NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Dkt. Patrice Serafin ahakikishe ifikapo Januari Mosi , 2023 hospitali hiyo iwe imeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Waziri Mkuu Kassim ametoa agizo hilo Disemba 12, 2022 baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambayo inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 12.4 itakapokamilika na imefikia asilimia 92 ya ujenzi.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Meneja wa TANESCO mkoa wa Katavi kuhakikisha ifikapo Disemba 23, 2022 awe amefikisha huduma ya umeme katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutawezesha kulaza wagonjwa 170 na hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa jamii.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amedhamiria kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
“Dhamira hii njema ya Rais Dkt. Samia tunaiona na ndio maana hapa manispaa ya Mpanda kunajengwa vituo vya afya vitano na vipo katika hatua ya umaliziaji, pia ametoa shilingi milioni 150 kwa ajili ujenzi wa zahanati.”