NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene amezindua Programu ya Education Plus inayolenga kuhakisha vijana balehe (wasichana na wavulana) wanawezeshwa kuishi maisha salama, yenye afya, na tija-bila ukatili wa kijinsia, VVU na UKIMWI.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akizindua Mpango wa Education Plus katika kilele cha shughuli za vijana kuelekea Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Lindi. (Picha na OWM).
Ametumia fursa hiyo kuwaasa vijana wote nchini kuzingatia jitihada za Serikali katika mapambano ya VVU na UKIMWI kwa kuendelea kujilinda na kulinda wengine huku wakijiepusha na tabia hatarishi.
“Rai yangu kwa vijana wote nchini, hususani wasichana, fanyeni kila muwezalo ikiwa ni pamoja na kuzingatia maudhui ya kampeni mbalimbali ili kujikinga na maambukizi ya VVU. Wale mlio shuleni na vyuoni hakikisheni mnaweka mkazo katika elimu na kujiepusha na tabia zote hatarishi zinazopelekea kupata maambukizi ya VVU,”amesema Waziri Simbachawene.

Akieleza hali ya maambukizi nchini Waziri Simbachawene amesema katika kuelekea lengo la sifuri ya maambukizo mapya, kama nchi maambukizo mapya yameendelea kushuka mwaka hadi mwaka, japokuwa sio kwa kasi ya kuridhisha. Kwani, hadi sasa takwimu zinaonesha kuwa takribani watu 54,000 waliambukizwa VVU mwaka 2021 nchini. Hii ni sawa na takribani watu 4,500 kwa mwezi au watu 150 kwa siku.
“Vijana wenye umri wa miaka 15-24 ndio kundi ambalo linaonyesha kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizo mapya, kwani katika watu wote wanaopata maambukizo mapya ya VVU kila mwaka, takribani asilimia 30 ni vijana wenye umri wa miaka 15-24 (yaani katika kila watu 10 wanaopata maambukizo mapya ya VVU watatu ni vijana wa umri huu),”amesisitiza.