Waziri Mkuu atoa wito kwa wadau mbalimbali kuhusu lishe bora nchini

NA FRESHA KINASA

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa rai kwa taasisi mbalimbali za utafiti nchini zihakikishe zinafanya tafiti za kimkakati zitakazosaidia kukabili tatizo la lishe katika kuandaa taifa la watu wenye afya bora watakaoleta maendeleo katika sekta mbalimbali.



Hayo yamesemwa leo Desemba 6, 2022 na Waziri Mkuu kupitia hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima wakati akihutubia Wananchi na Viongozi mbalimbali wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa lishe Tanzania uliofanyika katika Uwanja wa Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Amesema kuwa,katika kuhakikisha tatizo la utapiamlo linakabiliwa kuna haja kubwa ya watafiti kuwa na mikakati madhubuti inayokuja na majawabu sahihi ya kusaidia jamii kuwa na watu wenye afya bora wasio na matatizo ya afya ya akili na udumavu.
Pia, ameziagiza taasisi mbalimbali za serikali kujitahidi kutoa elimu juu ya umuhimu wa lishe bora kwa jamii kwa kuzingatia ulaji bora wa makundi ya vyakula kwa wajawazito, watoto wadogo na walio katika umri wa kuzaa kwani kufanya hivyo kutaifanya jamii kuwa bora.

Aidha, ameagiza TAMISEMI isimamie kikamilifu sekretarieti za mikoa kwa kuhakikisha zinatekeleza vyema mpango wa lishe sambamba na Mikoa na Halmashauri zitumie vyema muongozo wa kitaifa wa lishe mashuleni.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Kasper Mmuya amesema kwamba mkutano ulifanyika wa wataalam na wadau wa lishe pamoja na taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayojishughulisha na afua za lishe ambao umefanyika Desemba 5 hadi Desemba 6, 2022 umewezesha kujadiliana mambo mbalimbali na kupata maadhimio manne yatakayosaidia kuimarisha lishe.

Pia wameweza kutoa miche ya miti ya matunda 300 katika Manispaa ya Musoma ili ipandwe kwa lengo la kuhamasisha ulaji wa matunda na mbogamboga kwa lengo la kukabiliana na tatizo la lishe ambapo pia waliweza kupanda miche ya matunda katika Shule ya Msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.
Naye Mbunge Ester Matiko akizungumza kwa niaba ya Wabunge vinara wa lishe amesema, wabunge vinara wa lishe watahakikisha wanaishauri serikali kusudi iweze kupeleka wataalam wa lishe ngazi za chini kama ilivyoweza katika zingine kusudi wasaidie kuleta ufanisi katika utekelezaji wa afua za lishe.

Pia, Matiko amesema kwamba Bunge litahakikisha wizara 14 ambazo zipo kwenye mpango huo zinatekeleza mpango huo kwa nafasi yake katika kuhakikisha kwamba watoto wa Kitanzania wanaondokana na udumavu na utapiamlo.

Ameongeza kuwa, baadhi ya Halmashauri zimekuwa zikishindwa kutoa fedha Shilingi 1000 kwa ajili ya lishe kutokana na kutokuwa na utoshelevu wa fedha,hivyo ameomba jitihada zifanyike kutekeleza jambo hilo na kwamba Serikali iendelee kutekeleza afua za lishe kwa kushirikiana na Wadau wote kwani ni muhimu kwa kuwaanda watu wenye lishe bora watakao leta maendeleo nchini.

Aidha,Matiko amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amezidi kuwa hodari na kusimamia kidete suala la lishe nchini.
Abdallah Ulega akiongeza kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema kwamba, unywaji wa maziwa uko chini ambapo kwa sasa mtu mmoja hutumia lita 63 badala ya lita 200 kwa mtu kwa mwaka kwa mjibu wa Shirika la Chakula Duniani ( FAO.)

Amesema, ulaji wa nyama kwa sasa ni kilo 15 wakati kiwango kinachotakiwa kwa mtu mmoja ni kilo 50. Ulaji wa samaki kwa sasa ni kilo 8.5 kwa mtu mmoja kwa mwaka ambapo kiwango kinachotakiwa ni kilo 23 kwa mtu mmoja kwa mwaka. Huku ulaji wa kuku na mayai akisema si wa kuridhisha kwani huliwa na watu wenye kipato cha kati na juu katika maeneo ya Mjini.

Ameongeza kuwa, Wizara hiyo itaendelea kutekeleza afua mbalimbali na kuhamasisha ulaji na utumiani wa mazao ya mifugo na uvuvi katika majukwaa mbalimbali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuondokana na tatizo la lishe.
Mheshimiwa Ulega amemshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti upande wa mifugo ambapo yapo mambo mbalimbali wamepanga kuyafanya ikiwemo kutengeneza vituo vya ukusanyaji wa maziwa ili yakusanywe na kusindikwa kusaidia lishe bora pamoja na kununua mitamba bora na madume yasambazwe nchi nzima kuongeza tija kwa ngombe zilizopo.

Pia amesema katika kuleta ufanisi katika lishe wamepanga kuendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa kutoka lita sitini na nne hadi 100, kuongeza shule zinazokunywa maziwa kutoka shule 39 hadi 5000 nchi nzima, kuongeza ulaji wa nyama kutoka kilo 14 hadi 25, ulaji wa samaki kutoka kilo 8.5 hadi 10.5.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema, wizara hiyo imejipanga kuendeleza uzalishaji wa vyakula ili kuleta ufanisi ambapo amewashauri Watanzania kuendelea kuzingatia ulaji bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news