WAZEE, RAFIKI ZETU WAJUKUU-ANNA MKAPA

NA ADELADIUS MAKWEGA

MJANE wa marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, Bi.Anna Mkapa ametembelewa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na Baba Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu Joseph Jally kumjulia hali wakati huu wa kuelekea Sikukuu ya Krisimasi na mwisho wa mwaka.
Akizungumza mbele ya ugeni huo, Mama Mkapa alishukuru sana kwa kutembelewa nyumbani kwake na kusema kuwa, “Baba Askofu asante kwa kunikumbuka kunitembelea na bado ninakumbuka miradi yenu kadhaa tuliyowahi kuitembelea ikiwemo shule zenu za sekondari, mimi sasa ni mzee na rafiki zangu wa karibu ni wajukuu ambao nakuwa nao mara nyingi wakati kama huu wa sikukuu na mwisho wa mwaka hapa nyumbani.”

Kwa upande wake Baba Askofu mstaafu Joseph Jally alisema kuwa,”Anamshukuru sana mama Anna Mkapa kwa kuwapokea nyumbani kwake na anamkumbuka sana kwani Marehemu Rais Benjamin Mkapa enzi za uhai wake na mama Anna Mkapa waliwahi kuitembelea Dayosisi yao katika kukagua, kuzindua na kushirikiana nao miradi kadhaa ya kijamii.”

Mazungumzo haya kwa sehemu kubwa yalilenga masuala ya kiimani na juu ya kuelekea sikukuu ya Krisimasi na mwaka mpya, sala na maombi ambayo yakimkumbuka pia Marehemu Rais Benjamin Mkapa.

Baba Askofu Mstaafu Jally aliyeambatana na mkewe, Bi.Sara Jally na wanafamilia wengine aliiongoza Dayosisi ya Kaskazini Mashariki baada ya kufariki Baba Askofu Sebastian Kolowa mwaka 1992 na mwaka 1993 baadaye ndiyo akachaguliwa kuiongoza Dayosisi hii hadi anastaafu mwaka 2001 ambapo nafasi hiyo ilichukuliwa na Baba Askofu Stephern Munga (2002-2021) na sasa Dayosisi hii inaongozwa na Baba Askofu Msafiri Mbilu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news