Wamegewa maarifa namna ya kukabiliana na utakatishaji fedha haramu, vitendo vya kigaidi

NA DIRAMAKINI

NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi.Sauda Msemo ameongoza Semina ya Kupambana na Utakatishaji wa Fedha Haramu na Kupambana na Ufadhili wa Ugaidi (AML/CFT) kwa Wakala wa Bima,Wasimamizi wa Masoko ya Mitaji na Waendeshaji Mitandao ya Simu nchini.
Sekta ya Fedha nchini inatajwa kuwa ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi imara na mara zote huwa inategemewa kutoa mchango chanya katika kuwezesha wananchi kupata huduma na mikopo hasa ya uzalishaji.

Aidha, semina hiyo inakuja wakati mwafaka ambapo kama tunavyofahamu maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia urahisi wa kusafirisha fedha au kuhamisha fedha kutoka mahali kwenda mahali kwingine.

Shughuli za wanadamu, serikali na taasisi binafsi zimekuwa zikijihusisha katika miradi mikubwa ya maendeleo au uchimbaji wa rasilimali kwenye ardhi kama madini na gesi asilia au miradi ya ujenzi ya miundombinu na masuala ya umeme.

Maeneo haya yote yanahitaji kiwango kikubwa cha fedha. Hapa ndipo watumishi au wawekezaji wasio waaminifu wanatoa na kupokea rushwa ili kufanya maamuzi fulani ya kupendelea. Rushwa hizi ni za kiwango kikubwa cha fedha au maslahi kwenye mali fulani au mradi.

Wanaopata fedha hizi kupitia njia haramu huwa wanatafuta njia kadhaa za kuzifanya fedha au mali zao kuonekana kuwa ni halali na wakati mwingine huweza kuzitumia kufadhili matukio ya kigaidi kwa maslahi yao. 

Ndiyo maana Serikali nyingi Duniani ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeanzisha mfumo wa sheria wa kuweza kuzuia utakatishaji wa fedha au mali haramu.
Semina hiyo ambayo imeandaliwa na Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit) imefanyika Ofisi ndogo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ikiwa inakusudia kuongeza uelewa juu ya Majukumu ya Ufadhili wa Kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu na Kupambana na Ufadhili wa Ugaidi.

FIU kinawajibika katika kupokea, kuchanganua na kusambaza taarifa zote za miamala yenye mashaka na taarifa muhimu zinazohusiana na utakatishaji wa fedha haramu au taarifa za ufadhili wa ugaidi zilizotelewa na mtoa taarifa au vyanzo vingine ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, semina hiyo imeundwa ili kutoa maarifa muhimu katika AML/CFT/CFP na dhana za mbinu za kutegemea hatari, kuelewa utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi na hatari mbalimbali zinazokabili mifumo yetu ya kifedha, pamoja na kurekebisha mazoea yanayohusiana na kuzuia na kugundua Utakatishaji wa Fedha au Ufadhili wa Ugaidi.

Kwa nini BoT?

Kwa sababu,Benki Kuu ya Tanzania ina mamlaka ya kutoa leseni, kudhibiti na kusimamia benki na taasisi za fedha zikiwemo benki za biashara, taasisi za huduma ndogo za fedha, benki za jamii, benki za maendeleo, kampuni za karadha, taasisi za mikopo ya nyumba.

Pia watoa huduma ndogo za fedha, taasisi za taarifa za wakopaji, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na ofisi za uwakilishi za benki zilizoko.

Benki Kuu pia ina wajibu wa udhibiti na usimamizi wa masuala ya kifedha (uwekezaji) wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini Tanzania.
Jukumu la msingi katika udhibiti na usimamizi wa taasisi za fedha ni kuhakikisha kuna uthabiti, usalama na ufanisi wa mfumo wa fedha na kupunguza uwezekano wa wenye amana kupata hasara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news