NA LUSAJO MWAKABUKU
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka wajasiriamali walioshiriki maonesho ya Juakali Kampala Uganda kuongeza ubunifu ili waweze kufanya makubwa Zaidi kwani uwezo wa kufanya hivyo wanao kutokana na kazi wanazozionesha.
Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za SIKU YA TANZANIA (TANZANIA DAY) kwenye maonesho ya maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
“Nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na nimefurahishwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali. Kwa kweli, bidhaa zilizopo zinaonyesha kwamba wananchi wetu wengi ni wabunifu na wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi kama watapewa fursa ya kufanya hivyo. Ninawapongeza sana kwa ubunifu na kwa kuzalisha bidhaa hizi ambazo nyingi ni nzuri na zinavutia. Hata hivyo ninawashauri wajasiriamali muwe wabunifu zaidi kwa kuzingatia kwamba biashara ni ushindani,” alisema Waziri Riziki Pembe Juma.
Maadhimisho ya TANZANIA DAY yaliambatana na shughuli mbalimbali zilizofanywa na wajariamali wa Tanzania kwa lengo la kucherehesha maonesho na kuonesha utamaduni wa Tanzania pamoja na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini. Miongoni mwa shuguli zilizofanywa ni pamoja na maonesho ya mavazi ya asili, maonesho ya vito vya thamani na madini, vyakula vya asilia, ngoma za asili na muziki.
Akizungumza na maelfu ya washiriki wa maonesho hayo Waziri Riziki Juma Pembe mbali na kutoa wito kwa wana Jumuiya kununua bidhaa za ndani alielezea hatua mbalimbali zinazo endelea chukuliwa na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutatua changamoto zinazowakabili wajariamali, ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania amezitaja hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na; kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kuanzisha maeneo maaalum ya kufanyia biashara na kutoa elimu ya ujasiriamali.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akifurahia muziki wa asili uliokuwa ukipigwa wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.
“Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kuhakikisha wajasiriamali hawa hawaendelei kubaki wadogo bali wanapaswa kukua ili waweze kushiriki katika sekta rasmi kama wajasiriamali wakubwa.
"Vilevile kwa kushirikia na Sekretarieti ya Jumuiya tutahakikisha maonesho haya yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuwapatia fursa wajasiriamali wa sekta hii ili waweze kutambua fursa zilizopo katika nchi zetu na kushiriki katika uzalishaji na maendeleo ya nchi zetu,"alieleza Waziri Riziki Pembe Juma.
Hii ni mara ya tano kwa Jamhuri ya Uganda kuwa mwenyeji wa maonesho haya tokea kuanzishwa kwake mwaka 1999.