Waziri Mkuu azindua Kituo Kikuu cha Polisi Ruangwa

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua kituo Kikuu cha Polisi cha wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na amesema kuwa jengo hilo linalenga kuboresha utendaji wa polisi hususani katika ulinzi wa raia na mali zao.
Muonekano wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Ruangwa ambacho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekizindua Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi, Disemba 31, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amezindua jengo hilo leo Desemba 31, 2022 ambapo amesema mbali na kuboresha utendaji wa polisi pia jengo hilo litawarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuwapunguzia gharama za kutembelea umbali mrefu kufuata huduma.

Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekabidhi pikipiki mbili kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini kwa ajili ya kituo hicho pamoja na kituo kidogo cha Ndagala. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 190.
“Hatua hii ni lazima tumshukuri Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo haya”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 99 na kwamba katika mwaka ujao wa fedha wizara inakusudia kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za awali za askari wa kituo hicho.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ameiomba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ifanye maboresho ya makazi ya askari katika mkoa huo ili waweze kuishi katika mazingira bora Zaidi yatakayowawezesha kutekeleza majuku yao ipasavyo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekabidhi pikipiki 25 kwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ruangwa ili ziweze kuwasaidia makatibu wa kata katika kufuatilia utekelezaji wa Ilani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news