanda vyote kwa ajili ya bweni hili na muda wowote vitanda hivyo vitaletwa hivyo bweni letu litakuwa tayari kutumika mwakani,"amesema Gumbo.
Bweni hilo ambalo limekamilika mwezi Agosti, mwaka jana lilijengwa kufuatia agizo alilolitoa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dkt.John Magufuli alipofanya ziara mkoani Mara mwezi Septemba 2018 ambapo aliagiza wizara zinazohusika kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo ambapo yeye alitoa kiasi cha shilingi milioni 20 kwa ajili ya ukarabati huo ikiwa ni njia moja wapo ya kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyesoma shuleni hapo.