Watakiwa kuchukua taadhari dhidi ya wageni kuepusha ukatili kwa watoto

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wametakiwa kuwa makini na baadhi ya wageni wasiokuwa waaminifu wanaofika katika nyumba zao na kufanya ukatili dhidi ya watoto.
Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 10,2022 na Katibu Tawala Wilaya ya Musoma, Justine Manko kupitia hotuba yake iliyosomwa na Afisa Elimu Msingi wa Wilaya hiyo, Mwalimu Elizabeth Paulo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika Mugango wilayani humo.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema, "kila uhai unathamani tokomeza mauaji ya wanawake na watoto."

Ambapo kila mwaka kampeni hiyo hufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10, ikilenga kubadilishana taarifa na uzoefu, kujengeana uwezo wa pamoja katika kuunganisha nguvu na ushirikiano wa asasi za kijamii katika kuhamasisha, kueleweshana na kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.
Kupitia hotuba hiyo, Manko amesema, vitendo vya ukatili wa kijinsia vinafanywa na watu wa karibu katika jamii huku jamii imekuwa ikifumbia macho na kuona matukio hayo kama mambo ya kawaida ambapo madhara yake ni pamoja na kuongezeka kwa watoto yatima, watu wenye ulemavu na matukio ya mauaji.

Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo wa wilaya amewaagiza viongozi wa Serikali ngazi za kata, mitaa, vijiji na vitongoji kufuatilia na kuhakikisha uanzishwaji wa Kamati za MTAKUWWA na zifanye kazi pamoja na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto ndani na nje ya shule.

"Kuweni makini na wageni wanaoingia vijijini ikiwezekana anzisheni registers za wakazi na wageni ili waingiapo wajisajili ili kujua wamekuja kwa malengo gani. Hii itasaidia kudhibiti wizi wa watoto na matukio ya ukatili yanayofanywa na watu wasiojulikana," amesema Manko Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya ukatili katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Tanna Nyabange amesema kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 matukio 12,612 ya vitendo vya ukatili yaliripotiwa.

Akielezea mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Tanna amesema halmashauri imejipanga kuhuisha kamati za Ulinzi wa Mama na Mtoto (MTAKUWWA) katika kata zote za wilaya hiyo kamati ambazo zina wajibu wa kulinda ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Mikakati mingine ni pamoja na kuanzisha Madawati ya Ulinzi na Usalama wa mtoto ndani na nje ya shule na kushirikisha wananchi na wadau wote katika kupambana na vitendo hivyo.

Afisa Maendeleo huyo amesema anatambua na kuthamini miradi inayotekelezwa na wadau ukiwemo mradi wa "FUNGUKA PAZA SAUTI KUPINGA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA ULIOZOELEKA" ambao unatekelezwa na Shirika la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) unaotekelezwa kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society katika maeneo ya uvuvi.

"Katika kuimarisha uchumi wa kaya, vikundi 26 vya kijamii vimepatiwa mafunzo ya usindikaji wa chakula, utengenezaji wa batiki na uboreshaji wa bidhaa" amesema Thana.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa "Funguka paza sauti kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia uliozoeleka" kutoka Shirika la VIFAFIO, Robinson Wangaso ameishauri jamii kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pindi kunapoonekana kuna viasharia vya ukatili ili hatua zichukuliwe haraka badala ya kusubiria matukio ynapotokea kwani kufanya hivyo kutapunguza matukio hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news